Gabo: Ndoto yangu ilikuwa uanasheria si uigizaji

Muktasari:

Filamu ni eneo ambalo sikuwahi kulitarajia kama litanipa maisha, lakini leo ndilo limefungua mambo mengi kwenye maisha yangu," amesema mkali huyo wa kuigiza kwa hisia.

Ndoto yake haikuwa kuwa mwigizaji wa filamu, lakini familia yake haikumpa usimamizi thabiti  kwenye elimu yake, hivyo alipohitimu kidato cha nne ndoto yake ya kuwa mwanasheria ikayeyuka.

"Sijui kama ni familia zote za Pwani, lakini nyingi wakati tunakuwa zilikuwa mtoto kama unasoma na asome, kama hasomi basi, nyingi hazikuwa na msukumo wa watoto wao kwenye elimu.

"Hata kwangu, hakukuwa na msukumo wa kitu ambacho nilikitaka, familia nyingi hazikuwa za kukulazimisha mtoto ufanye kitu fulani," anaanza kueleza Gabo Zigamba na kuendelea.

"Nilipohitimu kidato cha nne,  majibu yalipotoka nilipata daraja la tatu.  "Majibu yangu hayakupokelewa kama vile ambavyo mimi nilitamani yapokelewe,  nilidhani na kutamani familia yangu ikae ijue naenda wapi, nini nitafanya na muelekeo wangu wa kielimu utakuwaje ili niwe mwanasheria kama nilivyokuwa nikiota, lakini ikawa ni tofauti.

"Hawakuelewa, kila kitu kikaachwa kwa staili ya kwamba wewe utajua mwenyewe, hapo ndipo niliingia kwenye maisha ya mtaani na ndoto yangu ya kuwa mwanasheria ikaendelea kuwa ndoto mpaja leo," amesema.

Apiga kazi kwenye mikate

Baada ya kuingia kwenye maisha mengine ya mtaani, Gabo amesema alipata kibarua kwenye kampuni (anaitaja) inayojishughulisha na uokaji mikate.

"Niliingia pale kama mhasibu, nikiwa kazini ndipo nilikutana na maisha mengine ya huku nilipo, haikuwa kazi ngumu kujifunza uigizaji, baada ya muda nilitoka nyumbani na kwenda kujitegemea Magomeni na kujikita moja kwa moja kwenye sanaa.

Alivyoingia kwenye filamu

"Filamu ni eneo ambalo sikuwahi kulitarajia kama litanipa maisha, lakini leo ndilo limefungua mambo mengi kwenye maisha yangu," amesema mkali huyo wa kuigiza kwa hisia.

Amesema alishiriki warsha iliyoandaliwa na Mgunga Mwamnyenyelwa, wakati huo Haji Mgwami na Bakari Mtaula walikuwa na taasisi yao maeneo ya Kigogo, ikawa rahisi kwenda kujifunza.

“Tukiwa pale  walitushauri kwanza kwenda kozi Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TasuBa). "Nilifanya sinema moja, kipaji nilichokionyesha, ndipo Sajuki (Juma Kilowoko, sasa ni marehemu) akanichukua na kufanya kazi zake mbili tatu, kuanzia pale ndipo watayarishaji  wengi wa filamu wakanitambua,' amesema Gabo ambaye jina lake halisi na Salim Ahmed.

Amesema, filamu ya ‘Jerusalem’ ambayo ilikuwa ya Jacob Steven (JB) ilikuwa sehemu ya mashabiki kumpokea kwa wingi kwenye ulimwengu wa Bongo movie, ingawa kazi ambazo anazikubali alizofanya akiwa mwongozaji ni ‘Mchanga’ na ‘Keni’, ‘Safari ya Gwalu’ na ‘Siyabonga’.

"Kwenye hizi filamu nafasi nilizoigiza  zilikuwa ngumu, katika filamu au tamthilia, uhusika ndiyo unatengeneza kitu kigumu ambacho utakiwasilisha kwa jamii.

Miaka 16 kwenye uigizaji

Tofauti na wasanii wengi, Gabo amesema hakupitia maisha ya msoto katika safari yake ya uigizaji ambayo sasa inatimiza miaka 16.

"Wakati naingia kwenye uigizaji, nilikuwa nafanya kazi hivyo nilikuwa nina mshahara, sikuwa tegemezi kwa watu, kipato kilinitosheleza hadi kupitiliza, sikuwa na familia wala majukumu mengi.

“Changamoto pekee niliyokutana nayo kwenye fani ni kukataliwa na kupewa majibu ya mkato.

"Japo sasa tasnia ni ngumu kwa maana ina kitu inahitaji na wanaohitaji kazi kuna kitu wanakihitaji hivyo sehemu hizi mbii zinakuwa kama zinakinzana.

"Wakati naanza kuigiza, nakumbuka (anamtaja mmoja wa waigizaji maarufu ambaye sasa ni marehemu) namna walivyokuwa wakitujibu, niliumia, lakini sasa naona ni kawaida na wamenifunza kufanya kazi bora na kuigiza kwenye nafasi ngumu.

"Japo mwanzo sikuwa na ndoto kabisa ya kuigiza, lakini kinachonifariji ni kwamba kitu ambacho sikukitegemea ndicho kinaninufaisha,”amesema Gabo.

Amesema akiwa shule ya msingi, alifanya uigizaji kama sehemu ya utani na kujifurahisha, japo sasa ndiyo imekuwa kazi yake inayomuingizia kipato.

"Shule ya msingi nilitunga igizo la kuwaaga darasa la saba, ambalo lilionyesha namna gani wajiandae na mtihani wao wa mwisho na wanavyokwenda  kukutana na maisha ya uraiani, sekondari pia nilikuwa naigiza tu kama utani.

"Lakini siku zote kila mmoja ana kipaji alichopangiwa na mwenyezi Mungu, hata nilipokuwa nakatiliwa japo iliniumiza wakati ule lakini sasa naelewa.

"Hata kwangu, mtu akija tu kimiyeyusho eti ni msanii siwezi kumkubalia, japo ni tofauti na mimi nilivyokataliwa, kwangu nikikukataa nakupa na maelekezo, zamani tulikataliwa mazima.

"Huwa nawauliza wanaokuja kwangu,. sawa wanapenda kuigiza, lakini kabla hujaomba kusaidiwa wewe unajisaidiaje katika kipaji chako, binafsi naamini kipaji na elimu vinakwenda sambamba ili viwe vizuri, ndiyo sababu hata niliposhauriwa nikasome Tasuba sikujiuliza mara mbili, nilizingatia,”amesema Gabo.

Amesema maisha yake yamebadilika sababu ya kuigiza, amefanya vitu vingi na kuingiza pesa kupitia fani hiyo, lakini kubwa kuliko, popote atakapokwenda Afrika Mashariki anajulikana sababu ya kipaji chake.

"Filamu ya Safari ya Gwalu, na Siyabonga zimebadili kwa ghafla maisha yangu, ni sehemu ambayo namshukuru Mungu zilinilipa vema,"amesema.

Licha ya kutopenda kuzungumzia maisha binafsi na mkewe, Gabo amesema sapoti anayompa sanjari na familia yake ikiwamo kumkumbusha kumtanguliza Mungu ni kubwa katika maisha yake.

"Anaipenda kazi yangu, hata wanangu pia kuna namna nimewajenga na hawatumii umaarufu wangu kujikweza," amesema Gabo.