Hizi ndio kali zilizobamba anga za burudani Bongo

Sunday April 04 2021
Kali pc
By Mwandishi Wetu

Hatimaye robo ya kwanza ya mwaka 2021 imetimia, mengi yamejiri katika safari hiyo yenye milima na mabonde, mafupi na marefu, furaha na huzuni. Lakini ni yapi ya kukumbukwa haswa? Makala haya yanaangazia kwa ufupi matukio 10 yaliyotikisa Bongo upande wa burudani katika robo ya kwanza ya mwaka 2021.

1. Kifo cha Dk. Magufuli

Machi 17 mwaka huu tasnia ya burudani nchini iligubikwa na wingu jeusi kufuatia kifo cha Rais wa tano, John Magufuli ambaye alikuwa karibu sana na wasanii.

Ni wazi wasanii watamkumbuka kwa mambo mengi aliyofanyia kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano aliyokuwa madarakani. Nyimbo walizotoa wasanii kuomboleza kifo chake hazina idadi, zimeimbwa na karibu kada zote za wasanii kuanzia katika Bongofleva, taarab, singeli na dini.


2. Sakata la Baba wa Diamond

Advertisement

Mama mzazi wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim maarufu kama Mama Dangote, Januari 29 mwaka huu aliibuka na kudai Mzee Abdul Juma sio baba halisi wa msanii huyo kama inavyofahamika bali ni Salum Nyange.


3. Kufungiwa Wasafi TV

Mapema Januari 6 mwaka huu, kituo cha Televisheni cha Wasafi TV kinachomilikiwa na msanii Diamond Platnumz kilifungiwa miezi sita na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatia kukiuka kanuni za maudhui kwa kumuonyesha msanii Gigy Money akinengua jukwaani akiwa amevalia nusu utupu.

Hata hivyo adhabu hiyo ilikuja kupunguzwa na Wasafi TV kuruhusiwa kurejea hewani Machi Mosi mwaka huu mara baada ya kukiri kosa na kuomba kupunguziwa adhabu hiyo.


4. Ndoa ya Lulu na Majizzo

Hili ni tukio lililokuwa linasubiriwa kwa kipindi kirefu ndani ya kiwanda cha burudani Bongo, hii ni kutokana na wawili hao kuwa katika uchumba kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Walifunga ndoa Februari 16 mwaka huu katika kanisa la St Gasper lililopo Mbezi Beach, Dar es Salaam. Tofauti na mastaa wengi, harusi ya Lulu na Majizzo ilifanyika kwa kujumuisha ndugu na marafiki wa karibu pekee.


5. Serengeti Music Festival

Tamasha la Serengeti Music lililoanzishwa na Serikali kwa lengo la kutangaza utalii nchini lilianzia Dar es Salaam mwaka jana na hatimaye makao makuu ya nchi, Dodoma ambapo lilifanyika Februari 6 mwaka huu.

Tamasha hili ndilo kubwa kufanyika katika robo ya kwanza ya mwaka 2021, likiwaweka wasanii zaidi ya 70 katika jukwaa moja.


6. Albamu kama zote

Hakuna ubishi robo hii ya kwanza mwaka 2021 imevunja rekodi ya miaka 10 na zaidi iliyopita ambapo wasanii sita wa Bongofleva wametoa albamu pamoja na Extended Playlist (EP).

Wasanii waliotoa albamu ni Lady Jaydee ‘20’, Rayvanny ‘Sound From Africa’, Weusi ‘Air Weusi’, Mbosso ‘Definition of Love’ huku Nandy ‘Wanibariki’ na Lava Lava ‘Promise’ wakitoa EP zao.


7. Gigy kibano cha Basata, Kenya

Hadi sasa msanii Gigy Money anatumikia adhabu ya miezi sita ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za sanaa aliyopewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa madai ya kutumbuiza akiwa nusu utupu kwenye tamasha la ‘Tumewasha’.

Akiwa bado kifungoni, Gigy alikwenda nchini Kenya kwa mwaliko wa mchekeshaji, Eric Omondi aliyekuwa anafanya tamthilia yake ‘Wife Material’, hata hivyo Gigy na Omondi walijikuta wakikamatwa na Bodi ya Filamu Kenya (KFCB) kwa madai ya kukiuka taratibu.


8. Sakata la Paula na Rayvanny

Katikati mwa Februari ilisambaa video isiyo na maadili ikimuonyesha Rayvanny na mtoto wa mwigizaji Kajala na mtayarishaji muziki P Funk Majani, wakijivinjari. Hilo liliibuka saa chache baada ya Harmonize kuweka wazi yupo katika mahusiano na Kajala.

Kusambaa kwa video hiyo kulipelekea Rayvanny kufikishwa kituo cha polisi.


9. Utambulisho wa Anjella Konde Music

Mwanzoni mwa Machi lebo ya Konde Music Worldwide inayomilikiwa na Harmonize ilitangaza kumsajili rasmi Anjella na kuwa msanii wa kwanza wa kike kuwa chini ya lebo hiyo. Mwimbaji huyo alikuwa ameshashirikishwa na Harmonize katika wimbo wake uitwao “All Night”.

Ikumbukwe ujio wa Anjella unaifanya Konde Music kuwa na jumla ya wasanii saba ambao ni Harmonize, Ibraah, Country Boy, Cheed, Killy na Skales kutokea nchini Nigeria.


10. Rayvanny kufungua lebo

Wiki tatu zilizopita Rayvanny alifungua lebo yake aliyoipa jina la Next Level Music (NLM) na kuwa msanii wa kwanza chini ya WCB kufanya hivyo.

Ikumbukwe wasanii kama Rich Mavoko na Harmonize waliojitoa katika lebo hiyo kwa nyakati tofauti, nao walienda kuanzisha lebo zao ila Rayvanny imekuwa tofauti kwani anaendelea kusalia ndani ya WCB.

Advertisement