Huyu Jux! Kila demu kaimbiwa aisee

Sunday June 12 2022
jux pic
By Nasra Abdallah

Wasanii ni wabunifu hadi kwenye mapenzi bana na ndio anachokifanya staa wa RnB, Juma Jux, ambaye amekuwa akiwatendea haki wapenzi wake kupitia muziki wake.

Ndiyo! Jamaa anatenda haki na hakuna mpenzi wake ambaye amemuacha akatoka kapa bila kupata utamu wa mashairi.

Iko hivi. Jux amekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na wasichana kadhaa na kila anayekuwa naye humuimba kwa kushirikiana naye ama kumweka kwenye mashairi yake.

Katika moja ya mahojiano yake aliyowahi kuyafanya hivi karibuni, Jux amesema akiwa kwenye mahusiano hupenda haswa na hawezi kuficha hisia zake na ndio sababu huyakoleza kwa nyimbo.


Nitasubiri

Advertisement

Ngoma hii ina miaka nane sasa tangu imetoka na siri yake kubwa ni kisa ambacho kilimpata Jux.

Wakati akiwa masomoni nchini China, Jux aliachia ngoma hiyo ikiwa ni miezi kadhaa tangu aliyekuwa mpenzi wake, Jackline Cliff, kukamatwa na kuhukumiwa kifungo nchini humo.

Hata hivyo, licha ya kiapo hicho kwenye ngoma hiyo, Jux hakuweza kutimiza, kwani alijikuta akiangukia kwenye penzi la Vanessa Mdee. Na hapa Jux hakusubiri tena, kwani Vanessa akashika nafasi na mambo kuwa motomoto.


Sisikii

Februari 2020, Jux na Vanessa wakiwa kwenye penzi moto kweli wakati huo kichuna huyo akiwa video vixen. Katika wimbo huo, Vanesa anaonekana kukamata mawasiliano ya Jux na mwanamke mwingine.

Malumbano hayo yanadumu hadi Vanesa kuanza kumpiga Jux na kuamua kuondoka na kipindi hiki hasa penzi lao lilikiwa limenoga kwelikweli.

Video ya wimbo huo ambao umetazamwa zaidi ya mara milioni 1, ukazidi kufanya couple hiyo ipendwe na kufuatiliwa zaidi.


Juu

Jux na Vanessa tena wakiendelea kufurahia penzi, wakachomoza na ngoma ya Juu ambayo ilibamba kinoma. Ndani ya video hiyo wawili hawa walionekana mwanzo mwisho wakijivinjari ufukweni, huku kila mmoja akieleza namna gani ataumia iwapo mwanzake atamtema. Hata hivyo, kilichotokea si kinajulikana au tukumbushie?


Sumaku

Huu ndio wimbo ambao ulikuwa wa mwisho kutoka hadharani ambao Jux alimshirikisha Vanessa tena kwa mara nyingine.

Wakati video ya wimbo huu unatoka Vanessa alionekana kulalamika kuwa hajashirikishwa na kwamba, hayakuwa makubaliano ya wimbo huo kuachiwa kwa namna Jux alivyofanya.

Hiyo ndiyo ikawa nafasi kwa mahakimu na waendesha mashitaka wa Instagram kuanza kuchunguza na kubaini kwamba, wawili hawa hawako pamoja tena.


Unaniweza

Ngoma nyingine ya Jux ambayo aliitoa wakati mapenzi yakiwa motomoto na msichana kutoka Thailand, Nnayikaa ambaye naye alikuwa moto moto.

Mrembo huyo ambaye anaelezwa ni daktari, walitengeneza video hiyo nchini humo ambayo iko kwenye mahadhi ya kimahaba, kwani Jux mara nyingi hizi ndio nyimbo zake.

Hata hivyo, mrembo huyo hawakudumu sana na Jux licha ya kuja mara kadhaa hapa nchini huku akieleza sababu kuwa ni umbali wanavyoishi.


Simuachi

Ni wimbo ambao ndio kwanza una wiki ya tatu tangu utoke ukiitwa ‘Simuachi’. Katika wimbo huo video vixen ni mjasiriamali Huddah kutoka nchini Kenya ambao, tayari kwa namna moja au nyingine wamethibitisha kuwa na mahusiano kutokana na matendo yao.

Tayari Huddah kashatua mara mbili nchini tangu ngoma hiyo imetoka akianzia kwenye uzinduzi na sasa amekuja kuzindua bidhaa zake za rangi ya mdomoni ambazo zitauzwa kwenye maduka ya African Boy yanayomilikiwa na Jux.

Advertisement