Lulu apata mtoto wa pili, mumewe Majizo athibitisha

Muktasari:

Lulu amepata mtoto ikiwa imepita mwaka na miezi mitano tangu alipojifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume

Dar es Salaam. Msanii wa filamu , Elizabeth Michael, maarufu ‘Lulu’ amepata mtoto wa pili wa kike na kumpa jina la Grecious.

Lulu amepata mtoto ikiwa imepita mwaka na miezi mitano tangu alipojifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume.

Taarifa hizo zimetolewa leo Jumanne Desemba 27,2022 na  Lulu kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, huku mumewe Majizo akilithibitisha hilo kwa kuandika, “Imekuwa ya baraka tele katika nyumba yangu, mimi na mke wangu Eliza tumejaaliwa mtoto wa pili.

“Bwana G anatamba kuwa kaka, amepata mdogo, mdogo naye anaitwa G, tunamshukuru sana Mungu wa mapendo kwa zawadi hii kubwa mno.


Majizo ameongeza, “Namshukuru sana na kupongeza mke wangu Elizabeth Michael kwa hili ambalo ni mwendelezo wa mengi yanayomfanya aendelee kuwa mama bora kwa watoto wetu na mke mwema kwangu.

 “Tuzidi kuombeana heri, Mungu awajalie watoto wetu (wangu na wenu) kukua kwema, wawe watu hodari, wacha Mungu na wenye mafanikio makubwa.

Akijibu ujumbe wa mumewe, Lulu ameandika, “Ahsante kwa kuwa baba bora kwa watoto wetu na mume hodari kwangu,”.

Mtoto huyo wa Lulu, anamfanya Majizo ambaye jina lake halisi ni Francis Ciza, kuwa na watoto wawili wa kike na watatu wa kiume.