Kwa hili la Ashura, mbengo zitofongoka

Sunday May 29 2022
ashura pic

Ni nusu mwaka sasa tunaukata. Kuna jipya? Yes! Mapya yanaibuka kila siku kuanzia asubuhi mpaka jioni. Uwezo wetu wa kuzalisha vituko tungewekeza kwenye kuzalisha uwele, mtama au mbaazi tungekuwa matajiri sana. Tusingekuwa na shida kabisa.

Wakati ukishangaa sarakasi za mbunge akiwa ndani ya Bunge. Ghafla unasikia la Tulia International Airport. Hujakaa ukatulia unasikia mbunge anamwaga chozi bungeni. Jambo la msingi wewe usizime data washa muda wote.

Unachomoka zako kazini kurudi kitaa. Unapita kwenye kiota chako upate kuupumbaza ubongo. Maana mitungi kazi yake ni kupumbaza ubongo. Ujione huna dhambi, huna shida wala madeni. Zikiisha asubuhi ndio unatia akili.

Wakati mhudumu anamimina mvinyo kwenye glasi, mbele yako runingani unamuona Kamanda Jumanne Muliro. Kwa umakini unataka kujua kuna lipi? Akili yako ikijielekeza kwenye ‘ishu ya Panya Road.’ Maana ndio pasua kichwa.

Unakutana na taarifa ya Bi Ashura wa Tabata ‘kumteka’ diwani. ‘Nshomile’ kaacha hekalu lake huko Mikocheni ushuani. Kaenda kujisalimisha kwa pisi uswazi huko, sijui Tabata Liwiti, sijui Senene kama siyo Mawenzi au Barakuda. Watajua wenyewe.

Stori inakupa hamu ya kutaka kujua zaidi. Diwani anatoweka ‘homu’ muda wote huo bila kujulikana alipo? Jambo linafikirisha na kugeuka ‘memezi’ ya wiki. Mpaka hapo kichwa kinawaka moto kwa wingi wa matukio.

Advertisement

Ndani ya siku tatu tu, matukio ni mengi kuliko idadi ya ndevu kwenye kidevu cha Petro au Osama. Sisi tumeamua kuzalisha vituko kila sehemu. Iwe mahakamani, bungeni au mitandaoni. Huko kwenye soka achana nako kabisa.

Sina maana hivi vituko havifai, hapana. Vinafaa na kwa sasa ndio vinafaa zaidi. Wakati bei ya mafuta ikitutia unyonge na mfumuko wa bei. Linaibuka suala la Panya Road. Akili zinahama jumla na kusahau shida zetu kwa muda.

Wakati nauli zikiwa mwiba mchungu. Tunaliwazwa na sarakasi na kilio cha mbunge. Kisha tunawekwa sawa na ‘ishu’ ya Bi. Ashura. ‘Veri interestingi’, Nshomile kumtoa Mikocheni mpaka uswazi Tabata, siyo jambo dogo mjue.

Tabata ndiko ambako mtu anakwenda dukani kununua vocha anarudi kalewa. Na hapa ndipo nagombana na Bongo Movie. Stori kama hii kama itaandikiwa muswada mzuri na ‘sripti’ tamu, yenye muongozo mzuri. Ni pesa ndefu sana.

Lakini, wao wanaleta stori za Juma na Uledi, mambo ya maskini kapendwa na mtoto wa tajiri. Kama lile Zali la Mentali la Profesa Jay. Panya Road yenyewe ni pesa kwenye filamu lakini yuko wapi wa kuitazama hiyo kama fursa? Hakuna!

Watanzania tunatengeneza matukio mengi ya filamu lakini tunakosa jicho la pesa. Tunaacha ‘peji’ za udaku instagram zisambaze bila kuzama ndani kwa kina. Ashura ni pesa ya wazi kwa jicho la filamu, lakini itaishia kuchekesha watu mitandaoni na kupita kama corona tu.

Tatizo wasanii wetu wengi wakiamka wanawaza uchawa kwa wanasiasa. Na ‘kutrendi’ kwa vituko na kujianika miili huko insta. ‘Komenti’ na ‘laiksi’ za ‘folowazi’ zina mvuto kwao kuliko namba kwenye akaunti kupitia sanaa yao.

Unaweza kuwa msanii mwenye pesa lakini hujivunii zile pesa kisanii. Kwa sababu hazitokani na sanaa. Hakuna pesa tamu kwa msanii kama inayokuja kupitia sanaa yake. Siyo tu tamu, pia ina thamani kubwa zaidi.

Pesa za nje ya sanaa zinawapa kichaa na wengi wao kuzitapanya hovyo. Huwezi kujiita msanii kama maisha yako unayaendesha kiuchawa chawa tu. Hii siyo poa.

Soko la filamu Bongo halijafa ila akili za kifilamu ndio zimekufa. Unasemaje soko limekufa wakati wasanii wanafuatiliwa zaidi kila siku mitandaoni? Tatizo ni wale ‘folowazi’ wanalishwa chakula cha nje ya sanaa yao ila kwa sababu ni bure freshi tu.

Ukienda kwenye kurasa zao mitandaoni wanachoposti ni tofauti na ‘mataito’ yao ya sanaa. Lakini watu wanawafuatilia na hata tamthilia zao zinafuatiliwa sana. Ni vipi filamu zipate kikwazo? Usambazaji? Hii siyo sababu.

Muziki na filamu hufanyika kabla ya wasambazaji kuwepo. Hitaji la walaji lilipokuwa kubwa likafanya wenye pesa wawekeze kwenye usambazaji. Na ndicho kitu kinatakiwa kufanywa leo hii. Ubora wa kazi utaleta kila kitu mezani.

Ukiwa na kazi nzuri, watakuja walaji, hitaji likiwa kubwa watakuja watu wa kati ambao ndo wasambazaji.

Pia, wapo watakaohitaji taswira ya msanii husika. Kampuni, biashara na ubalozi wa taasisi. Ndivyo pesa ya msanii ilipo achani kuzubaa nyie!.

Sanaa ina eneo pana sana la kuingiza mamilioni ya pesa, mbali na kudurufu kazi na kuzisambaza. Sanaa siyo mauzo tu ya kazi yako, pia taswira na sauti ni pesa nyingi pengine kuliko mauzo ya filamu husika. Yes!

Lakini yote haya yatakujaje? Utajiri wa msanii huletwa na ubora wa kazi yake. Kazi bora kwa filamu ni ipi? Namba moja ni stori nzuri. Namba mbili ni stori zuri. Na namba tatu ni stori nzuri. Kisha endelea na mengineyo.

‘Skripti’, ‘lokesheni’, ‘editing’ na mengine mengi hutegemea ubora wa stori. Kama msanii utakuwa na stori bora, huhitaji kuwa na gari la kifahari, mrembo mkali, nguo za thamani na kamera za mabilioni ili upige bao.

Lakini wasanii wetu wengi wanazingua kwenye ubora wa stori. Wanalipua na kuungaunga sana. Matukio ndani ya Bongo yapo mengi yanayogusa sana hisia za watu, lakini wasanii hawataki kuyatumia kama fursa. Kugeuza pesa.

Mtu akilibeba tukio la Ashura ambalo wengi wanageuza kichekesho. Na siyo tukio hilo tu, yapo matukio mengi sana. Ambayo Bongo hatuyatazami kifursa. Akaliweka kisanii zaidi, ile ni pesa. Na hakika “mbengo zitofongoka, acheeea!”


Advertisement