Mastaa waliofanikiwa ‘kuwateka’ Alikiba na Diamond

Sunday September 05 2021
Mastaa pc
By Peter Akaro

Kutokana na utimu wenye lengo la ushindani katika muziki, imekuwa ni ngumu kwa wasanii na watayarishaji kufanya kazi na Alikiba na Diamond kwa wakati mmoja.

Ushindani huo unawalazimisha kuchagua upande. Kama umechagua upande wa Alikiba basi ni wazi upande wa Diamond ni ngumu kupata nafasi, maana tayari umejipambanua kama mshindani.

Hata hivyo, kuna wasanii na watayarishaji muziki wamefanikiwa kuepuka mtego huo, ingawa ni kipindi cha nyuma ambapo upinzani wa wawili hao ulikuwa haujaota mizizi kama ilivyo sasa.

Miongoni mwao ni msanii wa Hip Hop, Chid Benz ambaye miaka ya nyuma alikuwa akishirikishwa sana na wasanii wenzake kutokana na sauti yake ilikuwa inauzika kwa urahisi na kufanya wimbo husika kupendwa na wengi.

Alikiba alimshirikisha Chid Benz katika wimbo wake ‘Far Away’ ambao ulifanya vizuri kwa kiasi chake, huku Diamond akimpa shavu katika ngoma yake ‘Nalia na Mengi’, hata hivyo wawili hao hawakufanya video ya wimbo huo.

Mwingine ni Mr Blue,ambaye ana ukaribu sana na wakali hao wawili, baada ya Diamond kujiita Simba jina alilokuwa analitumia Mr. Blue, aliamua kujipa jina la Nyani Mzee ili kuondoa tetesi zilizoanza kushika kasi kuwa hilo litaleta bifu kati yao.

Advertisement

Diamond alimpa shavu Mr. Blue kwenye wimbo wake uitwao ‘Nakupa Moyo Wangu’, pia wakaja kukutana tena katika wimbo wa marehemu Ngwea ‘BBM’ ambao Chibu aliimba kiitikio. Blue akaja kumshirikisha Alikiba kwenye ngoma yake ‘Mboga Saba’ baada ya kutokea kwenye video ya wimbo wake mwingine uitwao ‘Pesa’.

mastaa pcc

Mwanamama Queen Darleen ni miongoni mwa waliofanikiwa kuwateka wakongwe hao wa bongofleva. Aliinasa sauti ya CEO wa Kings Music Ali Kiba katika wimbo wake ‘Wajua’ Darleen anasema ”Sijawahi kuona prodyuza labda wa Alikiba akifanya kazi kwa Diamond, na prodyuza wa Diamond kufanya kazi Alikiba, kweli sijaona. Nafikiri hawajapata nafasi ya wao wenyewe kupangilia hilo, lakini msanii mmoja kati yao akitaka kufanya kazi na prodyuza yeyote sidhani kama atakataka, akikataa nadhani atakuwa hayupo sawa,” anasisitiza Queen Darleen.

Mama huyu wa mtoto mmoja wa kike alifanya nyimbo mbili na Diamond n ‘Zilipendwa’ na ‘Quarantine’.

Mtayarishaji muziki Mocco Genius kutoka studio za Imagination Sound, alianza na Alikiba kwa kumtengenezea wimbo uitwao ‘Mshumaa’, akaja kutengeneza ngoma ‘Cheche’ yake Zuchu ambayo amempa shavu Diamond. Mocco anasema watu wanaogopa kufanya kazi na mastaa hao bila sababu za msingi, anachojua wenyewe hawana neno. “Hofu tu kwa sababu suala la prodyuza kufanya kazi na wasanii tofauti tofauti ndio jukumu lake la msingi,” Mocco ameliambia gazeti hili.

Kundi la Navy Kenzo linaloundwa na Nahreel na Aika, hawa ndio wamefanikiwa kupitia vizuri zaidi katikati ya zile timu Kiba na Mondi. Nahreel ndiye aliyetengeneza wimbo wa Diamond ‘Nana’ uliotoka mwaka 2015, mwaka 2017 Navy Kenzo wakamshirikisha Alikiba katika ngoma yao iitwayo ‘Lin’, mwaka 2018 wakampa shavu Diamond kwenye ngoma yao ‘Katika’, huku Nahreel akisimama tena kama prodyuza.

mastaa pccc

Mtayarishaji muziki Marco Chali, anayefanya shughuli zake MJ Records Records. alifanya kazi na vijana hao wa Kariakoo akitengeneza ngoma ya Alikiba ‘Mapenzi yana run dunia’, baada ya miaka kadhaa akazalisha ngoma ‘Kesho’ ya Diamond.

Pamoja na uhasimu wao unaotokana na ushindani wa muziki, wawili hao waliwahi kusikika katika wimbo wa Kigoma All Stars ‘Nyumbani’ baada ya Alikiba kukosekana katika ngoma ya kwanza ya mradi huo, pia wawili hao walitokea wakiwa wameketi sehemu moja kwenye video ya wimbo wa Tundaman uitwao ‘Starehe gharama’.

Advertisement