Bongofleva inawenyewe, wamekuja juu hawataki ichezewe

Sunday May 02 2021
bongo pcc
By Nasra Abdallah

Bongofleva ni kiki, kiki ni Bongofleva, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa mambo yanayoendelea sasa.

Watangazaji na wasanii wa enzi Bongofleva inaonekana uhuni wamezungumzia hilo na kukemea uwepo wa kiki kwa madai zinaupoteza muziki waliopigania kwa machozi, jasho na damu.

Miongoni mwa watangazaji wa kwanza kuupa nafasi muziki wa Bongofleva ni Taji Liundi. Kwa ufupi Taji, ambaye wakati huo alikuwa akijulikana kwa jina la Master T, anatajwa kama mwasisi, mwanzilishi na vilevile mtayarishaji wa kipindi cha Dj Show kilichokuwa kinarushwa na Redio One, ambapo alianza kucheza nyimbo za wasanii wa ndani, hususan vijana tofauti na muziki wa dansi na taarabu na wasanii wa nje uliokuwa umezoeleka. Hii ilikuwa mwishoni mwa mwaka 1994.

Taji anaanza kwa kuitaka jamii kuokoa muziki huo kwa kuwakemea wasanii wanaoendekeza kiki.

“Wakikosolewa kwa nguvu zote ikiwamo kuacha kuzungumzia, kujadili kiki na kazi zao itakuwa mfano kwa wengine,” anasema.

Taji anasema kuna mambo manne yanayochangia wasanii hao kuendekeza kiki badala ya kazi. Anayataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwa na uelewa mdogo wa kujisimamia kisanaa, hivyo kufanya mambo wanayoyaona sawa kumbe hayana maadili mema kwa jamii.

Advertisement

Anasema yapo mashindano ya baadhi ya waandishi wanaofanya kazi na wasanii hao kutaka kuwahoji mambo ya ajabu watu ili waonekane wao au vyombo vyao vikubwa kuliko vya wengine.

“Jambo lingine ni kuwapo kwa wasanii wengi wasiokuwa na shoo, ndiyo maana napendekeza kuwe na idara ambayo itawawezesha kuzipata,” anasema Liundi na kuongeza:

“Tulipoanza kuupigania huu muziki tulijua siku moja utakua na kuwa mkombozi wa vijana, lakini huku unakopelekwa siko kabisa, wasanii wajitafakari, wakiuharibu kuurudisha hapa ulipofika ni kazi.

“Jamii haikubali kitu kirahisi kama wanavyodhani, unakubalika sasa kwa sababu kazi ilifanyika,” anasema Liundi.


Abby Skillz

Abby Skillz anasema moja ya mambo yaliyochangia wasanii wa enzi zao kuwa na heshima ni pamoja na watu waliokuwa wakiwasimamia, ambapo ilifika mahali ukikosea unapewa muda wa kupumzika nyumbani, jambo ambalo kwa sasa halipo.

“Hivi sasa kila msanii anajiona mkubwa kuliko mwenzie, hata wale ambao labda wangechukua nafasi ya kuwaonya wengine haipo,” anasema mkali huyo wa kibao ‘Mimi na Wewe’.


Aboubakar Sadick

Kwa upande wake, mtangazaji wa siku nyingi wa Redio One, Aboubakar Sadick, aliyekuwa akiendesha kipindi cha takribani saa tatu cha muziki wa Bongofleva, anasema ujio wa mitandao ya kijamii ndio umeleta haya mambo ya kiki.

Anasema mwanzo watu walikuwa wanabebwa zaidi na ujumbe uliopo katika muziki.

“Yatakwisha tu haya, nakumbuka zilipoanza simu za moja kwa moja kwenye redio watu walikuwa bado na ushamba wa kupiga na kutukana, ila ilikuja kwisha tu yenyewe na sasa wanaona kifaa hicho ni cha kawaida,” anasema Sadick na kuongeza:

“Madhara ni wasanii wachanga kuiga huu upuuzi, wataona ndiyo kawaida ili wajulikane na kufanikiwa na ikiachwa iendelee tutatoka katika muziki mzuri wa kufundisha na kuburudisha tutaingia kwenye matukio yasiyo na maana.

“Tofauti na sasa, wasanii wa zamani walikuwa wanaimba vitu vinavyogusa maisha yetu ya kila siku, lakini huu muziki wa kuimba matusi na bata unawagusa wachache sana wanaoishi maisha hayo na ikiwa wasanii watapata mashabiki wachache ndio wanaanza kugeukia kiki ili kuwaongeza, kumbe angeimba muziki mzuri asingekuwa na haja ya kiki,” anasema Sadick.


Profesa Jay

Joseph Haule, maarufu kwa jina la Profesa Jay anasema inaumiza yanayofanywa na vijana wa sasa katika muziki wa Bongofleva kama vile muziki huo ulikuja kama sadakalawe.

Profesa Jay anasema wakati wakifanya hivyo, wanapaswa kujua kuna watu waliupigania na kufika hapo ulipo.

bongo pc

“Hatupo tayari kuona watu wachache wakiuua muziki tuliopigania kwa kuendekeza upuuzi wa kiki.

“Tulipambana kweli kujenga imani kwa watu, taasisi na makampuni binafsi kuhusu muziki wa Bongofleva kuwa ni kazi kama kazi nyingine na sio uhuni kama watu walivyodhani, lakini kuna watoto wanataka kuturudisha tulipotoka, waache mara moja,” anasema na kuonya Profesa Jay.


Master J

Mtayarishaji wa muziki wa siku nyingi, Joachim Kimaro, maarufu Master J anasema kwa wanayoyafanya wasanii wa sasa katika muziki huo yanatia kinyaa.

Master J anasema imefika mahali wao kama watu walioupigania muziki huo hadi kufika hapo ulipo, wakati mwingine wanatamani kuzima redio, TV na mitandao ilimradi wasiangalie upuuzi unaoendelea.

bongo pccc

“Hawa vijana wa sasa wanafanya mambo ya ajabu sana, wakati tunaupigania muziki huu jambo kubwa ilikuwa msanii ajue kuimba na kutumbuiza kiasi kwamba akitoa wimbo kweli watu wanaupokea vilivyo na kutamani kuendelea kuusikiliza,” anasema.

“Tukiendelea na huu upuuzi wallah tutabakia kugombea wafuasi wa Youtube huku wenzetu wakiendelea kupiga hatua na kuchukua tuzo za kimataifa na kushiriki tuzo kubwa.

“Tujiulize tu wasanii kama wakina Wazkid, Burnaboy na Davido si tuliwajua kupitia kazi zao za muziki na sio kutrend na matukio ya ajabu,” anasema.

Ferooz

Mkali wa kibao cha ‘Starehe’, Ferooz Mrisho, maarufu Ferooz anasema inasikitisha muziki walioupambania miaka ya 1998 unashushwa heshima yake.

Ferooz anasema walipouanza walikuwa wanaonekana wanafanya kazi ya kihuni, jambo ambalo hata wazazi ilikuwa shida kuwaruhusu watoto wao kuingia na kujikuta wanafanya kwa kujiiba.

“Tulipambana mpaka muziki huo umesimama na kuzalisha ajira na kuchangia pato la Taifa na jamii, wakiwamo wazazi kuwasapoti, baadhi ya watu wanataka kuturudisha kule nyuma tulikokuwa tunadharauliwa, hii haikubaliki,” anaeleza Ferooz.

Anasema: “Ndiyo maana wasanii wenye vipaji wamepotea kwa sababu hakuna muziki ni kiki, kama huziwezi unaamini katika kazi unakosa nafasi, gemu limerudi kuwa la kihuni licha ya kuingiza fedha”.


Juma Nature

Mkali wa vibao kama ‘Ugali’, ‘Sitaki Demu’, ‘Inaniuma sana’, Juma Nature anasema wao wakongwe wa muziki huo kwa sasa wamejikuta wakikaa kimya kwa kuwa wakizungumza wanaonekana kama wanawaonea wivu watu fulani kwa kuwa tu wana hela na maisha mazuri.

Hata hivyo, anaeleza kuwa tofauti na wasanii wa sasa na enzi zao walikuwa wanaimba na muziki kuupenda kutoka kwenye damu na pia walikuwa wakitumia muda mwingi kuandika kitu kizuri cha kuleta kwenye jamii.

Mbaya zaidi kiki hizo wasanii wapo tayari kuharibiana katika kuchafuana kama vile hawana Mungu, tukiacha haya yaendelee watakuwa kama wasanii wa Marekani, watapigana risasi hadharani.


Dully Sykes

Dully anasema: “Kiukweli wasanii wa sasa ni kama wameshindikana unapowaambia suala la kiki sio dili, hiyo ni sawa na mtoto aliyezoea kufanya uhuni halafu mzazi umfokee yeye ndio anahama kabisa.

“Hivyo ukiniambia mimi kama kaka katika muziki tunatumia nafasi gani katika kuwaelimisha, hawa hawatusikilizi jamani ndio maana tumebaki kuwaangalia tu,” anasema mkali hiyo wa kibao cha ‘Shumileta’, ‘Salome’ na ‘Mtoto wa Karikaoo’.

Hata hivyo, Nature anasema kwa upande wa jamii kwa kuwa ndio mambo wamekubali kuchagua kusikiliza na kuangalia mpaka watu wapo tayari kukopa vifurushi ilimradi tu wasipitwe nayo, basi waendelee na hii tamthiliya halafu wataona mwisho wake utakavyokuwa.

Hata hivyo Dully anasema ifike mahali serikali ijikite katika kutengeneza kumbi kubwa za burudani ambapo wasanii wanakuwa na matamasha hata ya kila mwezi ya kupiga muziki live, ambapo hapo ndipo patawatenganisha wasanii wajanjawajanja wanaotegemea kiki na wale wa ukweli.

“Bila kufanya hivyo na kuendelea kuacha hawa wa kuimba kwa kuweka flash au CD, tutarajie kuona mengi huko mbeleni zaidi ya haya.

Advertisement