Dk Levy: ‘Wahuni’ Tafuteni pesa, ufundi peleka veta...

Sunday June 19 2022
Dk levy pic

Ni mwaka 2003 tu, miaka 19 iliyopita. Muda wa saa moja jioni. Nje ya geti jeusi la studio za Bongo Records. Bamaga kwa P Funk Majani. Ogopa! Ni wakati ule ambao ‘gemu’ lote lilikuwa chini ya nyayo za ‘Mdachi’ huyu.

Niko na Seleman Msindi ‘Afande Sele’. Jana yake usiku tulikesha Club Bilcanas, kuyatafuna kikatili maisha ya utawala wa ‘Big Ben’ Anko Mkapa. Tukiwa pale Billz ‘naiti kali’, tulikutana pia na ‘Ulamaa’ Solo Thang.

Pale Bilcanas kwa nje, mida ya usiku sana. Lazima ungekutana na masela wanaonukia marashi ya ganja. Wapo tu nje wakiangalia totozi zikiingia na kutoka. Zilizoongozana na ‘bebezi’ na zile zilizo singo.

Ni kama Jiji ndani ya Jiji. Kulikuwa na vibanda vya pombe, sigara, kuberi, rizla na misosi. Vilivyojazana nje ya Bilcanas. Wakati watu wakila maisha ndani ya club, nje pia ‘laifu’ iliendelea ya wadananda wa mjini.

Pale nje ndipo nilishuhudia ‘Ulamaa’ akibeba kijiji. ‘Vesi’ ya ‘Mtazamo’, aliipiga pale nje ‘akapela’ kwa mara ya kwanza. Masela walidata balaa na michano ya ‘msela na bishoo’ wa Mbagala ‘Misheni’.

Jioni ya siku hiyo, alitoka kwa Majani kuingiza hiyo ‘vesi’. Sasa kukutana na mwenye wimbo (Afande Sele), ikawa shangwe na kutambiana kila mtu akijivunia ‘vesi’ yake. Alianza Solo kuingiza sauti, akaja Sele kisha Jay alimaliza.

Advertisement

Mzuka wa ‘vesi’ ya Solo, ulimtia kichaa mtoto wa Kichangani Moro. Kesho akadamkiwa kwa Majani ili aingize ‘vesi’ yake. Tupo Bamaga kwa Majani, geti likafunguliwa na kiumbe wa kike adimu, ilikuwa ngumu sana kumuona.

Kiumbe huyu niliyekuwa namuona viunga vya Jitegemee Sekondari na huyu wa Bamaga ni vitu viwili tofauti. Achana na wa Jite Ute kwa Masawe. Huyu wa Bamaga alikuwa kanona kuliko nyama ya Pofu wa Tarangire.

Kajala? Nyie, nyie! Usione washikaji wanadata, msikie kwa jirani na kwa mitandao yenu hii ya kindezi. Sawa basi, tuseme yule Mmakonde ni mshamba. Vipi Majani naye ambaye alikulia ushuani hapa Dar?

Majani mtoto wa mjini. Wa kishua. Mkao ni Dar na Uholanzi. Na zaidi kasoma Tanganyika International School. Waulize watu wakuambie pale wanasoma watu wa aina gani na ‘ishu’ ikoje. Utakimbia mwenyewe!

Yote hayo kwa Kajala hayakuwa na maana. Mdachi ‘aliwehuka’, akawa haoni kitu kwa toto hili la Kisukuma toka mitaa ya Polisi Oysterbay. Huyu ndo Dada K wa Oysterbay Police. We msikie kwa watu tu kibwegebwege.

Kuna misukosuko mingi iliyochangia Bongo Records ipoteze nguvu. Lakini hisia za Mdachi kwa Kajala ni chanzo kimojawapo. Hatulaumu kwa hili, na bora hivi kuliko ‘ungeresti ini pisi’. Nguvu ya totozi ni zaidi ya tembo.

Konde alipigwa chini muda mrefu na Kajala. Akatumia nguvu, pesa, ahadi na kelele kibao. Ukiachana na bango na Range Rover, kuhonga pisi ndinga kama ile lazima uwe na vitu viwili, pesa na roho ngumu.

Na pisi kukataa Range ingekuwa ujasiri wa kiwango kisichopimika. Okay! Pengine kosa lake ni kubwa kiasi cha kutosameheka kirahisi. Na huenda ukubwa wa kosa umefanya atangaze zawadi ovyo ovyo.

‘Bro’ pesa haijawahi kuwa suluhu ya hisia za mwanamke. Lakini dunia ya sasa misimamo ya kibwege mbele ya pesa pia ni undezi mtambuka. Kajala katupa sababu ya kuelewa lile neno “Pesa ni sabuni ya roho.”

Wapo waliomsapoti kwa upendo wa kweli. Pia wapo waliomsapoti akatae ya ndinga kwa sababu ya choyo tu. Kujifanya wapo naye kumbe moyoni wanaumia ‘akipushi’ ‘Renji Rova’ hapa mjini. Hawa ndo wengi zaidi.

Walisimama naye kwa mtazamo wa akose, aendelee kusukuma Nadia sijui Raum kama wao. Katika kundi hili wapo wa karibu na wa mbali. Wale wa mbali ungewaona kwenye zile comment insta.

Wapo walioogopwa na Kajala yeye kama yeye. Roho ilitaka isamehe, ila wazazi, marafiki na jamii ndo msala kwake... Itamtazamaje? Inategemea na sababu alizotoa za kupigana chini na Konde. Hili lipo kwenye mapenzi.

Kwa ujumla sakata hili liliendeshwa na watu. Maisha ya kioo yanaumiza sana. Sisi tunaweza kuamini Konde aliumia sana, kumbe kinyume chake. Kumbe Kajala ndo alisumbuka zaidi katika maamuzi. Pesa imeshinda.

Kama dunia iliamua Mondi azae na Zari, Hamisa na Tanasha. Ni dunia hiyo hiyo iliyoamua Queen Kajala, arudi kwenye himaya ya Konde Boy. Dunia ya sasa inaendeshwa na pesa. Uchawi peleka kwenu kaka. Mjini pesa inaongea.

‘Renji Rova Blaki’ & Waiti’. Zote ‘pleti namba’ na kadi zake ni umiliki wa jina la Queen Kajala. Konde Boy anataka mtoto arudi awe mmiliki halali. Huyo Kajala mnamchukuliaje kwa mfano? Wapi kuna ‘boi frendi’ malaika siku hizi?

Uliyetaka Msukuma akatae una akili kweli? Siyo ajabu ‘ulikoment’ akatae ukitumia bando la ‘eksi’ wako. Una wigi la elfu 5 kichwani alilokununulia ili mrudiane. Eti unataka Kajala akatae ‘Renji’. Kuweni na akili basi kwenye vitu siriasi.

Dunia ya sasa achana na stori za utu una thamani kuliko pesa. Pesa ndo ina thamani kuliko utu. Utu ‘mai futi’. Mwacheni mtoto wa watu amwagilie moyo. Unadhani ‘Renji’ ni bando la jero kwamba kila mtu analo?

Oya! Wahuni wangu! Tutafute pesa ili tumwagilie nyoyo. Usifikiri Konde Boy kadata, pesa inaongea. Tufuta pesa ya ‘ela yote arifu’. Ufundi peleka Veta, unahaha kuweka mapingiri tumboni eti ‘siksi paki’ halafu huna kitu ? Wewe utabaki kuwa mlinzi tu.

Yaani ikifika Desemba hii, sijakamata milioni mia au mia mbili au mia tatu. Mimi, mimi, mimi! Nakamata mjegeje babaa! Za kichwa! Za kichwa! Woyo, siyo, woyoooo...

Advertisement