Cheka Tu kusaka vipaji mikoa mitano, mshindi kulamba Sh10 millioni

Monday April 12 2021
COMADY PIC
By Nasra Abdallah

Jukwaa la wachekeshaj wa majukwaani, Cheka Tu kusaka vipaji mikoa mitano huku mshindi kulamba milioni kumi.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu  Aprili 12 na  kiongozi wa kundi hilo, Coy Mzungu  katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu shindano hilo.

Mzungu amesema mashindano hayo yanatarajia kufanyika mikoa mitano ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya Sh10 milioni.

"Wakati mshindi wa kwanza akipata Sh10 milioni, mshindi wa pili atapata Sh5 milioni na mshindi wa tatu atapata Sh2 milioni," amesema Mzungu.

Mbali na fedha, washindi hao watazawadiwa viwanja wilayani Bagamoyo na kupewa ajira za moja kwa moja Cheka Tu.

Amesema lengo la kuazisha mashindano hayo ni kuzalisha vipaji vya fani ya uchekeshaji na kuinua vijana wenye uwezo.

Advertisement

Kwa upande wao majaji akiwemo Zembwela, amesema hawategemei kuona wachekeshaji wake hususani wanaume wakienda wamevaa magauni, au kupaka makeup ili wafanane kama wanawake.

"Standup comedy inamaanisha kipaji halisi bila kujibadilisha, unacheza na maneno  na vitendo na sio kujibadilisha kuwa mwanamke na endapo kuna mtu atakuja hivyo hatutasita kumtimua," amesema Zembwela ambaye jina lake halisi ni Hillary Daud.

Wakati mchekeshaji Clayton Chipando maarufu kwa jina la Baba Levo, yeye amewashauri vijana kuchangamkia fursa hiyo, kwani mbali ya kupata ajira kama unatoka mkoani kwa Sh10 milioni kumi unapata hela ya kuanza kujenga nyumba kwa kiwanja atakachopewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa vipindi vya Wasafi, Jamal Mustapha amesema angependakuona wanawake wakijitokeza kwa wingi katika kinyang'anyiro hicho ili kuongeza idadi ya wachekeshaji wa kike ambao kwa sasa ni wachache.

Advertisement