Kuna siri kati ya HipHop na uongozi?

Sunday June 27 2021
hiphopic
By Peter Akaro

Wiki hii msanii wa hip hop Bongo, Nickson Simon ‘Nikki wa Pili’ ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuiongoza wilaya hiyo akichukua nafasi ya Jokate Mwegelo, aliyehamishiwa Temeke.

Rapa huyo kutoka kundi la Weusi anakuwa ni msanii mwingine wa hiphop nchini kushika nafasi kubwa ya uongozi. Hawa ni baadhi ya wasanii wa muziki huo waliowahi kuwa viongozi hapo awali na hata sasa. Je, siri ni ipi hasa? Karibu.

1. Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ Mbunge

Huyu ndiye msanii wa kwanza wa hiphop kutoka kwenye Bongofleva kuingia bungeni kwa kura za wananchi, mwaka 2010 alishinda kiti cha Ubunge jimbo la Mbeya Mjini.

Mwaka 2015 ndiye aliongoza kwa kuchaguliwa na wapiga kura wengi kuliko mbunge yeyote kati ya wabunge 257 waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu mwaka huo. Sugu alifanikiwa kupata kura 108,566 kati ya 166,256 zilizopigwa, na kuwaachia wengine wakigawana kura 57,690.

2. Joseph Haule ‘Profesa Jay’

Advertisement

Novemba 2015 Profesa Jay akawa msanii mwingine wa hip hop kushinda ubunge kupitia kura za wananchi wa Jimbo la Mikumi, Morogoro baada ya kupata kura 32,259, huku mshindani wake wa karibu, Jonas Nkya akiambulia kura 30,425.

Tofauti na Sugu, licha ya Profesa Jay kushinda ubunge aliendelea kufanya muziki pamoja na kutumbuiza kwenye matamasha makubwa, na hata aliposhindwa kwenye Uchuguzi Mkuu 2020 ameendelea na kazi yake ya awali na sasa anatamba na ngoma, U’taniambia Nini’.

3. Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 Mwana FA naye akafanikiwa kushinda nafasi ya ubunge wa Jimbo la Muheza, Tanga kwa kupata kura 47,578, huku mshindani wake wa karibu, Yosepher Komba akipata kura 12,034.

Kwa mtiririko huo, utaona toka mwaka 2010, 2015 hadi 2020 kila uchaguzi mkuu umekuwa ukipeleka msanii wa hip hop bungeni na sasa wameanza kutoa wakuu wa wilaya. Je, kuna uhusiano gani kati ya muziki huo na uongozi?

Wasanii wafunguka

Akizungumza na gazeti hili, Rapa Fid Q amesema wasanii wa muziki huo wanaonekana kupata nafasi zao za uongozi duniani kote kutokana hiphop ni muziki wa kufikirisha, lakini mara nyingi huwa umejikita katika kuwasilisha mambo yanayoendelea kwenye jamii.

“Mara nyingi wasanii wa hip hop wanaimba changamoto ambazo zipo katika mazingira yanayowazunguka, kwa hiyo hilo hupelekea jamii kuona ni watu ambao wanafaa kiuongozi kutokana na kutumia sanaa kupaza sauti, kuwasemea wasiokuwa na nafasi ya kusema kuhusu changamoto zao, pia kuwa nao karibu na kuthamini maoni yao” anasema.

“Hiphop haiandai wasanii wake kuwa viongozi, ila unapokuwa msanii wa hip hop moja kwa moja unajikuta umekuwa kiongozi kwa sababu ni gemu la kishababi, kwa hiyo unapokuwa una mawazo ya kishababi huwezi kuwa mtu ambaye unafuata, inabidi uwe unaongoza,” anasema Fid Q.

Naye Nikki wa Pili katika mahojiano na gazeti hili kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka jana, alisema anaamini kila msanii bila kujali aina ya muziki au sanaa anayofanya anaweza kuwa kiongozi, ila itategemea zaidi namna anavyojiweka mbele ya jamii.

“Unaweza kuwa msanii wa hip hop lakini wakakupima wakaona huna hoja, wote tunaona Vick Kamata ni msanii wa kuimba lakini amekuwa mbunge. Kwa hiyo naona ni jinsi mtu anajiweka kibinafsi, sioni kama ina uhusiano na kuwa mwana-hip hop au kutokuwa,” anasema.

Aliendelea kwa kusema, “naona pia wasanii wa kuimba wana nguvu kama wakiamua kwenda wanaweza kufanya vizuri, lakini kama nilivyosema itaanza na wewe mwenyewe. Wanaweza kukuamini kama msanii, je, wanaweza kukuamini kama kiongozi?” anasisitiza.

Naye mtayarishaji wa muziki kutoka studio za Combination Sound, Man Water anasema kwa kiasi kikubwa muziki wa hiphop haujajikita kwenye kuburudisha, bali katika harakati za ukombozi wa kifikra.

“Ni kwa sababu ya maudhui ya hip hop yenyewe au asili yake ambayo ni harakati, hata wasanii wa rege ukiangalia maudhui ya nyimbo zao huwa yamelenga sana kwenye kukomboa fikra za watu na masuala ya kijamii. Sio watu ambao wapo kwenye kuburudisha sana ndio maana umeona kwenye baadhi ya nchi wanajitokeza kwenye harakati za kisiasa na kijamii” anasema.

Rapa Kala Jeremiah anasema hiphop sio muziki tu, bali ina misingi yake na mfumo wake, hivyo wasanii wanaoishi katika mambo hayo mawili wana nafasi kubwa kujitengeneza na kuonekana wanafaa kuwa viongozi.

“Hip hop kimfumo wake imekaa kiuongozi, unajua uongozi ni kusikia au kuona changamoto ya mtu na ikakuhusu, sasa unapotaka kuwa mwana-hip hop lazima uongee changamoto za wengine. Hivyo katika kutekeleza hilo ndio unajikuta umesimama kama kiongozi wao,” anasema Kala.

Kwa upande wake rapa Chemical, ambaye ni mshindi wa kwanza wa tafiti bora Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 2020/21, anasema suala hilo ni jinsi mtu alivyojiweka binafsi, kwani hata wanaofanya hiphop kuna muda wanabadilika na kufanya aina nyingine ya muziki.

“Ikija kwenye uongozi mimi naona ni dhamira ya mtu na amejipangaje kuupata, kwa hiyo sitaki kusema kuwa wana-hiphop ndio wanafaa sana kuliko wanaofanya aina nyingine ya muziki, hapana! Ni mtu amedhamiria nini na ameweka kipaumbele gani, kama mtu amejiwekea mazingira mazuri ya kuwa kiongozi baadaye, atafanikiwa kufanikisha hilo,” anasema Chemical.Advertisement