Kikwete ataja kilichomponza Steve Nyerere kwa Ommy Dimpoz

Muktasari:

  • Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema kilichomponza msanii Steve Nyerere ni kusema Ommy Dimpoz hataweza tena kuimba.

Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema watu wengi walikuwa wanaamini msanii Ommy Dimpoz asingeweza kurudi kuimba tena lakini kiherehere cha Steven Mengele maarufu kwa jina la Steve Nyerere cha kujitokeza na kuliongea hilo hadharani ndicho kilichomponza.

Siku chache baada ya Ommy kutoka kwenye matatibabu akihohiwa na chombo kimoja cha habari, Steve alisema Ommy hatoweza kuimba tena kutokana na eneo alilofanyiwa upasuaji ndilo ambalo linahusika kwa kiasi kikubwa na utoaji sauti.

Kauli yake hiyo ilisababisha watu mitandaoni kumshambulia mchekeshaji huyo na kumtaka amuombe radhi Ommy.

Usiku wa kuamkia leo Novemba 6 katika uzinduzi wa albanu ya Ommy inayokwenda kwa jina la Dedication, Steve ameitwa jukwaani na Ommy ambapo alimwambia Rais huyo mstaafu kuwa ametekeleza agizo lake la kuhakiksha hakosi kumualika msanii huyo.

Akikumbushia kauli aliyoitoa kwa Ommy, Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, amesema msanii huyo kilichompoza ni kiherehere chake kutoka hadharani kusema kuwa mwenzie huyo hataweza kuimba lakini ukweli ni kwamba kwa hali waliyomuona Ommy hata wakati anahojiwa na kutoa sauti kwa shida wengi waliamini hilo.

"Nilimwambia Dimpoz amualike Steve kwa kuwa yeye alikuwa miongoni mwa watu walioamini kuwa jamaa asingeweza kuimba tena na hakuwa peke yake ila yeye tu ana kiherehere

"Ila ukweli amewasemea wengi ambao walikuwa wanaamini jamaa amefika mwisho, sasa kiherehere chako kimekuponza," amemwambia Steve kiongozi huyo.

Kwa upande wake Steve ambaye kila alichokuwa akizungumza kilikuwa kikiwavunja mbavu wahudhuriaji wa hafla hiyo kwa kucheka alimuomba tena radhi Ommy na kufuta kauli yake hiyo licha ya kuwahi kufanya huko nyuma baada ya kukutana naye.