Mashabiki wafurika kumuona James Bond katika 'No Time to Die'

Friday October 01 2021
jamesbondipivc
By Mwandishi Wetu

London, Uingereza (AFP). Mashabiki wa James Bond nchini Uingereza jana (Alhamisi) walifurika katika majumba ya sinema wakati filamu mpya ya 007 ilipoanza kuonyeshwa, ikiwa ni miezi 18 zaidi ya muda uliopangwa awali.

Majumba ya sinema yamekuwa yakiuza tiketi kwa wiki kadhaa kwa ajili ya filamu hiyo mpya ya "No Time To Die", ambayo ni ya upelelezi wa hali juu na iliyozinduliwa Jumanne jijini London, huku walioiona wakiizungumziwa vizuri.

Inatarajiwa kuwa na mauzo makubwa kuliko yote katika wiki ya kwanza tangu mwaka 2019, wakati kampuni ya kumbi za sinema za Vue ilipouza zaidi ya tiketi 270,000 na Odeon zaidi ya tiketi 175,000 za malipo ya awali.

Filamu hiyo, ambayo awali ilitakiwa itolewe mapema mwaka jana lakini ikaahirishwa kutokana na mlipuko wa janga la Covid-19, ni ya tano na ya mwisho kwa Daniel Craig, ambaye ameigiza nafasi hiyo ya James Bond kama mpelelezi.

"Ni nzuri zaidi ya uzuri. Ni safi," gazeti la The Times limemkariri mchambuzi wa filamu, Kevin Maher, ambaye ameipa hadhi ya nyota tano.

Peter Bradshaw, wa The Guardian, pia ameipa nyota tano, akisema muda wake wa saa tatu, ambao si wa kawaida kwa filamu za James Bond, umehalalishwa.

Advertisement

"No Time To Die" ni sehemu ya filamu za kampuni kubwa ambazo zilizuiwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.

Advertisement