Bashungwa ataja maeneo manne kushirikiana waigizaji wa India na Tanzania

Wednesday November 10 2021
bashungapic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam.Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, ameyataja maeneo matano ambayo waigizaji kutoka nchini Tanzania na wale wa India wataweza kushirikiana katika kusogeza sanaa hiyo mbele.

Bashungwa ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 10,2021 wakati muigizaji maarufu kutoka nchni India, Sanjay Dutt, ambaye yupo nchini humo alipokutana na wasanii wa filamu na viongozi kutoka serikali wanaosimama sekta ya filamu.

Licha ya kufurahia ugeni huo, Bashungwa amesema kuna maeneo manne anayodhani ni vema wasanii wa nchi hizo wakishirikiana wataweza kufurahia vipaji vya filamu vilivyopo pande zote.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na utayarishaji filamu pamoja kwa kutumia mandhari zinazopatikana katika nchi zote mbili.

“Kwa kuandaa filamu pamoja kwa wasanii wetu, itapanua wigo wa mahitaji ya bidhaa hizi kwa jamii za pande zote mbili yaani Tanzania na India hali ambayo itapelekea kuongezeka kwa soko la bidhaa za filamu,”amesema Bashungwa.

Eneo jingine Waziri huyo amesema ni la usambazi au uuzwaji filamu za kitanzania ili kufikia hadhira kubwa duniani.

Advertisement

Amesema kwa sasa Tanzania huzalisha filamu 1400 kila mwaka ambazo  hutayarishwa kwa lugha ya kiswahili, lugha ambayo inazungumzwa na takribani watu milioni 150 duniani wakiwemo Diaspora wanaoshi katika nchi mbalimbali za Magharini na Mashariki ya mbali.

‘Kutokana na hali hiyo, inaaminika kuwa filamu za kiswahili zina uwezo wa kupata soko kubwa iwapo kutakuwa na mikakati mizuri ya kimasoko, jambo ambalo tasnia ya filamu hapa nchini haina,”amesema Waziri huyo.

Maeneo mengine amesema ni kuwa na jumba changamani la filamu  litakalokuwa kitovu cha shughuli mbalimbali za filamu na kuwa na miundombinu ya kisasa ya utayarishaji wa filamu kama studio za utayarishaji, sehemu za kurekodia  filamu na kumbi za sinema.

Huku eneo la nne amesema kuwa na matamasha ya tuzo za filamu  na kubainisha kuwa vipaji vya nchini humo vinahitaji fursa zaidi katika matamasha na tuzo za kimataifa kwani mpaka sasa watayarishaji wa filamu 100 wa Tanzania wameshinda tuzo mbalimbali za filamu na kati yake zaidi ya 20 ni za kimataifa.

Advertisement