Kuna chawa, sanaa, tamaa na njaa

Sunday May 02 2021
sanaa pc

YES! Kuna wana, wanasanaa ndani ya miili, mioyo na akili. Wanaishi kwa sanaa, wakifanya kama sehemu ya maisha yao ya kila siku. Hawa wako makini na miiko na mioyo yenye dhamira ya dhati. Kuanzia kazi yenyewe, matendo, utembeaji mpaka uvaaji wao. Iko hivyo.

Hawa huwezi kuona wakifanya sanaa ili wasikike. Mara nyingi hukasirika pindi sanaa inapochezewa. Hawa ni watu ‘projekti’ kila baada ya ‘projekti’, kila siku kinachofuata ni ‘projekti’. Haijalishi ‘gemu’ limejaa watata. Wanafanya sanaa hata watata huishia kudata na mashabiki kufuata.

Lakini kuna wenye tamaa ambao hufanya sanaa kutokana na mafanikio ya mtu fulani, kwenye sanaa yake. Hawa mara nyingi wanakuja na kutoweka kama upepo wa Jobo. Wanashindwa kudumu, kwa sababu hawana misingi mizuri katika sanaa.

Kwao wanaamua kutaka kupata anachopata mwenzao, na siyo kufanya kilichopo moyoni mwao.

Hawa sanaa hata ikiwapa pisi nzuri wanaachana na sanaa yenyewe. Wanakuwa bize na pisi kali kitaa, wakiishi kwa kivuli cha sanaa miaka yote.

Huamini kuwa sanaa ni kwa ajili ya kumiliki pisi kali mjini. Hawana mwendelezo mzuri na huishia kuponda kila linalofanywa na wenye sanaa toka ndani ya damu zao. Sampuli hii ndio wapondaji mitandaoni na kitaa.

Advertisement

Kuna wale wenye kufanya sanaa kwa sababu ya njaa zake. Hawana sanaa mioyoni wala kwenye akili zao za kawaida.

Lakini baada ya kupigika huko kwao huko, wanaona mchongo wa fasta ni kufanya sanaa. Hawana wito wala ari ya sanaa, njaa zinawasukuma kuifanya. Hawana mwisho mwema na mara nyingi ndio wale wanaoishia kuitangaza sanaa kama kitu cha ovyo.

Yes! Wanafanya wanalotaka hata la kudhalilisha utu wake mwenyewe, mradi akitajwa au kuzungumziwa kila kona, kwao ni mafanikio. Njaa zinafanya ajitoe ufahamu kabisa. Hawa ni miongoni mwa sampuli ya watu wanaorudisha nyuma sana hii sanaa ya Bongo. Wanafaa kupigwa vita, wasionewe haya wala soni.

Hapa ndipo utaona anatupia picha za utupu kwenye mitandao. Hawa ni wasanii wenye njaa au tamaa. Ni virusi kwa sanaa zote Kibongo. Na wako wengi kuliko wenye sanaa ya kweli mioyoni mwao. Wa kike hutumia sanaa kupata madanga, wa kiume huitumia kupata masponsa ya kike. Ambayo hayana akili zaidi ya kumiliki pesa.

Wakati kuna mandezi ambao wakishapata pesa huko wanakojua, huwaza kukamatia staa flani wa muziki au filamu. Basi kuna msanii naye anawaza kuuza sura na shepu, ili apate matutusa hayo ya aina hiyo. Ni kama nyumbu mbili zinazoviziana ili zitafunane. Hizi ni ngedere zinazotafuna mazao ya sanaa na kusepa.

Na sanaa zetu zimevamiwa kwa kiwango kikubwa sana na kupelekea kuelewa nani ni shabiki na nani ni mwanamuziki. Sasa hivi wanaishia kujitofautisha kwa kujiita chawa wa fulani, na huyu chawa wa yule. Mwanasanaa unaamua kujitoa akili kwa kujiita chawa wa mwanasanaa mwenzako. Hizi ni akili za kimatope zenye mafuta ya taa ndani yake.

Aliyejulikana kama shabiki miezi mitatu nyuma, leo anajiita mwanasanaa. Aliyejiita mwanasanaa miezi miwili nyuma, leo anajiita shabiki wa mwanasanaa. Yaani shabiki anakuwa msanii na msanii anakuwa shabiki wa msanii. Hapa kuna mchanganyiko mbaya sana, ambao hupelekea kuzalisha matakataka matupu kwenye sanaa yetu.

Kinachokera ni kwamba, hawa chawa hawa. Wamekuwa na nguvu zaidi kuliko wanasanaa wenyewe. Hatuwezi kuzuia hii hali, kinachokera ni kile kinachoendelea sasa hivi. Na wasanii wenyewe wakitumia chawa wao kuharibu mazingira kwenye sanaa yetu. Chawa wamekuwa kama vimbunga, wana nguvu kuliko mademu wa wasanii.

Hivi sasa ukitaka kujua msanii fulani ana mipango gani, mtafute chawa wake, ndio wanaoelezea kila kitu, na wanaaminika kwa sababu wanachosema ndicho wanachofanya. Chawa huyu anasema kuwa msanii fulani atafanya hili. Na kweli kesho unaona msanii huyo akifanya hivyo hivyo, huku akiwa na yuleyule chawa. Kwa nini wasiaminike?

Chawa wa siku hizi wanawachagulia wanasanaa rafiki, demu, vazi na kipi cha kuongea.

Mwanasanaa anaishi kwa maelekezo au matakwa ya chawa wake. Na chawa nao wanaona ni sifa namba moja kuitwa chawa. Hii kwa lugha ya zamani waliitwa wapambe. Kizazi kile walisema wapambe nuksi, sasa kizazi hiki kiseme chawa nuksi.

Kuna tatizo hivi sasa. Tatizo la kugeuza sanaa kama ‘shoorumu’ kwa baadhi ya watu. Sanaa inatendwa na kulipwa baya badala ya jema. Sanaa haina kosa, ila kosa lipo kwa wakosaji wanaoitumia sanaa. Ni baadhi tu kati ya kundi kubwa la sanaa na wanasanaa, ambao wanafanya haya. Sanaa imejaza wenye njaa, tamaa na chawa.

Wakati zamani wanasanaa walipokezana vijiti, hawa wenye chawa wa leo wanapokezana kiki. Ndiyo mchongo uliopo mezani kwa wengi wao. Kiki imekuwa sehemu ya sanaa na wasanii popote.

Kiki imekuwa kama maiki, gitaa, ngoma, kinanda nk. Wanatuaminisha hilo kwa matendo na maneno yao ya kila siku. Ukisikia skendo ya msanii, kesho anaachia ngoma mpya.

Kiki zinavuka mipaka, utu na utamaduni wetu hii leo. Sasa kiki zimepata ujauzito na sasa zimejifungua kitoto kiitwacho chawa. Ndani ya kiki kuna chawa na ndani ya chawa kuna kiki. Wakati kiki ni matendo au tukio, chawa ni watu ndani ya watu na kiki zao. Kifupi ni kwamba kiki zimezalisha chawa, na sasa chawa wanazalisha kiki.

Chawa wana sauti kuliko wazazi wa wanasanaa. Na sasa chawa wanataka kuwa mahakama ya maamuzi ya migogoro ya sanaa na wanasanaa. Wanataka kuwa Baraza la Sanaa (Basata), kuwa visemeo vya wanasanaa na sanaa yenyewe. Wanajikuta juu ya utaratibu wa sanaa na wasanii.

Chawa wamekuwa sehemu ya vichocheo vya migogoro ya wasanii. Na chawa wapo wa aina nyingi, watu kama watu. Na kuna kurasa za watu mitandaoni, nazo zinafanya kazi ya chawa kwa kupitia akili za chawa wenyewe. Wamiliki wa hizi kurasa mitandaoni wengi ni chawa wa wasanii, ambao hulipwa au kupewa ‘ofa’ kwa uchawa wao.

Wanatumika kudhoofisha wasanii na sanaa. Kwa kutengeneza mazingira ya ovyo ya uhusiano wa wanasanaa. Bahati mbaya sana, chawa hutengenezwa na wanasanaa husika. Ni kirusi kinachotafuna sanaa. Huu uwe wakati wa kuua chawa wote, ili ‘kumeinteini’ sanaa iwe na stamina.

Hatuwezi kusifia kuwa sanaa imekua kwa kuwatazama wasanii wawili au watatu, ambao kimsingi wamezungukwa zaidi na chawa kuliko wasanii wenzao. Tutakuwa tunajiongopea tukisema muziki umepanda. Muziki unashuka sana Bongo na wanaotamba ni walewale. Filamu pia zimeshashuka kitambo. Ila kuna wanamuziki na waigizaji wachache ndio wako juu. Nje ya sanaa lakini.

Advertisement