Jay Z ajiunga Instagram kwa kishindo

Wednesday November 03 2021
jayzeeeepic
By Peter Akaro

Msanii wa Hip Hop maarufu duniani toka Marekani, Jay Z ameamua kujiunga katika mtandao wa kijamii wa Instagram.

Mtandao wa Instagram ulianzishwa Oktoba 2010 na Kevin Systrom na Mike Krieger, Aprili 2012 ulinunuliwa na kampuni ya Facebook ambayo sasa inajulikana kama Meta.

Baada ya kuanzishwa kwake ulipata watumiaji milioni 1 ndani ya miezi miwili, hadi kufikisha mwaka mmoja tayari ulikuwa na watumiaji milioni 10. Takwimu za sasa zinaonyesha mtandao huo una watumiaji bilioni 1.2 na kushika nafasi ya tano kama mtandao wenye watumiaji wengi.

jayzpic

Leo Novemba 3, 2021 imekuwa siku nyingine katika historia ya mtandao huo kwa kumkaribisha Jay Z, ambaye walikuwa wanamngojea, hilo lilizuia mtu yeyote kufungua akaunti kwenye mtandao huo kwa jina la Jay Z.

Mara baada ya kujiunga ukurasa wake umeshapata kitiki cha blue (verified) kuonyesha kuwa ni halali, na imemchukua saa tatu pekee kufikisha wafuasi (followers) milioni 1, huku chapisho lake la kwanza likipendwa (likes) na watu zaidi ya 340,000 ndani ya saa sita pekee.

Advertisement

Jay Z ameamua kumfuatilia (follow) mtu mmoja pekee ambaye ni mkewe, Beyonce mwenye  wafuasi zaidi ya milioni 216, huku naye akimfuata mumewe pekee.

Utakumbuka mshambuliaji wa Manchester United kutoka nchini Ureno, Cristiano Ronaldo ndiye binadamu mwenye wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram akiwa nao zaidi ya milioni 362.

Kwa mujibu wa kampuni ya kimataifa ya masoko mtandaoni, Hopper HQ kutoka nchini Uingereza, Ronaldo ndiye anaongoza kwa kulipwa fedha nyingi kwenye mtandao huo kwa kuchapisha matangazo ambapo kwa mwaka huu anachukua Dola1.6 milioni sawa na Sh3.71 bilioni.


Advertisement