Flaviana Matata aweka wazi ndoa yake kuvunjika

Thursday November 18 2021
matatapic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Inakuwa ni mara ya kwanza kwa mwanamitindo Flaviana Matata kuweka wazi kuhusu ndoa yake kuvunjika, tangu lilipotokea hilo miaka miwili iliyopita.
Matata ameweka wazi hilo Jumanne Novemba 16, 2021 kupitia ukurasa wake wa Instagram wakati akielezea namna alivyopenda na kuguswa na mahojiano ya msanii maarufu duniani Adele na  mtangazaji maarufu wa runinga Oprah Winfrey kuhusu suala zima la uaminifu na maisha yake na talaka.
Mwanamitindo huyo ambaye tetesi zake za kuachikwa zilikuwa zikisemwa lakini mwenyewe hakuwahi kulisema amefunguka na kuandika; “Kabla ya kuaibisha watu kuhusu talaka tafadhali jaribu kuwa na huruma, hakuna mtu anayeolewa ili apate talaka.
Akizungumza kutoka kwenye uzoefu wake binafsi, Matata amesema alitalikiana na mume wake mwaka 2019 ambapo mitandao haikumruhusu kupumua na kuwa kana kwamba aliua mtu.
“Niko katika nafasi nzuri sana sasa na mimi mwenyewe na nimepona, asante kwa kabila langu dogo kwa kuwa pale kwa ajili yangu kwani ilikuwa ya kikatili kweli.
“Ni kwamba baadhi yetu huchagua kuficha maumivu kutoka kwa umma, mtandao unaweza kuwa wa kikatili sana na hii ndiyo sababu ni vigumu kwa watu kufunguka kuhusu mapambano yao isipokuwa wale wachache wenye ujasiri.
“Hatusaidii mtu kwa kumuaibisha mtu wakati ndoa haifanikiwi na hii ndiyo sababu ya watu kukaa kwenye ndoa zenye huzuni, matusi na sumu,” amesema.
Hata hivyo Matata ameeleza kwamba mahojiano ya Adele yamemgusa na kumtia moyo hatimaye kusema kitu na kuongeza kuwa jamii inahitaji kufanya vizuri, Mungu ni upendo

“Kwa kusema kidogo, jamii yetu inapaswa kufanya vizuri zaidi na kuacha kuwalaumu wanawake wakati ndoa zinapovunjika na kwanini wanawake ndio wa kulaumiwa? ” amehoji Flaviana.

Advertisement