FA vua suti, tupe 'rimiksi' ya mabinti kitaani hatuelewi

Hasara! Ndiyo, ya pesa ya kinywaji kilichotoweka kichwani. Baada ya kusikia maneno ya kuumizana ya kibwege kutoka kwa bwege mmoja hivi.
Mshikaji anadondosha chozi kwa ajili ya kiumbe wa kike. Ni mzuri, ndiyo. Pengine mzuri sana kuliko madem kibao waliojaa mitaani, baa na kwenye barabara za jiji la Chalamila.
Mida ya jioni Jumapili iliyopita nikiwa Kinondoni katika baa maarufu lakini yenye umri mdogo tangu kufunguliwa. Wana kibao wakiumiza koo na meno kwa pombe na nyama choma.
Watu wako 'bize' kiasi kwamba wamepoteza kumbukumbu kama kuna kifo. Kila nimuonaye ana uso wenye nuru ya kipuuzi ya kuamini hakuna shida.
Kuna mwamba kando yangu. Simulizi yake inakera kwa tabia za mkewe. Ana wakati mgumu, ni miongoni mwa watu wasio na furaha duniani. Uso umejenga urafiki na kifo cha kujitakia.
Mwisho nilimpuuza na michozi yake baada ya kuniambia mkewe alimpata mitandaoni. Nikagundua nipo na kijana mwenye uchizi kichwani. Nikahamia kaunta kuvuruga ubongo kwa mtungi.
Mwenye akili hawezi kuoa demu muuza sura mitandaoni. Sikatai kwamba hata na wao ni viumbe wa Mungu, huyuhuyu wa Yakobo na Isaka, lakini wenzetu wana ukaribu zaidi na shetani.
Wanawake wanafanya dunia iwe hivi. Bila wao dunia ingekuwa ya kipuuzi sana aisee! Sitamani hilo litokee hata kwa nusu saa.
Pengine FA angechelewa kutoka kimuziki. Lakini mabinti walifanya awe miongoni mwa wakali wa miondoko ya kizazi kipya. Ukitaka ufanikiwe haraka kimuziki, waimbie wanawake.
Wengi wapo jela kwa sababu ya kuwaridhisha wanawake zao kifedha, wanapoona bila pesa wataishia kuwaita shemeji, wanaamua kufanya lolote. Mtu yupo radhi kugombana na ukoo wake wote kisa totozi.
Totozi hulazimisha pesa ya kiwanja na tofali, uamue kununulia ndinga. Halafu sijui wamerogelezewa na magari. Hata kidume kikiwa na gari la kubebea maiti ili mradi kuna viti, kwao sawa.
Totozi na ndinga ni kama siasa na rushwa.
Pia vitu kama poda, wanja visingekuwepo. Changamoto nyingi na maendeleo ya dunia hii yanaletwa na wao. Bila wao magari ya kifahari yangekuwa ya kazi gani?
Bila wao hakuna kidume wa kwenda kwenye majumba ya filamu kukaa sehemu zaidi ya saa mbili kuangalia igizo huku akitafuna bisi?
Kila kitu kizuri kipo kwa ajili yao. Ndio wanunuaji wakubwa wa bidhaa zote. Hununua chakula kwa wingi kuliko uwezo wao wa kula, nguo na viatu kwa wingi kuliko muda wanaotumia kuzurura. Wanavaa vitu vingi mwilini kuliko ukubwa wa miili yao.
Nywele, nyusi, kope vyote vya kuvaa. Sikioni kuna hereni. Mkononi bangiri. Shingoni mkufu na kiunoni cheni au shanga. Mguuni kuna vikuku. Pia kucha zote za kuvalishwa. Hapo hujaongelea mavazi, mafuta na mapambo mengi yasiyo ya lazima. Demu ni pambo la dunia. Wameumbwa hivyo.
Ukitaka utajirike haraka uza bidhaa kwa ajili yao. Wao wameifikisha dunia hapa ilipo. Ndio chanzo cha uchungu na utamu pia. Wanafanya dunia iwe hivi ilivyo kama ni mbaya au nzuri.
Wanawake ni maua wanawafanya wanaume wafurahie maisha au wasifurahie.
Nenda pale walipo wanaume tupu, eneo hilo lazima lijenge urafiki na uchafu kuanzia watu mpaka mazingira.
Wao ni chanzo cha dhambi zote zilizopo kupitia dada wa dunia Eva a.k.a Hawa.
Hivi sasa ni tofauti sana. Sidhani kama wanawake wote wanasikilizwa siyo tu na Mungu, bali hata shetani mwenyewe. Wanafanya mambo ambayo hata shetani hakuwa na 'aidia' nayo.
Pisi za dunia ya sasa kama shetani angewafuata kama alivyomfuata Hawa wa Adam.
Angeshangaa anakutana nao njiani wakimfuata kwenda kumrubuni yeye ili aje kuiteketeza dunia na viumbe wake.
Wanawake wa mjini hivi sasa shetani wao mkuu ni mitandao. Utandawazi umekuwa shetani kamili kwa madem, kuliko hata shetani mwenyewe wa kuzimu kama siyo ahera.
Aliyemrubuni Eva pale Edeni, anatakiwa arudi shule kusoma upya elimu ya kurubuni madem. Ili awe sawa na mitandao ya kijamii. Huko ndiko kunakofanya wanawake wafanye lolote ili waonekane.
Akili za mitandaoni zimeua ndoa nyingi. Zimevuruga biashara kibao, mapenzi kama siyo uchumba.
Shetani wa mitandao anataka mtu ule chakula kama cha 'Kempiski' kila siku. Kuanzia 'brekifasti' mpaka 'dina'. Hivyo ndio vyakula wanavyopost wehu mitandao. Wewe! utaanzaje kupost ugali na dagaa?
Maisha ya mtandao yanakufanya uogope mpaka kivuli chako. Hufanya watu washinde ndani kutwa nzima kama hawana kitu. Kwa sababu wakitembea mitaani wataonekana tofauti na anachoonyesha mitandaoni siku zote. Dem wa mtandaoni hana dhambi, kasoro wala shida. Hali chakula kibaya. Amekamilika kama malaika. Ndio maana kazi yao ni kuwakosoa wenzao tu kina Hamisa na wengineo.
Mwana FA, mabinti wa enzi za Halima Bandawe, hawapo leo. Wao walivaa baibui na hijabu zikatazo kichwa. Hawa hawana aibu na vibabu ndio wanavila vichwa. Tunahitaji 'rimiksi' ya mabinti.