Mabadiliko makubwa Tuzo za Oscars Jumapili

Saturday April 24 2021
oscarpic

Los Angeles, Marekani (AFP). Kutoka kampeni ya kupinga ubaguzi katika kutuza wasanii bora wa filamu, mfumo dume hadi janga la virusi vya corona lililosumbua dunia, tamasha la Oscars litakuwa na mabadiliko makubwa wakati litakapofanyika usiku wa kuamkia JUmatatu.

Wasanii wa rangi kutofauti-- weupe, weusi hadi wa asili ya barani Asia-- wametajwa kuwania tuzo tofauti katika tamasha hilo kubwa duniani ambalo lilikuwa likikosolewa kwa ubaguzi, hasa kutokana na muundo wa wapigakura.

Wachezaji filamu wa rangi tofauti wametajwa kuwania tuzo karibu katika vipengele vyote, na waongozaji wanawake wawili wametajwa kuwania tuzo kwa mara ya kwanza na kulipa nafasi tamasha la mwaka huu kuandika historia mpya.

oscarpicc

Taasisi inayoandaa tamasha hilo ya The Academy of Motion Picture Arts and Sciences, imefanya mageuzi makubwa katika miaka ya karibuni, ikiingiza kundi kubwa la wapigakura kila mwaka na ambao wanaakisi vizuri utofauti wa jamii, baada ya kukosolewa sana kuwa ilikuwa ikipendelea wazungu na wanaume.

"Nadhani tamasha hili la Oscars litakumbukwa milele kama ambalo mabadiliko yaliyofanywa miaka sita iliyopita katika chombo cha upigaji kura-- baada ya kampeni ya #OscarsSoWhite (Oscars imejaa weupe)-- yamefanikiwa baada ya ahadi ya waandaaji wenyewe," muigizaji mweusi wa Marekani anayetamba na filamu ya "Menece ll Society, Dwayne Barnes aliandika katika safu yake ya tovuti ya Deadline.

Advertisement

Wakati ni vigumu kutofautisha moja kwa moja mabadiliko katika waliotajwa kuwania tuzo mwaka huu, kuanza kwa mbio za safari hii za Oscars ni tofauti na za miaka iliyopita.

Mwaka jana, Cynthia Erivo alikuwa ni muigizaji pekee asiye mweupe katika vipengele 20, lakini safari hii marehemu Chadwick Boseman, aliyeigiza filamu ya "Ma Rainey's Black Bottom", muigizaji mweusi wa Uingereza, Daniel Kaluuya ("Judas and the Black Messiah") na nyota wa Korea Kusini Youn Yuh-Jung ("Minari") wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo.

oscarpiccc

Muigizaji mwenza wa Boseman katika filamu ya "Ma Rainey's Black Bottom", Viola Davis ni mmoja kati ya wacheza filamu wanaowania tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike, wakati Chloe Zhao, mzaliwa wa Beijing, China aliyeigiza filamu ya "Nomadland", anawania tuzo ya Muongozaji Bora akipambana na Emerald Fennell ("Promising Young Woman").

Kampeni ya #OscarsSoWhite ilianzishwa Januari 2015 katika mitandao ya kijamii kupinga uwingi wa wasanii wazungu waliokuwa wakitajwa kuwania tuzo kila mwaka.

Wakati huo, taasisi hiyo ilikuwa na wajumbe 6,000 na asilimia 93 walikuwa waepu, wakati asilimia 76 walikuwa wanaume.

Hadi katikati ya mwaka, kundi hilo liliongeza idadi ya wanawake maradufu, hadi kufikia theluthi moja, huku asilimia 19 ikiwa ya makundi ambayo yalikuwa na uwakilishi mdogo.

"Imechukua miaka michache kufanya haya, lakini kuna kila sababu kuwa na matumaini kwamba mabadiliko haya (katika kutafuta wanaowania tuzo) ni kitu cha mara moja," aliandika Barnes.

Kama ilivyokuwa katika #OscarsSoWhite, harakati za #MeToo iliyosukumwa na ufunuo wa unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na Harvey Weistein, ambaye ni maarufu Hollywood, ziliibua wito wa kutaka uwakilishi zaidi wa wanawake katika nyanja zote.

Kampeni hizo zimeongeza joto katika miaka ya karibuni, lakini zimekumbana na janga la virusi vya corona na mabadiliko ambayo hayakutarajiwa.

Janga la corona lilisababisha kumbi za sinema zifungwe na kuchelewesha uzalishaji wa filamu ambazo zingekuwa gumzo katika Oscars, kama "West Side Story" iliyotayarishwa na Steven Spielberg na "Dune," iliyoongozwa na weupe.

"Kwa kweli zilitingisha mti, na mwaka huu kwa mara ya kwanza, kwa sababu Covid-19 iliziondoa filamu nyingi kubwa... uwanja ulikuwa wazi," alisema Sasha Stone, mwanzilishi wa tovuti ya Awards Daily ambayo imekuwa ikichambua filamu tangu mwaka 1999.

Tukio la kukabidhi tuzio kwa wasanii bora litafanyika kwa kiasi kikubwa Hollywood kutokea ukumbi wa Union Station, ambao umechaguliwa ili kuwezesha waalikwa kutokaribiana, ikiwa ni njia ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya coorna.

Watakaotumbuiza nyimbo katika hafla hiyo watakuwa Hollywood lakini katika jengo jipya la makumbusho la taasisi hiyo, wakiwa eneo la paa na ukumbi wa Hollywood, wakati wasanii wa barani Ulaya watakaoshindwa kusafiri kwenda Hollywood, watakuwa katika sehemu maalum jijini London na Paris.

Advertisement