Familia yasema kifo kimegonga mlango ‘Costa Titch’

Msanii Constantinos Tsobanoglou enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Msanii Costa Titch aliyejipatia umaarufu kwa nyimbo za Amapiano amefariki dunia baada ya kudondoka jukwaani wakati anatumbuiza kwenye tamasha la Ultra jijini Johernsburg.

Dar es Salaam. Nchi ya Afrika Kusini imepata pigo lingine la kumpoteza msanii Costa Titch ikiwa ni mwezi mmoja tangu kutokea kifo cha Kiernan Jarryd Forbes maarufu kama AKA kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nchini humo, familia imethibitisha kifo hicho.

 Usiku wa Jumamosi Machi 11,2023 wapenda burudani nchini humo walipata mshtuko baada msanii wa miondoko ya Rap na Amapiano, Constantinos Tsobanoglou mwenye umri wa miaka 28 maarufu kama Costa Titch ambaye alifariki wakati akitumbuiza jukwani katika tamasha la muziki la Ultra lililofanyika jijini Johannesburg linaloandaliwa na IDM ambapo huwa linafanyika kidunia nchini humo.

Baada ya video nyingi kusambaa kwenye mitandao zikionyesha namna msanii huyo alivyodondoka jukwaani na kufariki akiwa anatumbuiza katika tamasha hilo, familia yake imetoa taarifa ya kuthibitisha kifo hicho.

''Kifo kimegonga kwenye mlango wetu kimetupora mtoto wetu mpendwa kaka na mjukuu Constantinos Tsobanoglou mwenye umri wa miaka 28 ambaye Afrika Kusini imempenda ni kwa maumivu makubwa tunathibitisha kifo chake.

“Tunakushukuru kwa wahudumu wa dharura na wote walio kuwepo katika saa zake za mwisho hapa duniani, kama familia tunapitia wakati mgumu wakati tukijaribu kuelewa kilichotokea tunaomba muendele kutuombea.'' Imeandika taarifa iliyotolewa na familia ya Costa Titch.

Coast Tich alijipatia umarufu mkubwa kupitia nyimbo ya Big Flexa ambayo mpaka sasa kwenye mtandao wa Youtube ina watazamji milioni 45 na namna ya uchezaji wake.

Vilevile msanii huyo enzi za uhai wake aliwahi kufanya kazi na wasanii tofauti nchini kama vile Diamond Platnumz, Mbosso pia alishiriki nyimbo ya ‘Wanjera’ ya Ommy Dimpoz na Navy Kenzo nyimbo ya 'Game, Kamatia Chini' akiwa kama dansa.

Baada ya habari hizo baadhi ya watu mashuhuri wametoa salamu za rambirambi akiwemo Julius Sello Malema, mbunge wa Bunge la Afrika Kusini, wengine ni wasanii Navy Kenzo, Diamond Platnumz na wengine wengi.