Mapenzi ya watu maarufu yanavyofurahisha na kuhuzunisha wengi

Sunday October 03 2021
mapenzi 3
By Elizabeth Edward

mapenzi 2

Teknolojia ya matumizi ya mitandao ya kijamii imeshika kasi na umekuwa kama uwanja wa fujo kila mmoja anautumia apendavyo.

Kwa baadhi ya wenye majina makubwa, wakiwamo wasanii kwao ni tofauti kidogo, kwani watake wasitake ‘watatrend’ mitandaoni iwe kwa ‘kujiposti’ au ‘kupostiwa’ na mashabiki zao.

Licha ya kuwa si watu maarufu wote au mastaa wanaoweka wazi kila kitu chao kwenye mitandao ya kijamii, ila hivyo vichache kuna ambao wanavutiwa navyo na kutamani kuviishi.

Inaelezwa kuwa licha ya wakati mwingine wahusika kuwa na nia njema kwa kuweka wazi hata kwa uchache kuhusu maisha yao, mitandaoni kuna watu ambao siku zote mawazo yao ni hasi.

Kulingana na mwanasaikolojia Theresia Kivamba, upo uwezekano wa wahusika kupata changamoto zinazotokana na mambo yao kuwa hadharani.

Advertisement

“Inahitaji uwe umekomaa kifikra kukabiliana na yanayoendelea kwenye mitandao, kama mmeamua kuukabidhi ulimwengu uhusiano wenu. Ikitokea kashfa au msuguano unaowahusu ambao utahusisha na watoto pia kama wapo, ukubali na kuacha lipite, tofauti na hapo unaweza kujidhuru,” anasema na kuongeza:

“Kama watoto wamefikia umri wa kuelewa kinachoendelea kwenye mitandao tatizo linakuwa kubwa zaidi, kwani ni vigumu kuvumilia wanapoona wazazi wao wanashambuliwa mitandaoni,” anasema Theresia.

Hata hivyo, mshauri wa mahusiano, Deogratius Sukambi anasema kwa kiasi kikubwa utamaduni huo unatokana na msukumo wa kijamii.

“Inawezekana maisha yanayoonyeshwa kwenye mitandao si halisi, sasa wanaowafuatilia wanataka kuishi kama mastaa hao, hivyo kuna uwezekano wa wapenzi kuingia kwenye mgogoro kutokana na kutaka maisha ya watu wanaowafuatilia mtandaoni,” anasema Sukambi.

Sukambi anashauri watu maarufu kuishi maisha yao halisi, ikiwamo kufuata mila na tamaduni za kuthamini mahusiano yao na kuyaweka mbali na jamii ya mitandaoni.

Hawa wafuatao mahusiano yao ni mfano wa kuigwa na yamekuwa yakifuatiliwa kwa muda mrefu katika mitandao ya kijamii.


Lulu na Majay

Hawa ni wanandoa wapya ila wamekuwa wakifutiliwa kwa muda mrefu tangu ilipothibitika kuwa wapo kwenye mahusiano. Licha ya umaarufu wa Lulu kutokana na uigizaji, wapo wengi wanaotembelea ukurasa wake kuona mahusiano yake na hata kufuatilia mitindo yake ya mavazi.

Majay pamoja na kuweka taarifa kuhusu kazi, amekuwa pia akitupia picha za mwenza wake mitandaoni na inapobidi kuweka ujumbe anaotaka umfikie, kitu kinachowavutia wengi.


Vanessa na Rotimi

Mahusiano yao hayana muda mrefu, ila yamekuwa na mvuto kwa wengi, hii ni kutokana na namna wanavyoonyesha hadharani jinsi wanavyopendana.

Vanessa amekuwa akionyesha zawadi anazopata kutoka kwa mchumba wake huyu na hivi karibuni walitangaza matarajio ya kupata mtoto na tayari ameshazaliwa na waliweka wazi pia jina lake kuwa anaitwa Seven. Hakika kwa sasa ndiyo penzi linalofuatiliwa sana.


Aika na Nahrel

Miongoni mwa mastaa waliodumu kwenye mahusiano na hawana skendo licha ya kuuambia umma kuwa wapo pamoja ni Aika na Nahrel. Wawili hawa wanaounda kundi la Navy Kenzo wamejaliwa watoto wawili. Picha zao au za familia zimekuwa zikivutia wengi kuwafuatilia.

mapenzi 1

Shaa na Master J

Hawa pia wapo kwenye tasnia ya burudani, Shaa akiwa mwanamuziki na Master J mtayarishaji, mwanzoni walijaribu kuweka mahusiano yao nje ya macho ya watu, lakini kama ilivyo kwa wengi mapenzi hayana siri, wakati ukafika mambo yakawa hadharani. Kawaida kwa wao kupostiana au kumposti mtoto wao kwenye mitandao na wapo wanaovutiwa na wawili hawa wakiwa pamoja na kutamani kuwa kama wao.


Rayvanny na Paula

Ni miongoni mwa mapenzi mapya mjini, penzi hili limeshika kasi kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii likiwahusisha vijana hawa, Rayvanny akiwa mwanamuziki maarufu kutoka kundi la WCB, Paula akionyesha nyota yake kuelekea kwenye masuala ya mitindo.

Vijana wengi, hasa wanaochipukia wanavutiwa na wawili hawa, huenda ni kutokana na wanavyojinadi kwenye mitandao na kuonyesha namna gani wanavyopendana kiasi cha Paula kutokea kama video queen kwenye wimbo mpya wa Rayvanny. Mengi yamekuwa yakisemwa kuhusu uhusiano huu kutokana na Paula kuonekana bado binti mdogo ambaye hapaswi kuonyesha hadharani kuwa tayari ameshaingia kwenye mapenzi.

Mambo hayo na mengine yamefanya wawe wanafuatiliwa sana mitandaoni na wakati mwingine kuzua gumzo linaloweza kudumu siku nzima.


Nancy na Luca Neghesti

Kama ilivyokuwa kwa Faraja, Nancy pia umaarufu wake ulianza baada ya kubeba taji la Miss Tanzania. Ana wafuatiliaji wengi mitandaoni, kwa mfano Instagram pekee ana wafuasi 1.4 milioni, vivyo hivyo kwa mumewe mfanyabiashara na mwanasiasa Luca Neghesti. Kwa pamoja wamekuwa chachu ya vijana wengi, hasa wanaopenda maisha ya kisasa, wakionekana kuwafuatilia na kujifunza kutoka kwao.

Hawa walifuatiliwa sana, lakini mambo yalikwenda kombo


Wema na Diamond

Licha ya kwamba kuweka mahusiano hadharani ni tabia ya wengi, penzi kati ya Wema Sepetu na Diamond Platnumz linaweza kuwa na rekodi ya kugusa vijana wengi wa Kitanzania waliokuwa wakiwafuatilia kupitia mitandao ya kijamii. Mvuto wao ulikuwa wa aina yake, hata hivyo kilichokuwa na mwanzo hakikosi mwisho, penzi hili likasambaratika.


Diamond na Zari

Penzi kati ya wawili hawa lilitikisa Afrika Mashariki, lakini kama ule usemi wa Kiswahili ‘ngoma ikivuma sana mwisho hupasuka’, hatimaye kila mmoja akashika njia yake, ikiwa ni baada ya kupata watoto wawili, Latiffah na Nillan.

Wawili hawa walitengeneza mvuto mkubwa mitandaoni kutokana na namna walivyoamua kuweka mambo yao, huku umaarufu wao huko ukiongeza chachu, kwani wanafuatiliwa na watu wengi. Diamond katika mtandao wa Instagram pekee anafuatiliwa na watu 13.3 milioni, huku Zari akiwa an wafuasi 9.6 milioni, hivyo wakiweka kitu huko kinasambaa haraka. Waliachana na kuwagawa mashabiki wao, wapo waliopenda na ambao wanatamani kuwaona wakiwa pamoja tena.


Vanessa na Jux

Kabla ya kutua kwa Rotimi, Vanessa Mdee alinasa kwenye penzi la Jux, wakati huo akiwa mwanamuziki mahusiano yao yalinogeshwa na umahiri ambao kila mmoja alikuwa nao kwenye muziki, walishirikishana kwenye nyimbo kadhaa zilizowafanya kutengeneza fedha na kuongeza mashabiki ambao walipenda kuwaona pamoja. Hata hivyo waliishia kuachana.


Kajala na Harmonize

Hili linaweza kuingia kwenye orodha ya mapenzi ambayo hayakudumu kwa muda mrefu, licha ya mahaba mazito waliyokuwa wakionyesha kwenye mitandao ya kijamii. Wanaowafuatilia wapo ambao walivutiwa na kutamani kuendelea kuwaona wakiwa pamoja, ila wapo pia ambao hawakuyapenda.

‘Show off’ za kula bata, kupeana zawadi, kupiga picha na sherehe za hapa na pale ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yanawavutia waliohusudu penzi hili. Mengi yalitokea baina ya wawili hawa na kuwasababishia kubwagana.


Ruby na Kusah

Penzi la wawili hawa ni kama sinema, Kusah akiwa mtunzi na Ruby mwanamuziki ilikuwa moja ya ‘couple’ matata. Umahiri wa Kusah kwenye utunzi ukakutana na sauti yenye nguvu ya Ruby, mashabiki wakapata burudani ya aina yake na kutamani kuwaona wakiwa pamoja. Nao waliachana na kubaki historia.

Advertisement