Jaymoe siyo wa kupewa maua, anahitaji heshima

Makumbusho na Kijitonyama. Zikawa maarufu zaidi ya Mikocheni na Mbezi. Ikawa ujanja kupiga misele au kuishi kipande hicho. Makumbusho ikawa juu kama 'Malibu' ya Bongo hivi.

Hata 'pisi' za kitaa hicho zilijitawisha wadhifa fulani kwa kujua ama kutojua. Kifupi ni kwamba umaarufu wa Makumbusho na K'nyama, ni kama ulienda sawa na makuzi ya Bongofleva.

Uliza vijana wa nyakati zile. Achana na Makumbusho na K'nyama kama mitaa, pia chimbo la Graveyard mitaa hiyo. Hakuna msanii nyakati zile ambaye hakupeleka komwe lake pale kabla ya 'kutrendi' katika vituo vya redio. Ilikuwa Mecca au Vatican ya Bongofleva. Ilikuwa kama ofisi za Fifa na UEFA ya Bongofleva. Kuanzia wanamuziki, waandishi na mapromota walilazimika kupajua Graveyard.

Ili kumpata Daz Baba kwa shoo ama andiko, lazima ungefika ofisi za Fifa yao. Hawakuwa na simu za mikononi wala ofisi. Bali walipatikana kwenye chimbo zao na chimbo namba moko ndio lile. Unatagemea nini?

Pale wapo waliokwenda kumoka ganja. Baada ya muda flan wakageuka kuwa wanamuziki tena wakubwa. Na wapo wasanii waliokwenda kupiga stori tu, baada ya muda fulani wakageuka kuwa wapuliza mimoshi wakubwa.

Ni chimbo ambalo liliharibu vijana na kuwajenga kwa ukubwa uleule. Yes! Ungekutana na mabingwa kwelikweli wa kuandika 'vesi'. Na mabingwa hasa wa kupuliza mimoshi. 'Wati e gemu?'

Unakumbuka mpini wa 'Kama unataka dem'? Ambao ndani kuna sauti nzito ya Msafiri Kondo (Solo) na sauti laini sana ya Aboubakar Shaaban (Chilla)? Ndiyo! Kuna majina yametajwa ya pisi kali mule.

Suzzy wa maghorofa ya Bima na Mos Def ni pisi za kitaa Makumbusho na K'nyama. Walikuwa maarufu bila hata kuigiza kama Nora, wala kutangaza kama Amina Chifupa, lakini wakawa mastaa. Mpaka leo wapo.

Umaarufu wao ni kwa sababu ya kuishi 'Malibu' ya Bongo. Hakuna kitu kizuri bila kukipamba. Hata Makumbusho na K'nyama zilikuwa tamu kwa sababu ya kupambwa. Na wapambaji waliojua kuzipamba.

Vipi baa kama Chaga 'Baiti'? Umaarufu wa Chaga 'Baiti' haukuendana hata na ubora wa huduma na mandhari ya baa yenyewe. Lakini ikawa juu kuliko Steve Nyerere, Swebe, wala Mpoki wa wakati ule.

Kwa sababu tu masela walijua kuzipa shavu. Na masela wenyewe ni wale wenye muziki wao. Kuna 'taim' neno Makumbusho lilikuwa kama ubini wa Jaymoe. Kuna muunganiko mkubwa wa Moe na Makumbusho.

Pini zake zote ukisikiliza, ndio utaelewa jinsi msela alivyofunga ndoa na mitaa hiyo.
Makumbusho na Kijitonyama zilibebwa na mabega ya mwamba huyu mwenye asili ya kusini. Ndiyo msela ni Konde Daddy!

Juma Mchopanga, aliisifia 'huudi' yake, akasifia pisi za 'huudi' yake. Na aliishi kwa namna ya 'huudi' yake ilivyotaka. Huwezi kupendwa 'huudi' bila kuyaishi yale yote ya 'huudi' yako, na ndicho msela alichofanya.

Alikuwa mtawala wa Makumbusho, wa Kijitonyama na Graveyard yenyewe. Na uzuri wake ni kwamba ni maeneo yale yanakaribiana na makao makuu ya BongoRecords, kwa Mdachi Majani.

Ina maana kwamba wakati Jaymoe akiwa tayari chini ya Mdachi. Ilikuwa rahisi kutembea hadi studio kumwaga mistari na kujikataa. Bamaga pale kwa P Funk ndio K'nyama yenyewe.

Jaymoe ni Mteule. Yeye na Jafari Ally Mshamu 'Jafarhymes', Taikun Ally 'Mchizi Mox’ na Kelvin Kimari. Hawa ni masela waliokuwa na kundi lililoitwa Sewer Celibacy.
Enzi hizo Jaymoe akijiita Ex-Marhem, Mchizi Mox akijiita Jambazi Mox na wenzao wakitumia majina yao halisi. Mwaka 2000, Clouds Fm waliandaa tukio pale Mambo Club, Oysterbay.

Ni tamasha la muziki na ndani yake kukawa na kusaka vipaji vya kuchana. Waliosimamia mchongo huo ni majaji watatu, ambao wote ni maprodyuza wakubwa, Master J, P Funk pamoja na Dunga.

Jaymoe na kundi la 'Sewer Celibracy wakashika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ikaenda kwa Msafiri Kondo a.k.a ‘Solo Thang’, Lady Luu akabeba nafasi ya tatu na namba nne akawa Mack Maliki 'Simba' a.k.a 'Mack 2B'.

Kundi la Sewer Celibacy, Mack 2B pamoja na Solo Thang, walipata ofa ya kutengeneza ngoma Bongo Records chini ya P Funk Majani. Wakati huo ni kwamba Majani ni wa moto hashikiki na hatabiriki.

Wakiwa studio wakisubiri kurekodi pini la "Hip Hop na Ragga", Kelvin alipata wazo na 'kushea' na wenzake kwamba, kwa kuwa jana yake waliteuliwa kuwa washindi, basi wajiite Wateule.

Masela wote wakakubaliana na wazo lile la Kelvin. Ndipo ukawa mwanzo wa jina la Wateule. Na kuunganisha miba kibao ya hiphop iliyokuja kugeuka lulu kwa game la hiphop hapa Bongo.

Anza na SoloThang, mwamba huyu ni Mteule. Njoo kwa Mchizi Mox na yule 'bishoo' Jafarhymes. Twende kwa Mac 2 B Simba na Lady Luu. Hawa wote walikuwa wa moto kwelikweli na gemu waliliteka jumlajumla.

Pamoja na ubora wao, lakini ni Juma Mchopanga pekee ambaye hadi leo bado ananata na 'biti' la muziki. Wateule wengine wapo, ukiacha waliotangulia mbele ya haki.

Lakini ni Jay To The Moe ambaye hata kesho anatembeza msasa kwenye hili game. Kwa nini asipewe heshima yake? Watu sampuli hii kwenye gemu la Bongo Hiphop hawahitaji maua bali heshima.

Bongo Flava Honors. Sasa wanataka kutoa heshima kwake Moe-Mbakiaji. Moe-Mawazo apate 'rispekti'. Moe-Tech avalishwe taji la heshima. Moe-Skills atunukiwe ukuu wa heshima. Yes! Anastahili sana. Ijumaa ijayo Bongo Flava Honors wanakuletea huyu kiumbe.

Ni palepale Alliance Francaise Upanga. Madude yote kuanzia "Ulimwengu ndo Mama" mpaka "Nisaidie Kushare" ya sasa. Zitapigwa kwa live band.
Hapo ndipo sehemu inapigwa shoo ya mswahili, lakini wazungu wanajaa kama mamtoni mwanangu. Twende tukale bata la kishua na mwanetu wa damu kabisa Juma Mchopanga. Jiiiia!