Bongo flavour ilivyompa PhD Profesa Shani

Profesa Shani Mchepange
Ukikutana naye kwa mara ya kwanza inaweza kukuwia vigumu kubaini kwamba ana uhusiano na muziki wa kizazi kipya hadi pale utakapozungumza naye.
Kwa muonekano ni mama wa makamo, anayependelea mavazi ya stara. Ni aghalabu kumuona akiwa kichwa wazi siku zote anajifunika kama ilivyo ada ya wanawake wa Pwani. Mkimya unapokutana naye kwa mara ya kwanza ila mchangamfu mno milango ya mazungumzo inapofunguliwa.
Huyu ni Profesa Shani Mchepange, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam (UDSM) na mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki).
Ndiye Mtanzania wa kwanza kufanya utafiti na kuandika andiko la kitaaluma kuhusu muziki wa kizazi kipya, maarufu kama ‘Bongo Flavour’, akijikita zaidi kuwatazama wanamuziki wanaoimba nyimbo za kufoka.
Utafiti kwenye muziki
Mapenzi yake kwenye muziki na sanaa kwa ujumla wake, ndiyo yaliyomsukuma kufanya utafiti kwenye eneo hilo, hasa baada ya kubaini licha ya muziki wa kizazi kipya kupendwa na wanajamii, hakuna tafiti za kutosha za kitalaam ambazo zimefanyika kuuangazia.
Kilichomshtua zaidi Profesa Shani ni kuona taswira hasi inayobebeshwa juu ya muziki huo, ilhali kuna watafiti wengi kutoka vyuo vikuu vya nje, wanaokuja nchini kufanya utafiti kuhusu muziki huo, huku kukiwa hakuna rejea za zilizofanyika ndani, hivyo kuanzia mwaka 2005 hadi 2009 aliamua kufanya utafiti katika eneo hilo.
“Nakumbuka PhD yangu nilianza kufanya mwaka 2005 na nilitaka nifanye kitu tofauti, hivyo nikafikiria eneo la sanaa, wakati huo muziki wa kizazi kipya ndiyo ulikuwa umeshika kasi nikaona nijikite upande wa hip hop. Nilipofuatilia nikabaini wengi waliofanyia utafiti eneo hili walitoka nje ya nchi.
Nikamshirikisha mwalimu wangu Profesa Senkoro kuhusu wazo hili, alinitia moyo ikizingatiwa kwamba hata machapisho hayakuwepo ilikuwa vigumu kupata marejeleo,” anasema Profesa Shani.
Ujasiri aliopewa na mwalimu wake ukazidi kumpa shauku ya kutaka kuchimba kuhusu muziki huo ndipo mwaka 2009 alipokuja na utafiti uliobebwa na kichwa cha habari ‘Nafasi ya muziki wa hip hop kama fasihi pendwa’ akiangalia kazi za wanamuziki wanne: Profesa Jay, Afande Sele, Zay B na Sister P.
Kutokana na kukosekana kwa marejeleo kuhusu muziki huo hapa nchini ilimlazimu kwenda nchini Marekani kwa muda wa mwaka mmoja kwa ajili ya kukusanya takwimu na taarifa kwa kina na hatimaye ikafika wakati wa kuwasilisha na kutetea utafiti wake.
“Niliweka matangazo karibu kwenye kuta za chuo kizima, kila mtu alishangaa kusikia Shani ana utafiti kuhusu muziki wa hip hop, wapo ambao hawakuamini kama mtu anaweza kufanya PhD ya muziki huu ambao wengi hawakuutenganisha na uhuni, hivyo ulifahamika kama muziki wa kihuni. Profesa Senkoro akazidi kunitia moyo na kunitaka nisiwe na hofu.
“Ilipofika siku ya kuwasilisha mada, nilimtafuta mwalimu mwenzangu ambaye alikubali kuwa DJ, basi kwenye ukumbi tukatenga kieneo chake na vyombo vyake kazi yake ilikuwa kupiga nyimbo ambazo nimezichagua kwa ajili ya kutetea andiko langu.
Kadiri muda ulivyokuwa unaenda kabla ya wasilisho kuanza, ukumbi ukajaa na bado watu wakawa wamejaa madirishani wakitaka kusikia utafiti kuhusu hip hop,” anasema Shani huku akionekana kuifurahia kumbukumbu hiyo.
Siku ya kuwasilisha mada alibadili mavazi yake yaliyozoeleka na kuvaa uhalisia wa wanamuziki wa hip, ni kama kusema alitupa gauni na mtandio akapigilia suruali ya jeans, tisheti, kofia na raba kama vile wafanyavyo wanamuziki wa muziki huo.
Anasema, “Yaani siku hiyo kila mtu alishtuka kumuona Shani akiwa na muonekano ule. Nilitafuta fulana kubwa, suruali ya jeans pana, raba na kofia nikavaa upande. Nikaingia kwenye ukumbi wa kuwasilisha na kuifanya kazi hiyo kwa ukamilifu. Sikutarajia kama ingepokelewa kwa ukubwa ule kwa kifupi watu wengi walipenda kuanzia mada hadi ubunifu wangu,”.
Shani anabainisha kuwa hata darasani kwake wakati mwingine huwa anafundisha kwa kuimba na wanafunzi wake katika kuhakikisha anachofundisha kinaeleweka na wanafunzi wanakuwa huru kumsikiliza na kumuelewa.
Anavyoiona fasihi
Nguli huyu wa lugha, anakiri kuwa fasihi inakuwa kutokana na ongezeko la waandishi wa kazi za fasihi kila uchwao, lakini changamoto inabaki kwenye hadhira akibainisha kuwa utamaduni wa kusoma uko chini na unazidi kupungua.
“Tunaendelea kupiga hatua ingawa bado kuna changamoto ila hatuwezi kuishia kulalamika, tunapaswa kujipanga kusonga mbele, ndiyo maana nimekuwa nikihamasisha wanafunzi wangu kuandika.
“Msisitizo zaidi nauweka kwa wanawake kwa kuwapa hamasa ya kuandika vitabu ikizingatiwa kwamba hadi sasa tuna idadi ndogo ya waandishi wanawake ikilinganishwa na wanaume. Tuendelee kuandika bila kuchoka wapo watakaosoma,” anaeleza.
Safari yake ya elimu
Shani alizaliwa miaka 52 iliyopita katika kijiji ya Mingungi, Wilaya ya Kilwa mkoani wa Lindi. Hadi kufikia miaka tisa hakuwa amepelekwa shuleni.
Si kwamba kulikuwa hakuna shule au alikuwa hajafikia umri wa kwenda shule ila elimu kwa mtoto wa kike haikuwa kipaumbele kwa familia yake na hilo lilionekana kwenye familia nyingi kijijini hapo, wasichana wengi hawakusoma.
“Baba yangu alifariki mwishoni mwa mwaka 1980, baada ya kifo chake watoto tuligawanywa kwa kuwa mama yetu hakuwa na uwezo wa kutulea peke yake kutokana na hali ya maisha. Baba yetu alikuwa na wake wawili hivyo tulipomaliza msiba watoto wote tulitawanya wengine walienda kwa mjomba, shangazi, baba mdogo na ndugu wengine.
“Mimi nilichukuliwa na dada yangu aliyekuwa akiishi Kurasini jijini Dar es Salaam, kwa kuwa nilikuja Disemba niliwahi uandikishwaji wa darasa la kwanza ambao huwa unafanyika Januari basi nami ndipo nilipopata fursa ya kuandikishwa darasa la kwanza katika shule ya msingi Kurasini,”anasema Shani.
Huo ukawa mwanzo wa safari yake hadi kufikia hatua ya kuwa profesa na msomi bobezi wa lugha na fasihi.