Didi-Stone: Binti wa Koffi anayetesa anga za Naomi

Monday October 11 2021
Didi 2

Kama maji ni kufuata mkondo, ‘lijendari’ wa soka Brazil na duniani, Ronaldo de Lima si angekuwa mtoto wa Mfalme Pele? Galacha wa kikapu, Bill Russell ni kwa nini siyo baba wa Michael Jordan? Au Magic Johnson si ingependeza akawa baba yake LeBron James?

Ukiwa na jawabu ni kwa nini bondia mkali kuwahi kutokea duniani, Joe Louis siyo baba wa Mike Tyson, haitakusumbua leo kuona kuwa Muhammad Ali siyo kizazi cha mbavu nene ulingoni, Jack Johnson.

Ngoja nikutonye; usikariri habari za mtoto wa nyoka ni nyoka, kisa umesikia Christiano Ronaldo Jr, mwana wa Cristiano Ronaldo, naye anakipiga sana tu uwanjani.

Hapo hapo nitakukumbusha kuwa mwanamuziki Frank Sinatra Jr, mpaka alipofikwa na mauti Machi 16, 2016, hakufikia hata moja ya 50 ya mafanikio ya baba yake mzazi, Frank Sinatra.

Tusomane kwenye jamvi hili; Didi-Stone ni binti wa mfalme wa Soukouss, Koffi Olomide. Humuoni akikata mauno ya ndombolo wala akiimba kitoko. Dunia inamtambua na kumheshimu kupitia fani ya mitindo, utadhani ametokea kwenye tumbo la malkia wa ‘fashoni’, Naomi Campbell.

Didi 1
Advertisement

Didi-Stone, ni mtoto wa Koffi wa kwenye ndoa kabisa. Mama yake ni Aliane, ambaye aliingia na Koffi madhabahuni kwa ajili ya sacrament ya ndoa mwaka 1993. Didi-Stone alizaliwa Julai 19, 1999, Marseille, Ufaransa. Ana umri wa miaka 22 sasa.

Kampuni ya kimataifa ya mitindo, Elite Model Management, ndio iliyomsaini Didi-Stone. Taasisi hiyo asili yake ni Paris, Ufaransa. Na ina matawi makubwa kwenye majiji ya New York, Los Angeles na Miami, Marekani, London, UK na Toronto, Canada. Zaidi, Elite Model Management, ipo chini ya kampuni mama, Elite World S.A.

Ni kwa sababu hiyo, utamwona Didi-Stone akipamba majarida mbalimbali duniani kama mwanamitindo. Akilamba dili za matangazo sawa sawa na masupastaa wa michezo kama Kylian Mbappe na Novak Djokovic, katika kampuni kubwa ya Hublot.

Yes, mwaka 2018, Didi aliingia mkataba wa kutangaza saa zinazozalishwa kwenye viwanda vya Hublot. Dili kama hilo, waliingia nyota wakubwa duniani, akiwemo mwanasoka wa kimataifa wa Ufaransa na Paris Saint-Germain, Mbappe na mbabe wa tenisi, Djokovic.

Kama si hapo, utamshuhudia Didi akiwa beneti na bishoo wa soka kutoka Brazil, Neymar, ambaye ameajiriwa na klabu ya Paris Saint-Germain (PSG). Vilevile mastaa wakubwa ulimwenguni, hususani wanamitindo.

Didi3

Didi ni mpenzi kindakindaki wa mavazi kutoka kwa mbunifu wa Ufaransa, Jean-Paul Gaultier. Didi pia ameshawahi kuchaguliwa kuwa kisura wa kampuni kubwa ya vipodozi duniani, L’Oréal.

Katika maisha yake ya uanamitindo, Didi ameshakula shavu la kutangaza bidhaa nyingi kutoka kwenye ‘brands’ kubwa, kama Gucci, Tom Ford, Tony Ward, Christian Louboutin, Djula Jewelry, Jean-Paul Gaultier, Edward Achour, Nina Ricci, Fenty, Jimmy Choo na Gianvito Rossi.

Hivyo ndivyo, Didi anavyoupa ulimwengu tafsiri tofauti. Si kila mtoto wa mwanasheria anaweza kuwa wakili. Si ajabu daktari akamleta duniani mtoto asiyeamini kabisa sayansi. Mtoto wa nyoka si kila wakati anaweza kuwa nyoka.

Isije kutokea Diamond Platnumz akang’ang’aniza watoto wake wawe wanamuziki. Vema mzazi kumwacha mtoto afuate uelekeo wa ndoto zake. Bila shaka, Koffi alishaona muziki wa “bakongo” sio mpango kwa Didi, hivyo akamwacha afuate wito wake wa kwenye mitindo na mambo yamejipa.

Inawezekana kabisa mtoto wa Alikiba akawa sonara au mhandisi. Ni wito. Dunia ijifunze sio kwa sababu mzazi alifanya kazi fulani kwa mafanikio, basi na watoto ndio waige. Kazi za dunia ni nyingi na haziwezi kuisha.

Advertisement