Beyonce atumbuiza na mwanaye jukwaa moja

What you need to know:

  • Kwa mara kwanza Beyonce alimpandisha jukwaani binti yake Blue Ivy kutumbuiza wakati wa shoo yake iliyofanyika Paris, Ufaransa jana ya Ijumaa.

Paris. ‘Kama mama, kama mtoto’ hivyo ndivyo ambavyo unaweza kusema baada ya Blue Ivy, mtoto wa kwanza wa Mwimbaji Beyonce kuonyesha uwezo mkubwa wa kuimba na kucheza baada ya mama yake kumpandisha jukwaani kwa mara ya kwanza katika shoo iliyofanyika Paris, Ufaransa jana ya Ijumaa.

Mwimbaji huyo, mwenye umri wa miaka 41, aliamsha shangwe kwa mashabiki walioghudhuria baada kumleta mtoto wake mkubwa Blue, (11) ili kucheza naye jukwaani katika ukumbi wa Stade de France.

Beyonce alionekana mwenye furaha baada ya binti yake kujiunga naye jukwaani huku Blue akidhihirisha kuwa anafuata nyayo za mama yake alipokuwa akicheza nyimbo za mama yake huku akiwaongoza wachezaji waliojumuika nao mbele ya jukwaa.

Wakati wakimaliza shoo hiyo Beyonce na Blue pamoja timu nzima waliweka ishara ya ngumi kuashiria kupinga ubaguzi wa rangi ambao watu weusi wamekua wakipitia maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Tamasha la Beyonce la Paris pia lilivutia wageni wengi mashuhuri, kwani watu kama Selena Gomez, Kris Jenner, Lenny Kravitz na Natalie Portman wote walitazama onyesho hilo.

Pia Beyonce alitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Tina Turner ambaye alikuwa nguli muziki ambaye alifariki Jumatano akiwa na umri wa miaka 83.

"Ikiwa wewe ni shabiki wangu basi wewe ni shabiki wa Tina Turner kwa sababu singekuwa kwenye jukwaa hili bila Tina Turner," alisema Beyonce katika shoo hiyo.

Kabla ya shoo, Beyoncé alimkumbuka Turner na kuandika “Ninashukuru sana kwa ushawishi wako, na njia zote ambazo ulifungua kwangu. Wewe ni mfano kwangu,”

Beyonce alitumbuiza katika jukwaa moja Tina kwenye Tuzo za 50 za Mwaka za Grammy mwaka 2008, kabla ya Tina kustaafu.