Kikwete kuzindua albamu ya Ommy Dimpoz

Muktasari:

  • Albamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa sehemu tatu tofauti katika jiji la Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Omar Nyembo maarufu 'Ommy Dimpoz' kesho Novemba 5, 2022 anatarajiaa kuzindua albamu yake huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

 Ommy Dimpoz ameyasema hayo leo Ijumaa Novemba 4, 2022 kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu ujio wa albamu hiyo.

Albamu hiyo aliyoipa jina la Dedication,itakuwa ni albamu yake ya kwanza kuotoa tangu alipoanza muziki miaka kumi iliyopita.

Akieleza sababu za kumualika Kikwete, Ommy amesema ni kutokana na kuwa mmoja wa viongozi anayependa muziki wa Bongo Fleva na kwamba amekuwa karibu naye kama baba yake.

"Mzee wetu huyu amekuwa akipenda sana kazi tunazozifanya, hivyo nikaona nimualike kuja kushuhudia albamu yangu hiyo ya kwanza na kupata maoni yake.

"Lakini pia amekuwa mshauri na baba kwangu kwani hata wakati nilipokuwa naumwa alikuwa akiwasiliana nami mara kwa mara na kunipa msaada wa hali na mali," amesema msanii huyo.

Kuhusu albamu yake hiyo, amesema ina nyimbo 15 huku moja ya sababu ya kuifanya ni kutokana na soko la muziki kwa sasa kutaka hivyo.

"Tunakutana na wafanyabiashara mbalimbali huko duniani na unapotaka kufanya nao kazi wanakuuliza albamu yako ipo wapi, hivyo nimeona ni wakati sasa nami kutoa albamu ili nifanye biashara," amesema Ommy.

Sababu nyingine alisema ni kutokana na kuwepo kwa majukwaa mbalimbali kwa sasa ya kuuza kazi za muziki tofauti na huko nyuma ambapo walikuwa wakitegemea watu wawili watatu nchini kuwasambazia kazi zao.

Pia uharamia wa kazi zao ni moja ya jambo lilolomrudisha nyuma kutoa albamu hasa walipokuwa walipotoka kwenye mfumo wa kutumia kaseti na kuhamia kwenye santuri (CD) ambazo pia watu walizidurufu.

Ommy kwa mara ya kwanza kwenye muziki alitambulika na wimbo wake wa Nainai na baadaye kuepua vibao vingine ikiwemo Baadaye, Me and You aliyoimba na Vanessa Mdee, Tupogo, Kajiandae na sasa akiwa anatesa na kibao cha Vacation.

Albamu hiyo ya Ommy inatarajiwa kuzinduliwa sehemu tatu tofauti katika jiji la Dar es Salaam, ambapo mbali na hoteli ya Rotana kesho, pia kutakuwa na ahafla itakayofanyika klabu ya Element Masaki na siku ya Jumapili itapelekwa ufukweni Kidimbwi Mbezi Beach.