Beyonce apiga 'show' dakika 90, akunja Sh56 bilioni

Muktasari:

  • Hatimaye msanii, Beyonce amerudi tena jukwaani baada ya miaka mitano kutoonekana akitumbuiza na usiku wa Januari 21 alitumbuiza huko Dubai burudani iliyochukua dakika 90.

Dubai. Mwanamuziki wa R&B wa Marekani, Beyonce Knowles-Carte maarufu (Beyonce) amefanya tamasha nchini Dubai baada ya kuwa na mapumziko ya miaka mitano ya kutofanya matamasha yake huku akikunja Sh56 bilioni za Kitanzania.

Mwimbaji huyo alilipwa kitita cha Dola 24 milioni sawa na Sh56 bilioni katika burudani aliyotoa kwa saa moja na nusu wakati wa uzinduzi hoteli ya Atlantis The Royal iliyopo Dubai.

Beyonce alifanya tamasha hilo huku kukiwa na baadhi ya masharti ya kutoruhusu mtu yeyote kupiga picha au video.
Taarifa inayopatikana katika tovuti ya TMZ imesema, Beyonce amefanya tamasha hilo usiku Jumamosi, Januari 21, 2023 lilioambatana na uzinduzi wa hoteli ya Atlantis The Royal katika Falme za Kiarabu.
Tamasha hilo lilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wasanii, wanamitindo pamoja na familia yake.
Katika tamasha hilo mashabiki wake walikuwa wanasubiri kwa hamu kuona tamasha hilo hii ni kutokana na umahiri wake wa kutumbuiza jukwaani.
Video iliyopo katika tovuti hiyo inaonyesha shangwe kubwa katika tamasha hilo lilofanyika kwa muda wa dakika 90 iliyojumuisha vibao vyake vikubwa  kama ‘Crazy In Love’, ‘Naughty Girl’, ‘Halo’ na ‘XO.’
Baada ya kumaliza onyesho hilo, ilipigwa fataki zilizochukua dakika tano kurushwa.