Mfuko wa wasanii Tanzania watengewa Sh1.5 bilioni

Saturday May 29 2021
mfukopic
By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Mfuko wa utamaduni kwa wasanii umetengewa Sh1.5 bilioni huku wasanii wakitakiwa kujiandaa kuandika madokezo ya kuomba fedha hizo kwa ajili ya kuendelea shughuli zao.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Mei 29, 2021 na kaimu mkurugenzi wa maendeleo ya sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Leah Kihimbi katika hafla ya uzinduzi wa Chama cha Waigizaji Dar es Salaam (TDFAA).

Mfuko wa wasanii ulianzishwa Novemba, 2019 katika kongamano la sanaa la mwalimu Nyerere lililofanyika jijini Dar Salaam ikiwa ni baada ya ombi la wasanii ili uwawezeshe kuendesha shughuli zao za sanaa.

Amebainisha kuwa fedha hizo zitaanza kutumika Julai 2021 huku akiwataka wasanii kujipanga kuomba fedha hizo.

"Msiogope kuomba hela mfuko ukianza kwa sababu kadri zitakavyokuwa zikitumika ndio Serikali itaona uhitaji wa kutoa au kuongeza lakini zikirudi wataona hamna haja nazo,” amesema Leah.

Akizungumzia mfuko huo mwenyekiti wa chama cha waigizaji Taifa, Chiki Mchoma amewataka wasanii kutolaza damu.

Advertisement

"Tumelia kwa muda mrefu kuhusu kukosa fedha za kuboresha kazi zetu, sasa mfuko wetu huo tayari umejazwa hela ni wakati wa kuanza kuandika madokezo kwa kuwatumia wataalam mbalimbali sio kusubiri muda ufike ndio tuanze kukimbizana," amesema  Mchoma.


Mwenyekiti wa TDFAA, Piere Mwinuka amesema wamefanya uzinduzi huo sambamba na kuja na kampeni ya 'Kipaji ni Kazi' lengo likiwa kutumia vipaji walivyo navyo kujiingizia kipato.


Kupitia programu hiyo, Mwinuka amesema wasanii watapewa elimu, kuundwa vikundi vidogovidogo ndani ya chama  na kuongeza wanachama.Advertisement