Khaligraph angejibiwa na mstari mmoja wa Solo Thang

Siyo yeye tu! Ulimsikia Ommy Dimpoz baada ya kifo cha Ngwair? Alisema wasanii hawapaswi kufa maskini. Wachache sana walimuelewa baada ya kauli hiyo. Alimtazama vibaya. Vidole alinyooshewa kama kakufuru. Unadhani ilipaswa alaumiwe?

Tulio wengi wa mapokeo. Hatujisumbui kufikirisha bongo zetu. Tunabeba jambo lolote. Tunalitafsiri vyovyote. Na kisha tunahukumu kivyovyote. Ukweli ni kwamba inaumiza sana msanii aliyewika sana kufariki hohehahe.

Hawakusumbua akili zao ili kumuelewa Ommy. Dogo ndio kwanza anatokatoka kisanii. Akawa mdogo kama tairi ya bajaji. Pipo hazikuelewa la muadhini wala mnadi swala. Akili zao zikaona ni dharau kwa kipenzi chao 'Kaowize'.

Toka Ngwair anatoka na kuwa msanii mkubwa. Muziki ulikuwa unalipa sana ndio maana Ommy ilimuuma. Tatizo kona ni nyingi kufikia pesa zilipo. Zamani kampuni ziliweka mzigo kwenye shoo na kufaidisha mapromota.

Leo zinaweka maokoto kwa msanii husika. Lawama za mashabiki na wasanii wenzake zilizidi mwisho wa siku Ommy akaomba radhi. Watu hawakupoteza muda kuitafakari kauli ya Ommy. Dogo alikuwa sahihi lakini kauli aliitoa wakati usio sahihi. Ndio kosa lake kuweka chumvi juu ya kidonda.

Ukweli ni kwamba muziki wakati huu na wakati ule, ilikuwa ni pesa. Msanii kufa bila kitu haina afya. Ndipo uhalali wa kauli ya Ommy ulipo. Kwamba msanii mkubwa haifai kufa maskini. Wasanii walitumika kuingiza watu Ikulu, kwa nini wakose maokoto?

Kuna makundi mawili. Wanamuziki wenyewe, waliojiita mameneja na baadhi ya vituo vya redio. Kuna wasanii husahau kuwekeza katika mambo mengine. Matokeo yake wakipotea kisanii na katika mfumo mzima wa maisha hupotea. Hawa walikuwa wengi miaka ya nyuma. Mameneja au baadhi ya vituo vya redio. Huamini kuwa wana mamlaka ya kuamua nani awike na nani azimike.

Hapo bila kujali uwezo wa mtu wala mvuto wake katika jamii. Hawaoni hatari msanii asipoelewana nao, kumzuia asifanikiwe katika sanaa yake.

Bongo wanavyopenda muziki ni haki msanii kufa maskini? Tuliacha kujadili kwa kina kauli ya Ommy, waja tukaponda na kuona ustaa unamtia wazimu. Ni kama Vinega wa Anti Virus, ila Ommy hakutoa 'miksi tepu' ya mitusi, alitumia hekima mbele ya wajinga. Ommy katika hili, alikuwa sahihi. Sanaa ikisimamiwa vizuri na Serikali ikadhibiti tabia za unyonyaji.

Na wasanii wakiamka na kukataa kunyoywa. Sioni msanii wa kufa maskini. Siyo wa muziki tu, pamoja na waigizaji. Tusizalishe mastaa wenye majina makubwa na umaskini mkubwa.

Kuna kauli kutoka kwa rapa Mkenya Khaligraph Jones. Utofauti wa kauli hizi, ni Khaligraph kaitoa katikati ya sherehe na ile ya Ommy kutolewa ndani ya majonzi mazito. Lakini 'riaksheni' ni ileile kutoka kwa Wabongo.

Wabongo wana tatizo mtambuka la kushindwa kutafakari kauli na vitu mbalimbali. Khaligraph kaponda marapa wetu kuwa wanazingua. Kabla walikuwa vioo kwa kina Khaligraph, lakini kwa sasa wanayumba.

Khaligraph anasema hii leo waliowaona kama kioo chao kwa michano. Hivi sasa wapo 'bize' na Amapiano na makelele mengine. Kwa hili mpaka aje malaika Gabriel ndipo tukiri kuwa kweli marapa wetu wanazingua? Siyo kwa michano tu hata kujiongeza.

Bongo wamekasirika na kuja juu wakimponda msela wa Nairobere. Hawajataka kutafakari na kujua pale walipoteleza. 'Gemu' linapomtegemea mpiga kelele bila 'floz' na 'wedi plei'. 'Gemu' la 'kubustiwa' na Amapiano kuna 'gemu' hapo? Khali yupo sahihi.

Hata 'emsizi' wanaojibu kauli za Khali, ni kama nao wanatumia hizo 'disi traki' zao 'kujibusti' wao wenyewe. Mtu ambaye angejibiwa na mstari tu wa Solo Thang, kajibiwa na kijiji cha marapa. Hapo ndio wanazidi kupigilia msumari juu ya bati la kuishiwa marapa.