Joti, Mkojani kuchuana mkali wa vichekesho tuzo za filamu

, Lucas Mhavile 'Joti'

Muktasari:

Tuzo za filamu mwaka 2022 zinaandaliwa na Bodi ya Filamu Tanzania ambapo itashindanisha filamu katika tanzu mbalimbali ikiwemo vichekesho vinavyofanywa na wasanii hao.

Dar es Salaam. Wachekeshaji maarufu, Lucas Mhavile 'Joti', Abdallah Mzunda 'Mkojani' na Tabu Mtingita wameteuliwa kuwania tuzo za filamu ambazo zinatarajiwa kutolewa Desemba 17, 2022 jijini Arusha.

 Majina hayo yamewekwa hadharani leo Jumamosi Desemba 9, 2022 na Bodi ya Filamu ambao ndiyo waandaji wa tuzo hizo na mwaka huu zinatolewa kwa mara pili.

Katika tuzo hizo, kipengele cha wachekeshaji bora, wasanii Joti, Mkojani na Tabu Mtingita watachuana katika kipengele hicho.

Joti ambaye filamu zake tatu kati ya tano alizozipeleka zimeingia katika mchujo huo wa mwisho wa kuanza kupigiwa kura, ameingia ķatika kipengele hicho cha mchekeshaji bora kupitia filamu yake ya "Usipite Jeshini'.

Wakati Tabu Mtingita akiingia kupitia filamu ya "Mama Mkwe", Mkojani ameingia na filamu ya "Ugaigai".

Wasanii wengine waliotajwa kwenye kipengele hicho ni Andrew Ngonyani (Brother K) aliyepata umaarufu kupitia vichekesho vya Futuhi.

Wengine ni Gladness Kifaluka wa vichekesho vya Kitimtim na Ally Chuma wa vichekesho vya "Jambo na Vijambo".

Akizungumzia kuteuliwa kwake, Joti amesema anashukuru kwa kufikia hatua hiyo kwa kuwa wachekeshaji ni wengi.

Alipoulizwa anaonaje alioteuliwa nao, Joti amekiri kuwa mchuano ni mkali na kuomba mashabiki zake kura zitakapoanza kupigwa wasimuangushe,  wampigie kwa wingi ili aweze kuondoka na ushindi  kama ilivyokuwa kwenye tuzo za mwaka jana.