Mchizi Mox: kutoka ndoto ya ubaharia hadi muziki

Waandishi wa gazeti la Mwananchi, Emanuel Msabaha (wa kwanza kushoto) na Imani Makongoro (wa kwanza kulia) wakizungumza na msanii Mchizi Mox (katikati) katika mahojiano maalumu. Picha na Loveness Bernard
Kama ilivyo ada, kila mtu huwa na ndoto zake anapokuwa na umri mdogo na huimarika au kubadilika kadiri anavyokua kutokana na mazingira anayoishi. Ivyo hivyo kwa msanii mkongwe wa hip hop Bongo, Mchizi Mox anasema moja ya ndoto zake maishani ilikuwa ubaharia.
Anasema baba yake alikuwa baharia na alisafiri sehemu nyingi pamoja naye, hivyo akavutiwa na kazi hiyo, ingawa ndoto zake hazikutimia.
Mchizi Mox ni miongoni mwa wasanii wanaounda kundi la Wateule akiwa na wenzake kama Jay Moe, Solo Thang na Jaffarai, pia kuna Lady Lou na Mack 2B ambao tayari wametangulia mbele ya haki.
Akizungumza na gazeti hili, Mchizi Mox anasema ukiachana na muziki, ndoto yake nyingine ilikuwa ni kufanya biashara, ndoto ambayo anaiishi kwa sasa kupitia kampuni yake iitwayo Kivuli cha Moxie.
“Nimetimiza ndoto yangu moja ya kuwa mfanyabiashara, kwani kwa sasa ninamiliki kampuni yangu inayojihusisha na uuzaji pamoja na utengenezaji wa majukwaa katika shughuli mbalimbali,” anasema Mchizi Mox.
Utakumbuka Mchizi Mox alipata umaarufu na ngoma zake kama ‘Vipi Mambo’, ‘Bado Nipo’, ‘Mikono Juu’, ‘Demu Wangu’, ‘Mdundiko’, ‘Chupa Nyingine’ n.k, huku akishirikishwa katika ngoma ‘Mikasi’ yake marehemu Albert Mangwair.
Kuanza muziki
Je, ni lini na wapi alianza muziki mkongwe huyu aliyevuma mwanzoni mwa miaka ya 2000? Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, anatupitisha hatua kwa hatua kuhusu safari yake ya muziki, masomo, umaarufu na mengine mengi.
Anasema kwa sehemu kubwa safari yake ya muziki ilibebwa na familia yake na marafiki, alianza muziki akiwa Shule ya Msingi Lumumba na kwa wakati huo alikuwa anapiga tarumbeta, filimbi na ngoma katika bendi ya shule.
“Nilianza kuandika nyimbo zangu mwenywe nikiwa sekondari, nilikuwa ninapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa marafiki zangu, jambo lililonipa hamasa sana wakati huo kufanya kitu kizuri,” anasema na kuongeza:
“Hivi vitu vyote vya muziki ilikuwa ni baada ya masomo, tulikuwa tunafanya muziki na rafiki zangu, hasa wakati wa mapumziko, ule muda wa uwanjani ndio hasa tuliutumia vizuri,” anasema Mchizi Mox.
Akiwa ni mtoto wa kwanza kwa mama na wa tatu kwa baba yake, Mchizi Mox anasema hakukumbana na kikwazo chochote kutoka katika familia yake, mara nyingi mama yake alikuwa anampa hamasa katika kuipambania ndoto yake.
“Mama yangu alikuwa ni mtu muhimu katika safari yangu ya muziki, kwani ndiye mtu wa kwanza kunishika mkono katika sanaa yangu, na sikupata ugumu wowote kutoka kwa ndugu yeyote, hilo lilinifanya niendelee kupambania ndoto yangu ya muziki,” anasema.
Kuibuka kwa Wateule
Baadaye Mchizi Mox alikuja kukutana na Jay Moe na Jaffarai aliokuwa akiishi nao mtaa mmoja, Makumbusho, Dar es Salaam. Anasema sababu ya kukutana kwao ilikuwa ni kiu ya kila mmojawao kufanya muziki, basi wakawa marafiki wa karibu zaidi.
“Mimi pamoja na Jay Moe na Jaffarai tulikuwa tunaishi mtaa mmoja, tulizoeana kwa sababu tulikuwa tunapenda kitu kimoja ambacho ni muziki, na hiyo ndio sababu hasa ya kuwa karibu zaidi kwa kipindi hicho,” anaeleza Mchizi Mox.
Wakiwa katika harakati za muziki, shule iliwatenganisha, Mchizi Mox na Jay Moe walikwenda kusoma Mbeya ila shule tofauti, hivyo hivyo kwa Jaffarai naye akashika njia yake kimasomo ila kila likizo walikutana na kuendelea na muziki wao. “Kila mtu alikwenda shule tofauti ila wakati wa likizo tulikuwa tunawasiliana ili tuweze kurudi pamoja katika muziki, urafiki wetu unaendelea kudumu hadi leo kwa kuwa tulishafanya vitu vingi pamoja,” anasema Mchizi Mox.
Baada ya kuibuka washindi katika mashindano ya kusaka vipaji vya muziki ambapo P Funk Majani na Master J walikuwa ndio Majaji, ndipo likazaliwa kundi la Wateule.
“Tuliimba mbele ya kina P Funk Majani na tulibahatika kushinda, tukichukua nafasi ya kwanza katika muziki wa hip hop, ndipo tukaanzisha kundi la Wateule na wenzangu,” anasema.
Utakumbuka kundi la Wateule lililoanza mwaka 1998 lilifanya vizuri na nyimbo kama ‘Msela’, ‘Si Ndio’, ‘Pengo’, ‘Nipende Nichukie’, ‘Tumerudi Tena’, ‘Vile Vile’ n.k.
Maisha ya umaarufu
Mchizi Mox anasema maisha ya umaarufu kwa kawaida yana faida na hasara zake, lakini kwake ilikuwa ni jambo la kawaida, kwani ni mtu ambaye amebarikiwa kipaji halisi, hivyo umaarufu haukumbabaisha.
“Kwangu ninaishi kawaida kwa kuwa muziki hauwezi ukanifanya niwe tofauti na mtu mwingine, ninachojua ni kwamba kila mtu ana kitu anachoweza kufanya zaidi ya mwingine,” anasema Mchizi Mox.
Anasema amekuwa akifanya muziki sio kwa kutafuta umaarufu, bali ni kitu ambacho anakipenda, tofauti na sasa inaonekana baadhi ya watu wamevamia katika muziki kusaka umaarufu kwa kufanya mambo yasiyofaa.
Kuhusu muziki wa Hiphop ulivyo sasa, Mchizi Mox anasema ubunifu ni kama umepungua kidogo kwa sababu kila siku vinasikika vitu vilevile vya miaka yote, “vijana wa wakati huu wanatakiwa kuongeza ubunifu katika muziki huu.”
Upande wa maisha binafsi, Mchizi Mox bado hajaoa ila amebahatika kupata watoto wawili, wa kwanza akiwa wa kike, Halima, 13, ambaye anakipiga katika klabu ya watoto Napoli nchini Italia, na mwingine wa kiume, Jasir ambaye amempata hivi karibuni.
Kuhusu Bongofleva Honors
Akiwa mmoja wa wasanii walioanza muziki kitambo, Mchizi Mox amezungumzia tamasha la Bongofleva Honors linalofanyika kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi kwa lengo la kumpa heshima yake msanii mmoja mkongwe wa Bongofleva.
Bongofleva Honors ni tamasha lililoanzishwa na mkongwe wa hip hop Bongo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ chini ya Deiwaka World, hadi sasa limewapa heshima wasanii kama Dully Sykes, TID, Juma Nature na Jay Moe.
Anasema Sugu amefanya kitu kizuri kuwakumbuka wasanii ambao ndio waasisi wa muziki nchini, huku akieleza kwamba tasnia ilikuwa inakosa kitu kama hicho, Mchizi Mox anaamini jukwaa hilo litawapa nafasi wasanii wa zamani kuendelea kupata mashabiki wapya.
Kazi na Mangwair
Ni vigumu kusahau kile alichofanya Mchizi Mox katika ngoma ya Mangwair ‘Mikasi’ kutoka kwenye albamu yake ya kwanza, A.K.A Mimi (2004), chini ya Bongo Records.
“Mimi na Mangwair tumefanya nyimbo mbili ambazo ni ‘Mikasi’ na ‘Demu Wangu’, zote zikiwa ni uandishi wangu, japokuwa ya Mikasi mistari ya mwanzoni aliandika yeye mwenyewe,” anasema Mchizi Mox.
Ikumbukwe Mangwair ambaye alisaini Bongo Records baada ya kutoka na ngoma yake, ‘Ghetto Langu’, Mei 28 mwaka huu ametimiza miaka 10 tangu afariki dunia hapo Mei 28, 2013 nchini Afrika Kusini.
Anatajwa kuwa msanii bora wa hip hop kuwahi kutokea Bongo, akiwa na uwezo mkubwa wa kufanya mitindo huru (free style).