Ifahamu safari ya ‘Chino Wana Man’, fundi wa amapiano Tanzania

Umewahi kushiriki mashindano, kisha ukashinda na kupewa zawadi ambayo hukuitarajia? Aidha ni kubwa au ndogo? Ndicho kilichomkuta Chino Wana Man, msanii anayekuja kwa kasi nchini.

Dansa huyo ambaye pia hivi sasa anaimba, anakumbuka namna alivyopambana hadi kufika hapo alipo.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Goba, Dar es Salaam, Chino ambaye jina lake halisi ni Isaya Michael Mtambo, anasema alianza u-dansa akiwa kijana mdogo.

"Wazazi hawakunielewa kabisa, japo sasa wanaona matunda ya kazi yangu, lakini kwenye muziki ukiwa ndiyo unaanza familia nyingi zinasumbua, ukizingatia mimi nimetoka kwenye familia ya dini sana.

"Hata hivyo nilijua nini nataka na leo hata wenyewe wanaona matunda," anasema.

Chimbuko la Chino Wana Man

Chino anasema hakuwahi kujifunza uchezaji wake mahali, bali ni vaibu tu ilitokea, akajikuta anapenda kucheza na mwili unampa ushirikiano.

Akieleza jina Chino Wana Man, anasema lilitokana na kupenda namna kabila la Wasukuma wanavyoitana mwanawane.

"Nilianza kujiita Chino mwanawane, Marioo alipokwenda Afrika Kusini kushuti wimbo ‘Mama Amina’, akawa anamuelekeza raia wa kule anayefanya naye kazi jina langu, akaomba maana ya mwanawane, alipoambiwa akaiweka kwa lugha yao na kuniita ‘Wana Man’.

Alivyokutana na Marioo

Chino amekuwa dansa kwa wasanii mbalimbali, kabla ya kufanya kazi na Marioo.

Anasema alikutana na msanii huyo kwa mtayarishaji muziki Aba, wakati huo alikuwa akifanya kazi na Rich Mavoko.

"Alikuwa akiniona ananipa hi! (akimsalimia), kipindi hicho hata sikuwa najua kama anaimba, hadi ulipofika muda wake ndipo nikafanya naye kazi," anasema.

Atoboa siri ya staili yake

"Mimi ni dansa muda mrefu, nimefanya kazi na wasanii wengi, hivyo nilijua nini nafanya, hata hivyo harakati za maisha zilisababisha nifanye chochote ili mradi ni cha halali.

"Nikaona nijipindue kwenye hii hii Amapiano, lakini ninayoifanya niibuni kwa kuwa na staili yangu ndio sababu hata uchezaji wangu ni tofauti na Wasauzi wenyewe.

"Ilinichukua muda mfupi kuianzisha hadi kuitambulisha hii staili, niliifanya nikilenga tu kuji-brand katika harakati za kuendelea kupambania maisha," anasema

Anasema kabla ya staili hiyo, alijaribu kufanya nyingine nyingi.

"Nilichojifunza ni kwamba kila kitu kinalipa lakini kwa muda wake, ndivyo ilivyotokea kwangu," anasema Chino, akifichua namna alivyoingia kwenye udansa kitambo.

Apewa zawadi ya juisi

Dansa huyo ambaye sasa anaimba anasema alianza kucheza akiwa kijana mdogo enzi Mr Nice anatamba kwenye muziki.

"Nilikuwa nikicheza mtaani nikishinda napewa pipi na wenye maduka huko kwetu Ifakara.

"Kama nilivyosema, familia ilitaka niende kanisani, nisali na kuwa mtu wa tofauti.”

Anasema katika kupambania ndoto zake, amedhulumiwa mara nyingi, japo kwa wakati huo haikumuumiza sana kwa kuwa hakuwaza pesa zaidi ya kupata njia ya kutoka.

"Nilitaka kufahamiana kwanza na watu, hivi sasa Mwenyezi Mungu ameninyanyua, sitaki kuyakumbuka maisha ya nyuma," anasema msanii huyo, ambaye amebainisha ataendelea kuimba na kudansi, akisema ataendelea kufanya vyote ili kujitafuta zaidi. Kuhusu kusimama mwenyewe, anasema hawezi kufanya hivyo, ataendelea kushirikiana na wengine kadiri itakavyohitajika.

Shoo ya kwanza iliyomtoa

Anasema ilikuwa ni Arusha wakati huo akiwa hajulikani sana.

"Alikuja Mussa Kizzy kutoka Sauzi (Afrika Kusini) akawa anafanya shoo Arusha, hivyo nikatakiwa nikafanye naye, nilipoambiwa hadi washikaji zangu walikuwa hawaamini, ila nikawaambia inawezekana kufanya shoo kubwa. "Nililipiwa tiketi ya ndege, hoteli na chakula na timu yangu, nikapewa na Sh1.5 milioni, wakati huo ni kubwa, ningepewa hata 200,000 kwangu ingekuwa sawa, tulifanya bonge la shoo ambalo kila mmoja hakutegemea," anasema Chino, ambaye amenunua Alphad kwa ajili ya kusafiria na timu yake ya watu wanane mpaka 10.

Aliwezaje kumshirikisha Fid Q

Wimbo wake ‘Mbinguni’ alioufanya kwa kuwashirikisha Fid Q na Jozeey umekuwa moja ya nyimbo zinazobamba nchini. Anasema mwanzoni alipomshirikishika mwanamuziki huyo wa zamani, alimwambia yeye sio profesheno kwenye amapiano, hivyo atataka kujifunza zaidi. "Fid Q ni bro (kaka), nilikuwa namfahamu kabla, siku moja katika harakati za muziki nilikutana naye Zanzibar, nikaenda kumsalimia na tukabadilishana namba. "Baada ya muda nikamuomba tufanye naye kazi, akaniambia huu muziki sio profesheno yangu, nahitaji maelekezo zaidi.

"Ni mtu ambaye anajua kuishi na watu, kwa levo yake kimuziki alinipa heshima kubwa kukubali kufanya kazi na mimi, tukaingia studio, kipindi chote alijua yuko na sisi wadogo zake, tumefanya kazi na imebamba," anasema. Licha ya mafanikio hayo, Chino anakumbuka namna alivyopambana kutoka, na zawadi yake ya kwanza kupewa kubwa kwenye kudansi ilikuwa ni juisi.

"Ilikuwa ni huko kwetu Ifakara, kulikuwa na mashindano ya kucheza, nilishinda na kuwa bingwa, nikapewa pakiti 10 za juisi za kuchanganya na maji.

"Nilinywesha mtaa mzima, hiyo ndiyo zawadi yangu kubwa ya kwanza niliyoipata kwenye dansi.”

Anasema baada ya shindano lile, alipitia kipindi cha mapambano kabla ya kuhamia Dar es Salaam na wazazi wake, wakiishi Tabata bonde la mchicha. "Harakati zilikuwa nyingi, wazazi walinisihi tu kusoma, waliamini mafanikio katika elimu, lakini kwangu ikawa tofauti, kipaji kimeokoa familia yetu," anasema.
Usumbufu wa wanawake

Kuhusu kuanzisha familia, huku akitabasamu, akiwa mbele ya mama yake, Patricia Philipo Ndaga, Chino anasema mzazi wake huyo hajawahi kumpangia mwanamke wa kumuoa "Hajui hata kama napata usumbufu wa wanawake, lakini ninachoshukuru Mungu ni kwamba naweza kujisimamia, malezi ya wazazi wangu yameniongoza kujua kipi kizuri na kipi kibaya. "Usumbufu wa wanawake naufahamu na ninaelewa niishi nao vipi, wakati utakapofika wa kuwa na mke nitafanya hivyo, lakini kwa sasa nipo naishi na familia yangu, dada zangu, kaka yangu, marafiki ninaofanya nao kazi na mama yangu hapa ni kwake," anasema Chino, ambaye anaishi kwenye mjengo wa ghorofa huko Goba. Nyumbani kwake kumechangamka na kila mmoja anafurahia hadi watoto wadogo ambao ni wa ndugu zake, wakitaniana utani wa hapa na pale kuchangamsha nyumba.

Chino, ambaye mara nyingi alikuwa akitoa maagizo ya mahitaji ya nyumbani na mambo mengine, anasema hiyo ni nyumba yake ya tatu kuhamia. "Kabla nilipanga nyumba mbili kwa nyakati tofauti, zote niliondoka na nguo zangu nikawaachia washikaji (marafiki) nikaja kuanza maisha mapya hapa, kila kitu ni kipya kwenye hii nyumba," anasema.

Kila atakapokwenda haachi pesa

Msanii huyo anasema katika maisha yake ya kila siku hivi sasa kuna vitu vingi haachi kuwa navyo, lakini kwanza ni pesa. "Mwanzoni nilikuwa siamini hiki kitu, lakini sasa naelewa siwezi kutembea bila pesa, popote ninapokuwa, furaha yangu ni kusaidia wengine, nikipita mtaani nikamuona muhitaji na kumsaidia hiyo ndiyo furaha yangu, napenda kile ninachoweza kukifanya basi nifanye," anasema.

Anasema wakati anahangaika kutafuta maisha, kuna muda alikuwa akiona magari yanapita anatamani tu mmoja asimame na kumsaidia japo Sh2,000 ya kula.

"Kama yale maisha nilishayavuka, bado kuna watu wanayaishi, hivyo huwa napenda tu kusaidia, sio hadi niombwe msaada, mimi nakumbuka nyuma njaa inauma, lakini hujui unakula nini. Huna kitu.