Malezi, utandawazi vyatajwa maadili kuporomoka

Muktasari:

  • Kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na vya kufedhehesha katika jamii ya Watanzania kumesababisha kilio cha kuporomoka kwa maadili kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.

  

Kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na vya kufedhehesha katika jamii ya Watanzania kumesababisha kilio cha kuporomoka kwa maadili kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.

Vitendo hivyo ni ubakaji, ulawiti, wizi na uporaji, mauaji, matumizi ya dawa za kulevya na matukio mengine ya utovu wa nidhamu.

Kukithiri kwa matukio haya kumetajwa kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo baadhi ya wazazi kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika suala zima la malezi.

Hili linadaiwa kusababishwa na mambo kadhaa, ikiwamo tabia ya wazazi kuogopa kukemea na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na watoto wao kutokana na sababu mbalimbali, hasa wadhifa.

Mambo mengine ni utajiri, nguvu na uwezo alionao mtoto, hali inayosababisha mmomonyoko wa maadili kuzidi kuota mizizi katika jamii.

Hali hiyo pia iligusiwa hata na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir katika sherehe za maulidi zilizofanyika mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Akitoa mawaidha katika sikukuu hiyo, Sheikh Zubeir alisema baadhi ya wazazi wamekuwa hawachukui hatua yoyote dhidi ya vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyotendwa na watoto wao, hali inayosababisha kuongezeka kwa uovu katika jamii.

“Wazazi tunashindwa kulea watoto wetu, hali inayosababisha panya road ambao wanafanya vitendo vya kihalifu katika jamii, inafika mahali wazazi tumewashindwa watoto wetu, mtoto anaweza kumjibu maneno machafu mama au baba yake, lakini mzazi wala hajali anacheka tu, huyu mtoto kasoma London, sasa akisoma London ndio awe jeuri kiasi hicho,” anasema Sheikh Zubeir.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Magreth John, mkazi wa Kimara ambaye ni mama wa watoto wanne, alisema hali hiyo imekuwa ikijitokeza katika jamii kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kusimama katika nafasi yao ya malezi.

Anasema pamoja na mambo mengine, wazazi wana jukumu la kuhakikisha wanawakosoa na kukemea vitendo vinavyofanywa na watoto wao ambavyo viko nje ya maadili, bila kujali rika au wadhifa alionao.

“Kuna msemo unasema, mtoto hakui kwa wazazi wake, hivyo haijalishi ana umri gani, anafanya nini au ana cheo kipi, bado wazazi wana jukumu la kukemea na kuonya maovu yanayofanywa na watoto wao,” anasema Magreth.

Anasema jambo lingine linalosababisha tatizo hilo ni hofu ya mzazi kukosa msaada kwa mtoto baada ya kumkemea juu ya vitendo fulani vya utovu wa nidhamu anavyovifanya.

Anasema hali hiyo inasababishwa kwa kiasi kikubwa na mzazi kuwa tegemezi kwa mtoto wake.

Peter Mashauri, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam ambaye ni baba wa watoto wawili anasema hali hiyo pia inachangiwa na kukua zaidi kwa utandawazi na dunia sasa imekuwa kama kijiji.

“Baadhi ya wazazi pia wanaiga malezi na tamaduni za mataifa mengine ambazo haziendani na tamaduni zetu,” anasema Peter.

Baba huyo wa watoto wawili, anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakitoa uhuru uliopitiliza kwa watoto wao bila uwepo wa mipaka, hali inayosababisha kukua wakiwa hawana hofu hata kidogo kwa wazazi wao.

“Katika malezi inatakiwa mzazi kuwa rafiki kwa watoto, lakini si kupitiliza hadi kufikia hatua ya kufanya utovu wa nidhamu,” anasema Peter.

Pia, anasema kutokana na baadhi ya wazazi kuvamiwa na ulezi wa kimagharibi, wamekuwa wakiyafumbia macho matukio hayo.

“Teknolojia na utandawazi, lazima vitumike kuleta tija na maendeleo na si madhara ya kuharibu watoto wetu na jamii kwa jumla,” anasema Peter.

Mkazi wa Kijitonyama, Badru Salum (76) ambaye ni mzazi wa watoto wanne anasema changamoto kubwa inayosababisha mmomonyoko wa maadili kwa watoto ni kutolelewa na kukuzwa katika misingi ya dini.

Anasema baadhi ya wazazi wa kizazi hiki wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuhakikisha watoto wao wanapata maarifa ya kidunia na kuweka nyuma maarifa ya kidini.

Salum anasema mtoto aliyekuzwa bila kuwa na misingi ya kidini atakosa hofu ya Mungu na akikosa hilo hawezi kujua thamani ya wazazi katika jamii.

“Vitabu vyote vinaelezea umuhimu wa wazazi katika maisha ya kila mwanadamu na umuhimu kusikiliza yanayohusiwa na wazazi,” anasema Salum.


Wanachosema wanasaikolojia

Akizungumzia jambo hilo, mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya malezi na uhusiano, Charles Nduku anasema wazazi kuogopa kuwakanya watoto wao ni hatari, hivyo inapaswa kupigwa vita kwa masilahi ya watoto na Taifa kwa jumla.

Anasema Waswahili walishasema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, hivyo moja kati ya sababu ya vijana kujihusisha na vitendo vya uhalifu na kutokuwa na nidhamu ni makosa katika malezi yaliyofanyika tangu akiwa mdogo.

Anasema vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na mtoto kwa wazazi wake vinaweza kuwa moja kati ya matokeo ya malezi aliyolelewa.

Mwanasaikolojia huyo anasema mtoto aliyelelewa katika misingi ya maadili ni ngumu kuonyesha utovu wa nidhamu kwa wazazi wake na hata watu wengine katika jamii, bila kujali wadhifa au fedha alizonazo.

“Wazazi au walezi wanatakiwa kutengeneza msingi wa kimaadili kwa mtoto kuanzia chini kujua nini kizuri cha kuiga na nini kibaya cha kukiepuka,” anasema Nduku.

Mwanasaikolojia Charles Mhando anasema ili kuondokana na hali hiyo, ni lazima wazazi wakubali kurudi katika nafasi yao na kutekeleza majukumu yao bila kujali msaada wanaopokea kutoka kwa watoto.

“Haijalishi mtoto wako ni nani au anafanya nini, wadhifa ama fedha zake pale anapofanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili wazazi wanatakiwa kukemea kwa nguvu zote,” anasema Mhando.

Anasema suala la kuwakemea vijana na watoto haliwahusu wazazi pekee, bali jamii nzima na kuongeza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupungua vitendo vya utovu wa nidhamu katika jamii.