Leo ni leo, Tyson Fury kuzichapa na Francis Ngannou

Mabondia Tyson Fury (kushoto) na Francis Ngannou (kulia)

Muktasari:

  • Leo Oktoba 28, 2023, Mwanamasumbwi Francis Ngannou maarufu "The Predator" anapanda ulingoni kuzichapa na bingwa wa ndondi wa uzito wa juu, Tyson Fury, huko Riyadh, Saudi Arabia.

Dar es Salaam. Leo Oktoba 28, 2023, Mwanamasumbwi Francis Ngannou maarufu "The Predator" anapanda ulingoni kuzichapa na bingwa wa ndondi wa uzito wa juu, Tyson Fury, huko Riyadh, Saudi Arabia.

BBC imeripoti kuwa pambano hilo linaelezewa na mashabiki wa michezo kama moja ya mapambano makubwa ya ndondi ya karne hii, na ni mtihani mkubwa kwa Ngannou.

Hata hivyo, swali ambalo mashabiki wengi wa michezo huu wanajiuliza ni Je, Ngannou ataweza kumshinda Tyson Fury ambaye hajawahi shindwa katika mapambano yake?

Wakati Ngannou ameibuka kutoka katika mchezo unaojumuisha aina zote za mapigano kama vile ndondi, mateke, mieleka, ngumi (MMA); kwa upande wa Fury ni tofauti kwani mwanamasumbwi huyo yeye tangu mwanzo anatumia mikono pekee.

"Kitaalamu itakuwa ngumu kwa Francis Ngannou ambaye amezoea MMA - kukabiliana na bondia bora zaidi duniani," ameeleza Léandre Nzie, mwandishi wa habari wa Cameroon.

Francis Ngannou alizaliwa katika familia masikini. Akiwa mdogo alikutana na changamoto kadhaa katika maisha ambazo zilimfanya kuchukua majukumu ambayo watoto wa umri wake, wasingeweza kuyabeba.

“Nilikuwa na umri wa miaka 10....Baada ya kuondoka nyumbani kwetu, nilienda kwa bibi yangu, Iinibidi kufanya kazi ili kuchangia huduma za nyumbani; kununua mafuta, chakula na kwa masomo kununua vitabu,” ameeleza Ngannou katika kipindi cha mtandaoni cha Joe Rogan.

"Lazima ufanye kazi na hivyo ndivyo nilivyoanza, ingawa kazi hii ilikuwa ya watu wazima, lakini sikukuwa na chaguo jingine," anaelezea bingwa huyo wa zamani wa Ultimate Fighting Championship (UFC).

Francis Ngannou alifanya kazi katika migodi ya mchanga hadi alipokuwa na umri wa miaka 17.

Kadiri umri ulivyosonga, matatizo yaliendelea kurundikana kwenye mabega ya Francis ambaye anataka jambo moja tu: kutimiza ndoto ya kuwa bingwa wa ndondi.

Kwa hiyo aliamua kuhamia Ulaya kwa kusafiri njia inayotumiwa na maelfu ya wahamiaji kwa kuvuka Jangwa la Sahara kisha Bahari ya Mediterania hadi Ufaransa, ambako hakuacha wazo la kujihusisha na ndondi.

Ambapo katika jitihada hizo, alifanikiwa kuingia katika mashindano ya MMA na kuwa bingwa.

BBC imeendelea kuripoti kuwa Ngannou alifaulu kuonyesha ustadi wake wa mieleka wakati wa pambano dhidi ya Mfaransa Cyril Gane na kuubakisha mkanda wake wa ubingwa wa UFC wa uzito wa juu.

Licha ya mafanikio yake, baadaye aliamua kuondoka. "Unajua kwamba mkataba wa UFC unaweza kuwa na vikwazo na huna la kusema." Francis Ngannou alisema wakati anatoa tangazo la kuachana na UFC.

Baada ya kuondoka UFC, alifanikiwa kutia saini Ligi ya Wapiganaji (PFL), shirika jingine la MMA, ingawa ni la hadhi ya chini kuliko UFC.

2015, pambano lake la kwanza UFC: Francis Ngannou alipigana katika pambano lake la kwanza dhidi ya Mbrazili Luis Henrique baada ya kusaini UFC. Alishinda kwa kumpiga KO mpinzani wake katika raundi ya pili.

Kipigo cha kwanza akiwa UFC: Baada ya mfululizo wa ushindi, Francis Ngannou alipigana na Stipe Miocic aliyekuwa akitetea mkanda wake. Ngannou alipigwa katika pambano hilo.

Bingwa wa UFC uzito wa juu: Miaka mitatu baada ya pambano lao la kwanza, Miocic alitaka kutetea taji lake tena dhidi ya Mcameroon huyo. Francis Ngannou alifaulu kumshinda Miocic na kushikilia ukanda wa uzito wa juu.

Pambano lake dhidi ya UFC: Wakati Francis Ngannou alipotangaza kuondoka UFC, baadhi ya watu walishuku kwamba atarudi kwenye ulimwengu wa MMA. Hata hivyo, aliweza kuwanyamazisha baada ya kutia saini mkataba wa kihistoria na PFL.

Akiwa na PFL, Francis Ngannou alipata uhuru aliokuwa ameutaka kutoka kwa UFC. Kuanzia sasa, ataweza kupigana kwenye ndondi - ndoto yake ya utotoni.

Pia atapata sehemu ya faida inayotokana na PFL kwenye hafla anazoshiriki. Mnyama huyo pia ameteuliwa kuwa balozi wa shirika hilo katika bara la Afrika.

Kwa mwandishi wa habari, Francis Ngannou ni nembo kwa vijana wa nchi yake.

"Francis ni kielelezo cha ustahimilivu, ni ishara ya ndoto iliyotimizwa kwa nguvu na mikono yake."

Oktoba 28, Francis Ngannou atatimiza ndoto yake ya utotoni. Anasaidiwa katika maandalizi na lejendari Mike Tyson ambaye pia atakuwa pembeni yake huko Riyadh.

Chanzo BBC