Diamond na WCB kunogesha ‘usiku wa Dk Mwinyi’

Msanii wa Tanzania, Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platnumz

Muktasari:

Hafla hiyo ya mapokezi ya Dk Hussein Mwinyi itafanyika Desemba 11, 2022 ikiwa ni siku tatu tangu alipochaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM taifa uliofanyika jijini Dodoma, Desemba 7, 2022.

Zanzibar. Msanii wa Tanzania, Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platnumz na kundi zima la WCB wanatarajiwa kunogesha “usiku wa Dk Mwinyi” katika viwanja vya Maisara Mjini Unguja kama sehumu ya mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Mbali na Diamond na kundi lake, pia watakuwapo wasanii wengine wa ngoma, taarab, kizazi kipya, singeli, hiphop, Beni, kidumbaku, marimba kutoka bara na visiwani kwa ajili ya kutumbuiza katika viwanja hivyo.

Shughuli hiyo ya mapokezi ya Dk Mwinyi itafanyika Desemba 11, 2022 ikiwa ni siku tatu tangu alipochaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM taifa uliofanyika jijini Dodoma, Desemba 8, 2022.

Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mapokezi hayo, Rashid Simai Msaraka ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Desemba 9, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi za makao makuu ya chama hicho Kisiwandui, Zanzibar.

“Siku hiyo patakuwa hapatoshi viwanja havitachagua wale watu wote wenye mapenzi na Dk Mwinyi, makamu mwenyekiti mpya wa CCM tunawakaribisha sana,” amesema.

Amesema wanategemea kuanzia siku hiyo saa 8:30 mchana, wasanii wote wakijumuisha wasanii wa Zanzibar All Stars, wasanii magwiji wa Zanzibar watakuwepo katika uwanja huo huku burudani rasmi itaanza kutolewa saa 1:00 usiku.

Mgeni rasmi ambaye atakuwa Rais Mwinyi ataingia katika uwanja huo saa 2:30 usiku, kisha atapata fursa ya kuhutubia hadhara na ndipo Diamond atapanda jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza, burudani itakayodumu hadi saa 6:00 usiku.

“Siku hiyo kutakuwa na mambo mengi ambayo mengine yatakuwa ya surprise (kushangaza), ni usiku wa kipekee watu kufurahi na kuburudika wanaompenda Dk Mwinyi bila kujali itikadi zao,” amesema.

Naye mjumbe wa kamati ya mapokezi hayo, Edwin George amesema wanaamini siku hiyo wananchi watajitokeza katika viwanja hivyo kupata burudani bure kupitia kwa msanii Diamond Platnamz na fursa kwa wasanii wa Zanzibar kujumuika na msanii huyo.

George ambaye pia ndiye mkuu wa viwanja vya Maisara amesema taratibu zote katika viwanja hivyo zimeshapangwa ili kuifanya Zanzibar kusimama kidunia siku hiyo.