Diamond atoa wimbo baada ya miezi saba

Friday June 25 2021
diamondpic
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Wakati leo Juni 25, 2021 ikiwa imetimia miezi saba rasmi tangu msanii wa WCB, Diamond Platnumz atoe wimbo wake 'Waah', ameamua kuachia mwingine mpya unaokwenda kwa jina la ‘Kamata’.

Ukimya huo ulikuwa ni kutokana na kuandaa albamu yake ya nne katika maisha yake ya muziki baada ya kuachia ‘Kamwambie’ (2010), ‘Lala Salama’ (2012) na ‘A Boy From Tandale’ (2017).

Mara ya mwisho kwa Diamond kutoa wimbo ilikuwa Novemba 25, 2020 alipoachia 'Waah!' ambao amemshirikisha Koffi Olomide kutokea DR Congo ukiwa ni wimbo wa tatu kufanya na msanii kutoka nchini humo baada ya Innoss'B na Fally Ipupa.

Hakuna ubishi kuwa wimbo 'Waah' pamoja na video yake ni miongoni mwa nyimbo za Diamond zilizopata mapokezi makubwa kwenye mitandao na kumuingizia fedha nyingi upande wa mauzo.


Mathalani video yake hadi sasa kwa upande wa YouTube pekee imemuingizia zaidi ya Sh100 milioni, hapo bado mauzo kwenye mitando kama Apple Music, Spotify, Deezer, Amazon Music n.k.

Advertisement


Rekodi ilizoweka wimbo wa Waah YouTube


1. Kufikisha watazamaji milioni 1 ndani ya saa nane.

2. Kufikisha watazamaji milioni 4 ndani ya saa 48.

3. Kufikisha watazamaji milioni 10 ndani ya siku saba

4. Kufikisha watazamaji milioni 20 ndani ya wiki tatu.

5. Kufikisha watazamaji milioni 30 ndani ya mwezi mmoja. 

6. Kufikisha watazamaji milioni 40 ndani ya miezi miwili.

7. Kufikisha watazamaji milioni 50 ndani ya miezi mitatu.

8. Kufikisha watazamaji milioni 60 ndani ya miezi minne.

Mashabiki wengi walitarajia Diamond angeachia wimbo 'Loyal' ambao tayari alikuwa ameachia kionjo chake kwenye mtandao wa Instagram ambapo alionekana akiimba ndani ya gari lake, Cadillac Escalade Sky Captain huku akiwa na mrembo wa Afrika Kusini aitwaye Cassi Scheppel (Ciara).

Advertisement