MASTORI YA OSCAR: Zama zinabadilika, lakini Kajala bado anatamba...

Thursday June 16 2022
kajalapic
By Oscar Oscar

KAJALA Masanja ni mwigizaji na mrembo aliyedumu kwenye kiwanda cha burudani kwa muda mrefu. Ni zaidi ya miaka 20 sasa Kajala ameendelea kusumbua.

Haiji tu kwa bahati mbaya. Inahitaji kujitunza kwa kiwango cha hali ya juu. Siku hizi wanaibuka warembo kila kukicha kwenye Bongo movie, lakini bado Kajala hana mbadala. Ni miongoni mwa watu wachache ambao zama haziondoki kwao.

Alikuwepo zama za analojia. Sasa tuko naye kwenye dunia ya dijitali. Watu wengi wa kwenye burudani waliochelewa kugeuka kutoka analojia kwenda dijitali wamepoteza mvuto.

Tazama mastaa wetu wa muziki. Tazama mastaa wetu wa soka. Kama ulichelewa tu kugeuka na zama, haupo tena. Hakuna kiwanda kigumu kufanya kazi kama eneo la burudani. Burudani ni mahali ambapo kila siku vinazaliwa vitu vipya.

Ni mahali ambapo ubunifu wa hali ya juu unahitajika. Leo hii nchi nzima inamzungumza Kajala, ni kwa sababu tu bado hana mbadala kwenye ulimwengu wa burudani.

Dunia ya burudani inataka mtu anayejiongeza. Iko kasi sana. Hongera sana Kajala kwa kuweza kudumu kwa miaka mingi. Unamkumbuka mwaka ulioanza kumuona Kajala kwenye ulimwengu wa sanaa na burudani? Nikumbushe kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Advertisement

Pamoja na kukaa kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 20, bado Kajala anabandikwa picha zake kwenye mabango nchi nzima. Bado Kajala anapewa zawadi ya gari mbili - tena Range Rover. Watu wengi walioanza sanaa na Kajala wameshapotea.

Kwenye gemu yupo kwa zaidi ya miaka 20, lakini bado anaheshimu watu. Amekuwapo kwa miaka mingi, lakini bado ni mnyenyekevu kwa yeyote anayepita mbele yake.

Vijana wengi wa kizazi hiki hawana tabia hiyo. Jina likishakua wanajisahau. Jina likishakua wanaanza dharau. Maisha hayataki kiburi. Maisha yanawahitaji kina Kajala. Wanakuja mabinti wadogo kwenye sanaa, lakini wanaondoka na kumuacha Kajala.

Advertisement