Diamond agawa chakula, fedha akisherehekea sikukuu ya Idd Dar

Friday May 14 2021
DIAMONDDDDPIC

Nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz akigawa fedha na chakula kwa mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam leo, katika kusherehekea sikukuu ya Eid Al Fitr. Picha na Ericky Boniphace

By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Nassibu Abdul maarufu Diamond Platnumz leo Ijumaa Mei 14, 2021 amegawa fedha na chakula kwa baadhi ya wakazi wa Tandale wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam akitimiza ahadi yake ya kusherehekea nao pamoja sikukuu ya Idd el Fitri.

Wakati akifanya hivyo mkoani Dar es Salaam, kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram, msanii huyo alieleza kutoa vyakula mkoani Kigoma, Morogoro kazi aliyoeleza kuwa itafanywa na ndugu zake na meneja wake, Babu Tale.

Leo saa 5 asubuhi Diamond alikutana na mamia ya wakazi wa Tandale, eneo alilokulia na kugawa nyama na mchele pamoja na fedha, Sh10,000 kwa watu wazima na Sh5000 kwa watoto.

DIAMONDDDPICC

Nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz akigawa fedha na chakula kwa mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam leo, katika kusherehekea sikukuu ya Eid Al Fitr. Picha na Ericky Boniphace

Ugawaji huo ulianza vizuri lakini kadri watu walivyozidi kuongezeka utaratibu ulivurugika kidogo na kulazimika polisi kuingilia kati na kuweka mambo sawa baada ya walinzi wa msanii huyo kuzidiwa nguvu na watu hao.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Diamond aliandika, “InshaAlah kesho (leo)  ndugu yangu Muislam ukiwa maeneo ya Tandale, Kariakoo, Kilungule, pia Morogoro Kusini Mashariki karibu katika mkono wa Eid Mubarak.”

Advertisement

“Ndugu zangu wa Kigoma Ujiji, kesho (leo) maeneo ya Buzebazeba , mtaa wa Sokoine kwa Mzee Bukuku nitakuwa nina mkono wa Eid pia, ukiongozwa na mjomba wangu Mrisho na familia yetu ya mzee Bukuku. Tafadhali mfike kupata salaam zangu.”


Advertisement