Kajala, Paula wahojiwa polisi wakidaiwa kusambaza picha za Harmonize

Tuesday April 20 2021
kajalapic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Mwigizaji wa filamu nchini Tanzania, Kajala na mwanaye Paula wamehojiwa kwa saa kadhaa polisi na kuachiwa kwa dhamana wakidaiwa kusambaza picha za utupu zinazodaiwa kuwa za msanii wa Bongofleva, Rajab Abdul  maarufu Harmonize.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 20, 2021 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha kukamatwa na kuachiwa kwa wawili hao baada ya kutua nchini wakitokea Dubai.

Taarifa za kukamatwa kwao zilianza kusambaa mitandaoni jana na leo Mambosasa amethibitisha na kufafanua kuwa walikamatwa  usiku wa kuamkia jana na kuhojiwa lakini waliachiwa kwa dhamana siku hiyo saa 1 usiku.

Kamanda huyo ameyataja makosa wanayotuhumiwa nayo ni kusambaza picha za utupu mitandaoni  zinazodaiwa kuwa za Harmonize  na msanii huyo ndiye mlalamikaji.

“Ni kweli tuliwakamata Kajala na Paula tukawahoji baada ya mlalamikaji Harmonize kuleta malalamiko kituoni lakini tayari tumeshawaachia kwa dhamana,” amesema Mambosasa.

Amesema wawili hao wataendelea kuripoti polisi mpaka hapo jalada la upelelezi wa kesi yao litakapokamilika na kufikishwa mahakamani kwa kuwa kesi za aina hiyo huchukua muda mrefu kuzifanyia uchunguzi.

Advertisement

Katika hatua nyingine Kamanda Mambossa amesema wasanii Rayvanny, Baba Levo na Juma Lokole nao wamelalamikiwa na Harmonize kwa kosa hilo la kusambaza picha za utupu na tayari wamehojiwa na polisi  na upelelezi bado unaendelea.

Siku tano zilizopita, Harmonize kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Instagram  alisema atawafikisha mahakamani na kuwadai fidia waliochafua jina lake mitandaoni kwa kusambaza picha hizo zinazodaiwa kuwa ni zake.Advertisement