Darassa ataja malezi ya mtoto wake kuwa sababu ya kupotea

Tuesday January 12 2021
Darassa pic
By Kelvin Kagambo

Dar es Salaam. Rapa Sharif Thabeet, maarufu kwa jina la Darassa ameachia albamu yake wiki mbili zilizopita, huku akieleza sababu ya kupotea kwake katika anga za muziki. 
 Albamu hiyo aliyoipachika jina la “Slave Becomes a King” ni ya kwanza tangu aanze kujishughulisha na muziki na imebeba ngoma 21 ndani yake.

Ikumbukwe mwaka 2016 alijizolea kundi kubwa la mashabiki kupitia wimbo wake uliobamba unaokwenda kwa jina la  “Muziki”. Darassa alipotea katika gemu la muziki  kabla ya kurudi Desemba 23, 2020. 
 
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Darasa ameelezea kilichompoteza kwenye gemu kwa kipindi chote hicho kuwa ni majukumu ya kifamilia ikiwamo malezi ya  mtoto wake wa pili.
 
“Nilikuwa nalea, mimi na mke wangu tumepata mtoto wetu wa pili. Kwa hiyo sikuwa nataka kuchanganya vitu viwili kwa pamoja.
 
“Hata hivyo hakuna kilichoharibika kwa sababu mimi na timu yangu tuliweka kila kitu kwenye ratiba. Kwa hiyo naweza kusema tupo ndani ya muda,” amesema Darasa.

Kuhusu album yake hiyo, Darassa ameeleza maana ya jina la  albamu yake inayoitwa “Slave Becomes The King” (Kutoka kuwa mtumwa mpaka kuwa mfalme) akisema ni sehemu ya kusherehekea mafanikio ambayo yeye, timu yake na mashabiki wao waliyapata kupitia muziki wake.
 
“Utakumbuka tulianza muziki ‘Kiswahili’ sana. Hatukuwa na mipango mizuri ya kibiashara, tulikuwa tunafanya kwa sababu tuna vipaji na ni kitu tunachokipenda lakini mashabiki zetu walitupa nguvu ya kutamani kukuwa zaidi na hatimaye ndoto zetu zimekuwa kweli,” amesema.
 
Amefafanua zaidi neno  Slave (mtumwa) katika albamu yake linamaanisha nyakati ngumu alizokuwa akipitia yeye pamoja na timu yake, kabla hawajaanza kupata mafanikio ya kifedha kupitia muziki wake, na neno King (mfalme) linaelezea mahali walipofikia sasa hivi. 
 
Albamu hiyo ina nyimbo 21 ambazo kati yake 18 ameshirikiana na wasanii wengine akiwemo Alikiba, Nandy, Marioo, Billnas na mkongwe Juma Kakere.

Advertisement