Diamond mkubwa kwenu ila sio kwa Zuchu

What you need to know:
- Diamond anaelekea kutimiza miaka mitatu bila kutangaza rasmi uhusiano wake mpya, tangu kuachana na Tanasha Donna wa Kenya Machi 2020 wakiwa wamejaliwa mtoto mmoja, Naseeb Jr, lakini kwa Zuchu penzi jipya limechipukia.
Ndivyo ilivyo, staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz amenasa kwa Zuchu ambaye anazidi kuzipa nguvu tetesi za kuwa wapo mbioni kufunga ndoa ikiwa ni zaidi ya miaka miwili tangu wahusishwe kuwa na uhusiano.
Hata hivyo, Zuchu tayari ni mke wa Diamond, hiyo ni kwa mujibu wa kauli ya Diamond mwenyewe wakati akimtambulisha Zuchu katika 'birthday party' ya Dada yake, Esma Platunumz iliyofanyika Februari 2, 2023.
"Hapo ndipo tutajua kama ana mapenzi na wifi yake," alisema Diamond wakati akimkaribisha Zuchu katika tafrija hiyo.
Ikumbukwe Diamond anaelekea kutimiza miaka mitatu bila kutangaza rasmi uhusiano wake mpya tangu kuachana na Tanasha Donna wa Kenya Machi 2020 wakiwa wamejaliwa mtoto mmoja, Naseeb Jr aliyezaliwa Oktoba 2019.
Kwa kifupi, tangu kutambulishwa kwa Zuchu WCB Wasafi, Aprili 2020 Diamond hajawahi kuhusishwa na mwanamke mwingine zaidi ya Zuchu ambaye hadi sasa wameshirikiana katika nyimbo tatu, Litawachoma, Cheche na Mtasubiri.
"Mkubwa kwenu ninyi ila kwangu hana kauli," ni moja ya mistari kutoka kwenye wimbo wa Zuchu, Fire iliyotoka kwenye mradi wake, 4:4:2 pamoja na wimbo mwingine, Jaro.
Mapema leo Zuchu amechapisha picha zake na Diamond katika ukurasa wake wa Instagram ambazo zimevuta na kuteka hisia kuwa wawili hao ni wanandoa au wanandoa watarajiwa kama ambavyo imekuwa ikizungumzwa.
Dada wa Diamond, Esma Platunumz amemuita Zuchu 'Bibi Harusi', katika chapisho hilo liloteka mazungumzo mtandaoni.
Hii sio mara ya kwanza kwa wawili hao kuhusishwa na kuoana, mfano Machi 2022 Diamond alipotoa EP yake, First of All (FOA) jambo hilo lilichukua nafasi kubwa na hata ziara zake kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya kuitangaza EP hiyo lazima angeulizwa suala hilo.
Alipoulizwa na BBC Swahili ikiwa mkewe mtarajiwa anatokea visiwani Zanzibar (nyumbani kwa kina Zuchu), Diamond aliishia kucheka ila alithibitisha kuwa yupo kwenye mipango ya kuoa.
"Kila binadamu anataka kuoa, nitaoa, ndiyo natamani kuoa, bibi harusi watu watamuona, inawezekana akawa miongoni mwa watu ambao washawahi kumuona au pengine hawahi kumuona," alisema Diamond.
Lakini kumekuwa na hisia kuwa wawili hao kufanya hivyo kama kiki tu hasa pale wanapokuwa wametoa au wanataka kutoa kazi mpya, mfano kwa sasa wote wana kazi mpya, Zuchu ametoa wimbo wake, ‘Utaniua’ huku Diamond akiachia ‘Yatapita’ na ‘Zuwena’.
Aprili 2022 wakati Diamond anaelekea kusaini dili la ubalozi na kampuni moja ya mawasiliano ya simu nchini, alitumia mitandao ya kijamii kusema anakwenda kumtambulisha ampendaye, mashabiki wakangojea wakidhania ndio ndoa na Zuchu lakini haikuwa hivyo.
Ikumbukwe Diamond Platnumz amewahi kuwa na uhusiano na wanawake maarufu Tanzania na Afrika Mashariki kama Wema Sepetu, Penny, Zari The Bosslady, Tanasha Donna, Hamisa Mobetto n.k, huku akijaliwa watoto wanne katika mahusiano hayo.