Jay-Z: bilionea anayezalisha mabilionea

Sunday August 15 2021
JZ pc
By Peter Akaro

Wiki iliyopita Jarida la Forbes lilimtangaza mwimbaji Robyn Fenty ‘Rihanna’ kuwa ni bilionea mara baada ya utajiri wake kufikia dola 1.7 bilioni na kuwa mwanamuziki wa kwanza wa kike kufikia mafanikio hayo.

Ukiachana na muziki na uigizaji, kampuni yake ya urembo, Fenty Beauty iliyozinduliwa mwaka 2017 kwa kushirikiana na kampuni ya bidhaa za kifahari LVMH, inatajwa kuchangia sehemu kubwa ya utajiri wake ikiwa ni dola 1.4 bilioni.

Rihanna anakuwa msanii mwingine kufikia hadhi ya ubilionea akitokea kwenye mikono ya Shawn Carter ‘Jay Z’ baada ya Kanye Omari West (Kanye West) aliowatengeneza wakati akiwa Rais wa Def Jam Recordings.

Mwaka 2003 Jay Z alitangaza kuacha muziki akiwa tayari ameshatoa albamu tisa zake binafsi na nane za kushirikiana, alikuwa ameshatengeneza utajiri wa dola milioni 300, huku akimiliki sehemu ya timu ya NBA, Brooklyn Nets pamoja na miradi mingine mikubwa.

Kuacha muziki kulimpa nafasi ya kuwa Rais wa Def Jam Recordings, hilo lilipelekea Universal Music Group (UMG) ambayo ilikuwa kampuni mama ya Def Jam kununua sehemu ya lebo ya Jay Z, Roc-A-Fella Records kwa dola milioni 30.

Akiwa kama Rais wa Def Jam, Jay Z aliwasaini Kanye West, Rihanna na wasanii wengine wapya kwenye lebo hiyo ambao walifanya vizuri. Hadi anastaafu kama Rais mwishoni mwa mwaka 2007 baada ya kumaliza muda wake, tayari wasanii hao walikuwa wametengeneza himaya katika muziki.

Advertisement

Mwaka 2019 Jarida la Forbes lilimtambua Jay Z kama msanii wa kwanza wa hiphop kuwa bilionea, akiwa na utajiri wa dola 1 bilioni ambapo sasa umeongezeka na kufikia dola 1.4 bilioni.

Forbes walitaja vyanzo vya mapato ya Jay Z ni kuwa na hisa ya dola70 milioni kwenye kampuni ya usafiri ya Uber, dola70 milioni kwenye masuala ya sanaa, dola50 milioni kwenye umiliki wa majumba ya kupangisha, muziki, umiliki wa mtandao wa Tidal pamoja na umiliki wa kampuni ya Roc Nation.

Mwaka 2020 Forbes wakamtangaza Kanye West kuwa bilionea akiwa na utajiri wa dola1.3 bilioni, hata hivyo mwaka mmoja nyuma Kanye alidai utajiri wake ulifikia dola3.3 bilioni baada ya Forbes kuripoti ni dola890 milioni.

Baada ya mwaka mmoja Forbes walikuja na takwimu nyingine kuhusu utajiri wa Kanye West ambapo ulifikia dola1.3 bilioni na sio dola3.3 bilioni kama alivyodai hapo awali.

Forbes walisema utajiri wa Kanye umechangiwa na biashara zake za nguo na viatu, Yeezy Sneakers na muziki. Kwa matokeo hayo, Kanye alipandishwa rasmi na kupewa hadhi ya ubilionea akiwa ni msanii wa pili wa hiphop duniani baada ya Jay Z.

Jay Z, mwenye mchango kwa mabilionea wenzake hawa, kwenye moja ya nyimbo zake ananukuliwa akisema; ‘I’m not a businessman, I’m a business, (Mimi sio mfanyabiasha, bali mimi ni biashara’).

Julai 24, 2009 Jay Z aliwashirikisha Kanye West na Rihanna katika wimbo wake uitwao ‘Run This Town’ ambao ulikuwa ni wa pili kuuachia kutoka kwenye albamu yake ya saba iitwayo ‘The Blueprint 3’, wimbo huo ukafanya vizuri hadi kushika nafasi ya pili kwenye chati za Billboard Hot 100.


Advertisement