Filamu 'Slay' aliyocheza Idris Sultan yarejea Netflix

Sunday August 08 2021
Idriss pc
By Peter Akaro

Dar es Salaam. Hatimaye filamu ya 'Slay' aliyocheza Mtanzania, Idris Sultan na wenzake kutoka nchi mbalimbali Afrika imeweza kurejea kwenye mtandao wa Netflix tangu iondolewe Mei 2, 2021.

Filamu hiyo iliweka Netflix Machi 26 mwaka huu, huku Idris akiweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza nchini kuingiza filamu kwenye mtandao huo mkubwa duniani kwa mauzo ya filamu.

Sababu ya kutolewa ni kutokana na kukiuka taratibu za hakimiliki ambapo filamu hiyo imetumia wimbo uitwao 'All For You' wa msanii, Wendy Shay kutoka Ghana bila makubaliano yoyote.

Baada ya suala hilo kumalizika ndani ya miezi, Netflix wameirejesha filamu hiyo kwenye jukwaa lake.

Ukiachana na Idris, filamu hiyo ina wakali kama Tumi Morike, Ramsey Nouah, Fabian Adeoye Lojede, Enhle Mbali, Amanda Du-Pont, Lillian Dube na wengineo.

Je, filamu ya Slay inahusu nini?

Advertisement

Kama jina lake, Slay linavyojieleza, ni filamu inayozungumzia vijana wanaopenda kuishi maisha ya anasa wakati hawana shughuli yoyote ya  kuwaingizia kipato.

Picha linaanza pale Ramsey Nouah 'Richard' anapomtimua kitandani asubuhi na mapema Amanda Du-Pont 'Candy', anamtupiwa nguo yake ya ndani nje. Hii ni kutokana nyumba ni ya kaka yake, Fabian Adeoye Lojede 'Reggie' ingawa amekuwa akiwalaghai ni yake, hivyo anaogopa asije kukutwa na mwanamke ndani.

Candy ni mrembo asiye na shughuli yoyote mjini, anategemea kuishi kwa ofa za wanaume, kitendo cha kufurushwa kama paka mwizi kinamkata sana, anamueleza rafiki yake Dawn Thandeka  'Lunge' anayeishi naye. Amekuwa ni mwenye bahati mbaya sana, hawezi kumsahau Trevor Gumbi 'Weirdo' alimpeleka viwanja na kula na kunywa, kisha kumtoroka bila kulipa bili.

Upande wa pili Idris Sultan 'Musa' ni dereva wa Uchemba Williams 'Dot Kom', anampelekea Bosi wake huyu viwanja kukutana na Mrembo Enhle Mbali Mlotshwa 'Penny' aliyemjulia Instagram, lakini Musa hana muda na warembo ingawa wamekuwa wakivutiwa naye.

Baadaye Musa anakuja kuvutiwa na Simphiwe Ngema 'Ierato'  ambaye ni rafiki wa Penny na wanaishi pamoja, ila Ierato hapendi kuwa na tabia kama za rafiki yake Penny anayesaka wanaume mtandaoni ila inamlazimu kuwa hivyo ili kupata fedha. Musa anajua ili kuunasa moyo  wa Ierato lazima ajidai naye ana fedha, hivyo inamlaghai yeye sio dereva wa Dot Kom.

Lakini naye Ierato alishavutiwa na Musa aliyemuokoa kutoka kwenye mikono ya Leroy Gopal 'Chief Zaddy' aliyekuwa anamlazimisha kuwa naye kimapenzi pindi alipotoka na Penny. Chief Zaddy anaishi maisha ya kutapeli, hivi karibuni katapeli  Rands40,000 kutoka kwa Kaly Bossy Asante 'Emmanuel', raia wa Ghana aliyeenda Afrika Kusini kutafuta kazi.

Alipokea fedha hizo kwa makubaliano ya kumsaidi kupata kibali cha kufanya kazi nchini humo, baada ya kutapeliwa, Emmanuel anapata ushauri kutoka kwa rafiki yake, Kabomo Vilakazi 'Charlie'  ambaye anamueleza ili kupata kibali kwa urahisi atafute mwanamke wa Afrika Kusini amuoe au kuzaa naye.

Basi Emmanuel anajikuta akiangukia kwenye mahusiano na mama mtu mzima, Shaleen Surtie-Richards 'Delillah' lakini kumbe tayari huyu Bibi ana mahusiano na Charlie. Mwishoni Delillah anawatimua wote nyumbani kwake kutokana kila mmoja alitaka kuwa naye pekee yake akilelewa kama Marioo.

Advertisement