Dk Mpango awahakikishia wasanii mkono wa Serikali

Muktasari:

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka wasanii wanaoiga utamaduni na sanaa za nje kuhakikisha kuwa hawapotezi heshima na asili ya Taifa.

Pwani. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewahakikishia wasanii Serikali itaendeelea kuwaunga mkono, huku na akizitaka sekta za uytamaduni, sanaa na michezo kuwanufaisha vijana wengi zaidi nchini.


Makamu wa Rais Dk Mpango ametoa kauli hiyo Novemba 11, 2022 wakati akizindua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.


“Sanaa ndiyo roho ya taifa lolote, hatuna budi kuhakikisha tuna sanaa yenye asili na maadili yanayotuwakilisha Watanzania.


“Nawasihi Watanzania wenzangu na hasa wasanii wetu wa kizazi kipya kuepuka tabia ya kuiga kila utamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili yetu,” amesema.


Dk Mpango amewasisitiza wasanii nchini endapo watalazimika kuiga Sanaa na utamaduni wa mataifa ya nje wahakikishe hawapotezi asili na heshima ya taifa.


Ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kutengeneza maudhui ya kazi zao kwani wasanii ni kioo cha jamii.


Katika hatua nyingine, Dk Mpango ameilekeza Wizara ya Utamaduni na Michezo kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa alipokutana na timu ya taifa ya Serengeti Girls Julai 2022 Ikulu ya Dar es Salaam, la kujadiliana na Wizara ya Fedha na Mipango juu ya namna bora ya kuongezewa bajeti ili ajira kwa vijana kupitia sekta ya burudani zisikwame.


“Katika suala hili Waziri nataka ripoti au taarifa suala hili limefikia wapi kiutekelezaji wake na naomba taarifa hii inifikie kabla ya Desemba 30, 2022 kabla ya kufunga nusu mwaka ya mwaka wa fedha,” amesema Dk Mpango.


Pia Dk Mpango ameagiza tamasha la Bagamoyo liendelee kuboreshwa kila mwaka ili lifikie hadhi ya matamasha mengine makubwa duniani.


Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Mohamed Mchengerwa amesema, kazi ya Wizara hiyo ni kuwaletea furaha na faraja kwa Watanzania pamoja na kubuni mambo mbalimbali ambayo yataleta furaha na amani kwa nchi yetu.


“Malengo yetu katika tamasha hili na lile la Sauti za Busara kutuka Zanzibar ni kuyaendeleza matamasha haya ili kuyafanya kuwa ya kimataifa.


“Tumeshapokea maelekezo kutoka kwa Rais ili kushirikiana nao pamoja kuhakikisha tamasha la Bagamoyo pamoja na Tamasha la Sauti za Busara la Zanzibar yataendelezwa kuwa na taswira ya kimataifa katika siku za usoni hatua itakayosaidia kulitangaza taifa letu ndani na nje ya nchi kimataifa,” amesema Mchengerwa.