Kikosi Kazi: Hatujabebwa na kiki, tunakuja na albamu

Muktasari:

  • Kundi la muziki wa Hip Hop Bongo, Kikosi Kazi limesema ukimya wake ni kutokana na kuandaa albamu, huku wakisisitiza mapokeo yao mazuri kwenye gemu hayajatokana na kiki.

Kundi la muziki wa Hip Hop Bongo, Kikosi Kazi limesema ukimya wake ni kutokana na kuandaa albamu, huku wakisisitiza mapokeo yao mazuri kwenye gemu hayajatokana na kiki.

Ni zaidi ya mwaka mmoja kundi la Kikosi Kazi lipo kimya, mara ya mwisho kutoa ngoma ni Aprili mwaka jana uitwao ‘Amani’ wakimshirikisha Carola Kinasha.

Kundi hilo linaundwa na wasanii wanane kutoka jukwaa la Tamaduni Muzik ambao ni Nikki Mbishi, P Mawenge (P The MC), One The Incredible, Songa, Azma, Stereo, Mansu-Li na ZaiiD.

Akizungumza na gazeti hili, Songa anasema albamu yao imeshakamilika itatoka baada ya kila mmojawao kutoa kazi binafsi.

“Mpaka sasa Mansu-Li, mimi tumetoa albamu, P Mawenge ametoa EP, Nikki Mbishi, ZaiiD na One The Incredible wanakuja na albamu,” anasema Songa. Utakumbuka wimbo wa kwanza wa Kikosi Kazi, ‘Kazini’ ulitoka Julai 2020 baada kundi la Weusi kuwachana Tamadani Muzik katika ngoma yao ‘Interlude Nyeusi’ na wao wakajibu na kupata mapokezi makubwa.

Akizungumzia hilo, P Mawenge anasema mapokezi waliyopata awali ni makubwa, kwani kazi zao zimefanya vizuri mtandaoni na kuwataka mashabiki kupima uwezo na sio kukariri kile wanachosikia.

“Kuna wanaodhani tulifanya vizuri kwa sababu ya msuguano uliotokea wakati ule, tunachowaomba mashabiki zetu wapime uwezo wa kazi zetu wasisikilize maneno ya kupandikizwa,” anasema Mawenge. Nyimbo walizoachia mpaka sasa ni Kazini, Sala, Fanya Wewe, Anthem ft. Chibwa, Miss 2020 ft. Kita The Pro, Mamelody ft. Gossby, Last Warriors wakishirikiana na wasanii wa Kenya, Kaa la Moto, Breeder LW, Trabolee, Kayvo Kforce na Romi Swahili.


HISTORIA YA KIKOSI KAZI


Kundi hili linaundwa na wasanii wanane ambao wamefanya kazi nyingi pamoja kwa kutengeneza jukwaa la Tamaduni Muzik ambapo ndani yake kulikuwa na wasanii kutoka lebo na makundi tofauti. Mfano Nikki Mbishi, One The Incredible, Stereo na Songa hawa walikuwa chini ya lebo ya M Lab, Nikki na Stereo walikuwa chini kundi la Lunduno, baadaye wakaanzisha kundi lingine, Sisi The Trio, ambalo kuna Nikki, One na Stereo. Hata hivyo, One tayari alikuwa ndani ya kundi la Illmatix pamoja na Songa, huku ZaiiD na P Mawenge walikuwa sehemu ya kundi la Sisi Sio Kundi (SSK).


Kuhusu bifu la P Mawenge na Nikki Mbishi

P Mawenge ameweka wazi kuwa bifu lake na Nikki Mbishi lilimalizika baada ya kuitwa na watu wanaowaheshimu katika sanaa, na kuwataka kumaliza tofauti zao zilizoibuka na kuteka mazungumzo hasa mtandaoni.

“Tulimaliza kimya kimya bila kuhusisha vyombo vya habari, pili wakati tunalitatua hilo ilikuwa ni kile kipindi cha Uviko-19 na kulikuwa hamna namna ya kukusanya watu na kuwajulisha, hivyo tukalimaliza wenyewe kindugu,” anasema. Wawili hao waliingia katika vita ya maneno pale P Mawenge alipoamua kujibu ‘diss’ ya Nikki Mbishi aliyoitoa kwenye wimbo’Straight Outta Gamboshi’ kukosoa vikali kitendo cha wasanii wa Hip Hop akiwamo Mawenge kupiga picha na Rapa Cassper Nyovest nchini Afrika Kusini badala ya kuomba kolabo, kwa kuachia wimbo wake uitwao ‘Futi Sita’.