Davido afikisha wafuasi milioni 20 Instagram

Friday April 23 2021
davidopic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Msanii wa Nigeria, Davido amefikisha wafuasi milioni 20 katika  mtandao wa kijamii wa Instagram.

Hiyo inamfanya Davido aliyezaliwa mwaka 1992 ambaye jina lake halisi ni David Adedeji Adeleke kuendelea kushika namba moja kati ya wanamuziki wenye wafuasi wengi katika mtandao huo barani Afrika.

Hadi mwishoni mwa 2015 msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz ndio alikuwa msanii mwenye wafuasi  wengi zaidi kwenye mtandao huo akifikisha milioni 1.5.

Hata hivyo, Septemba 2016 akaondolewa kwenye nafasi hiyo na Davido ambaye sasa amefikisha wafuasi milioni 20 huku Diamond akifikisha milioni 12.2.

Mbali na Davido, wasanii wengine wenye wafuasi wengi Instagram barani Afrika ni Yemi Alade (milioni 13.7), Tiwa Savege (milioni 13.4) na  Wizkid (milioni 12.1).

Licha ya kuachwa na Davido, Diamond anayetamba na wimbo Waah aliomshirikisha mwanamuziki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Koffi Olomide, amepitwa na Yemi Alade na Tiwa Savege wote wa Nigeria.

Advertisement

Kwa mujibu wa mtandao wa Worldometer nchi ya Nigeria inakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 210, huku Tanzania ikiwa na watu  milioni 59.7, jambo linaloweza kuwa msaada kwa wasanii hao wa Nigeria kumpita Diamond kutokana na wingi wa watu katika nchi hiyo.

Hadi sasa mcheza soka wa klabu ya Juventus ya nchini Italia, Cristiano Ronaldo raia wa Ureno ndio mwenye wafuasi wengi zaidi duniani kwenye mtandao wa Instagram akifikisha milioni 279 akifuatiwa na mwanamuziki wa Marekani,  Selena Gomez mwenye wafuasi milioni 222.

Imeandikwa na Peter Akaro, Mwananchi  [email protected]

Advertisement