Mahakama yampokonya baba kazi ya kumtunza Britney Spears

Thursday September 30 2021
brtittypiccc
By Mwandishi Wetu

Los Angeles, Marekani (AFP). Baba wa Britney Spears amepokonywa jukumu lake tata la kumsimamia binti yake baada ya jaji wa Los Angeles kutoa uamuzi jana (Jumatano), akimaliza mzozo wa muda mrefu na wa uchungu kwa nyota huyo wa muziki wa pop.

Kuwa chini ya usimamizi maana yake Britney hakuwa na mamlaka kamili ya fedha zake wala maamuzi mengine muhimu katika maisha yake.

Katika uamuzi wa jana, Jamie Spears ametakiwa kuachia mara moja majukumu yote ya usimamizi ambayo sasa amepewa kwa muda mtu mwingine kwa maslahi ya mwanamuziki huyo, Jaji Brenda Penny alisema, akiuelezea utaratibu wa awali kuwa hauwezekani.

britypicc

"Bwana Spears anaagizwa kuacha majukumu yote ya kumsimamia (Britney)," alisema Jaji Penny.

Baba wa Britney amekuwa akiendesha maisha ya mwanamuziki huyo kwa miaka 13 iliyopita chini ya utaratibu wa kisheria ambao nyota huyo mwenye miaka 39 amekuwa akiuelezea kuwa "wa kinyanyasaji".

Advertisement

Uamuzi wa Jumatano umekuja baada ya kampeni ya muda mrefu iliyofanyika hadharani, na baada ya kuibuka kwa makala mbili nzito wiki iliyopita, zikiwa na tuhuma kwamba Jamie Spears anasikiliza simu za binti yake.

Mwanasheria wa Spears, Mathew Rosengart alimuelezea baba wa binti huyo kuwa ni "mkatili, mlevi na mnyanyasaji".

"Britney anastahili kuamka kesho bila ya usimamizi wa baba yake," alisema Rosengart. "Ni kitu ambacho mteja wangu anataka, ni kitu ambacho mteja wangu anahitaji, ni kitu ambacho mteja wangu anastahili."

Mamia ya mashabiki wake walijazana nje ya mahakama wakishangilia na walilia wakati habari za uamuzi wa mahakama zilipoibuka.

Sam Asghari, mchumba wa Spears, aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akisema"BRITNEY HURU! HONGERA!!!!!!!!!" akiweka picha inayomuonyesha mtu ambaye inawezekana ni yeye akimkabidhi uaridi mwimbaji huyo.

Katika shauri lililofunguliwa wiki hii, wanasheria wa Spears walisema: "Kila siku inayoenda yeye (baba wa Britney) akiwa msimamizi wake -- kila siku na kila saa -- ni kitu ambacho kinamsababishia binti yake maumivu na machungu."

Madai hayo yanaonekana kupewa nguvu na makala ambayo gazeti la New York Times liliitoa Ijumaa ambayo inadai kuwa Jamie Spears ana vifaa vya ufuatiliaji vilivyowekwa chumbani mwa binti yake kwa ajili ya kurekodi mazungumzo yake.

"Kwa kweli inanikumbusha mtu aliyekuwa jela," mfanyakazi wa zamani wa ulinzi aliwaambia watengenezaji makala hiyo inayojulikana kama "Kumdhibiti Britney Spears".

Wanasheria wa nyota huyo wa muziki wa pop walisema tuhuma za Times kuhusu baba yake zilionyesha "hali ya kutisha na uvamizi usiojali wa faragha ya binti ambaye ameshakuwa mtu mzima."

Jamie Spears amekanusha kufanya vitendo vya kumpeleleza binti yake kinyume cha sheria.

Makala nyingine kwenye mtandao wa Netflix ya "Britney vs Spears," iliyotolewa Jumanne -- inadai kuwa mwimbaji huyo alijaribu kuajiri mwanasheria wake binafsi mwanzoni mwa miaka ya usimamizi wa baba yake, lakini alikataliwa.

Hatimaye mwezi Julai, Spears alifanikiwa kuteua mwanasheria wake -- Rosengart -- na mwezi uliopita, baba yake alifungua shauri kupinga kuondolewa kwa usimamizi wake.

jaji huyo alimteua mhasibu John Zabel kuwa msimamizi wa muda wa majengo ya Spears, utaratibu aliosema unaweza kuendelea hadi mwishoni mwa mwaka.

Wanasheria wa Jamie Spears walipinga kuondolewa usimamizi, na kukanusha madai kwenye makala ya Times wakihoji ukweli wa ushuhuda wa binti yake kuwa usimamizi ulifikia kiwango cha unyanyasaji.

  

Advertisement