Diamond awacharukia Forbes orodha ya wasanii matajiri

Wednesday May 19 2021
Diamond pc
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Wiki moja baada ya jarida la Forbes kutoa orodha ya wanamuziki matajiri zaidi barani Afrika, staa wa bongo fleva Diamond Platnumz amelibwatukia jarida hilo, akilitaka lifanya kazi yake vizuri.

Mwanamuziki huyo, ambaye jina lake halisi ni Naseeb Abdul, ameshika nambari 28 katika orodha hiyo, thamani ya utajiri wake ikionyeshwa kuwa dola 5.1 milioni za Kimarekani (sawa na Sh11.8 bilioni za Kitanzania).

Kileleni mw aorodha hiyo yuko mwanamuziki mkongwe, Youssour N'dour wa Senegal, ambaye ameshinda tuzo mbalimbali, ikiwemo ya Grammy na Forbes imekadiria utajiri wake kuwa na thamani ya dola 145 milioni za Kimarekani, akifuatiwa na Akon, anayeishi Marekani (dola 80 milioni) na wa tatu ni Black Coffee (dola 60 milioni) na wanne ni Wizkid (21 milioni) na wa tano ni Davido (dola 20 milioni).

Diamond yuko chini ya Chameleon wa Uganda, akishika nafasi ya 24, Okweame Kwame (25), Tinashe (26), na Stoneway (27) wote wakikadiriwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola 6 milioni kila mmoja.

"Tunaweza kukamilisha orodha hii bila ya kumuweka huru nyota wa rock kutoka Tanzania?" limeandika jarida hilo chini ya kichwa kidogo cha habari kinachotaja jina la Diamond Platinamuz na thamani ya utajiti wake.
"Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa anakadiriwa kuwa na thamani ya dola 5 milioni za Kimarekani.

"Nyota huyu milionea wa rock amepata utajiri huu kutokana na kufanya kazi kwa bidii na jitihada. Watu wanapenda sanaa yake na muziki na kumfanya ajipatie mamilioni."
Jarida hilo halijataja vyanzo vya utajiri wake.

Advertisement

Katika ukurasa wake wa Instagram, Diamond ameonekana kuchukizwa na taarifa hiyo na kuandika ujumbe mkali.

"FORBES: Wakati mwingine tafuteni (taarifa zangu) kwa Google kujua thamani yangu halisi kabla ya kuniweka katika orodha yenu ya kijinga ya wasanii matajiri Afrika,” ameandika Diamond.

Mbali na kujipatia fedha kwa njia ya muziki, nyota huyo anajivunia fedha anazopata katika matangazo ya biashara yanayotumia taswira yake kama Pesi, na anamiliki vyombo vya habari na majengo.

Kauli ya nyota huyu imewaibua mashabiki wake ambao wametoa ushauri mbalimbali kwa nyota huyo.
“Atumie akili! Forbes wao ni wakadiriaji tu kupitia mali unazomiliki na streams unazopata katika platform za muziki. Pia maisha unayoishi,” alisema

Cleo Maungo.


Shabiki mwingine,
Brandy Charles alisema: “Usitumie nguvu kuingia orodha ya Forbes. Namba hazidanganyi. Hawa Forbes hawajaanza leo na wanajua nini wanafanya, labda waandae orodha ya hapa kwetu bongo halafu ndio ulalamike, lakini kwa Afrika kwanza hiyo waliyokupa wamekupendelea sababu bado unatakiwa kuendelea kukazana achana na Forbes."
Naye mtu anayejiita ”

Zakwetu Artists ameandika “Ina maana Simba huna mpunga unaozidi $ 1M. Hii ni hujuma hii. Eti hadi Akothee kakuzidi. Forbes wameanza siasa. Simba sasa kama vipi weka data wazi Tanzania tutambe.”


Mwingine aliyemtuliza ni
Zimba Magar ambaye ameandika “usipige kelele kwa vitu vidogo. List ya forbes haiathiri wewe kupata endorsments mpya, haiathiri wewe kukua zaidi. Ile ni kama wake up call tu. Acha iwe vile vile, wewe wekeza zaidi.”


Naye Darmakazi ameandika: “Hapa kinachoangaliwa ni Net worth =Asset - Liabilities, na sio Cash unayomiliki. Na kama ungenunua ile private jet basi ungejitoa rasmi kwenye hiyo top 30 na kuhamia top 100 maana ungekua na nafasi kubwa.”

Advertisement