Diamond: Zuchu akitoka WCB inabidi alipe Sh10 bilioni

Muktasari:

Zuchu alisajiliwa rasmi Wasafi Aprili, 2019, akiwa ni msanii wa pili wa kike kusainia katika lebo hiyo.

Dar es Salaam. Sakata la mjadala wa mikataba inayoingiwa na wasanii wa lebo ya WCB bado linaendelea kuteka vichwa vya habari.

Hii ni kutokana na mabosi wa lebo hiyo kila uchwao kusema maneno tofauti akiwemo mkurugenzi wa lebo hiyo, Naseeb Abdul maarufu kama ’Diamond Platnumz.’

Mojawapo ni pale shabiki aliyejitambulisha kwa jina la qwixa_azz kuandika katika Instagram “Diamond, Zuchu akitaka kutoka atadaiwa bilioni mbili maana sasa hivi ni msanii mkubwa baada ya ‘bigy’ akimaanisha Diamond.

Akimjibu shabiki huyo, Diamond ameandika “Aaah huyo sio chini ya Sh10 bilioni sio unaona namba yake huko mjini YouTube baba,” ameandika Diamond Platnumz.

Mpaka sasa, Zuchu ndio msanii wa kike anaongoza kwa kuangaliwa zaidi kwenye mtandao wa YouTube, katika nchi za Jangwa la Sahara, ambapo mpaka sasa ana wafusai wasiopungua milioni mbili.

Ukiachilia Diamond, meneja wake Hamisi Taletale ”Babu Tale’, jana kwenye ukurasa wake wa Instagram ameandika namna wanakuja kivingine katika kusaini mikataba na wasanii wapya watakaowasajili.

Tale ameandika ”hivi karibuni tutasaini wasanii wawili kujiunga lebo ya Wasafi ila safari hii tumeamua msanii atakua na mashaidi wawili kutoka COSOTA na BASATA.

“Music ni biashara yetu na nijukumu letu kukuza na kusimamia hii kazi hatuwezi kuacha hata iwe vipi,” ameandika Babu Tale.

Hivi karibuni sakata la mikataba wanaoingia wasanii hao lilibuliwa na mtayarishaji maarufu wa muziki, P.Funky Majani na kueleza wasanii hao hukatwa asilimia 60 ya wanachoingiza kwenye lebo na asilimia 40 ndio wanapewa jambo aliloliita nila kinyonyaji.

Siku chache baadaye msanii Rayvanny naye alitangaza kuondoka kwenye lebo hiyo huku ikidaiwa anapaswa kuilipa lebo Sh800 bilioni na baadaye wasaanii hawa walionekana kwenye ofisi za Basata, ikielezwa ni sakata hilo ndilo liliwafikisha huko.