Mikataba kikwazo kwa mastaa bongo

Sunday July 24 2022
mikatbaapiic
By Peter Akaro

Hivi karibuni mwimbaji wa Bongofleva, Rayvanny ameondoka kwenye lebo ya WCB Wasafi ya Diamond Platnumz aliyodumu nayo kwa miaka sita. Nyota huyo kutoka mkoani Mbeya ni wa tatu kuachana na lebo hiyo kwa kipindi cha miaka minne baada ya Rich Mavoko na Harmonize. Pia msanii Country Boy anakuwa miongoni mwa wasanii walioachana na lebo zao baada ya kuondoka Konde Music Worldwide yake Harmonize hapo Januari.

Wasanii kuachana na lebo zao pindi wanapopata mafanikio au kushindwa kuwika limekuwa jambo lenye mjadala mpana uliojikita upande wa mikataba. Wapo wasanii wanaodai kunyonywa na lebo zao, pia zipo lebo zinazodai kupata hasara kwa uwekezaji waliofanya kwa wasanii wao.

Akifafanua nini cha kufanya katika sintofahamu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Utawala wa Taasisi ya Haki za Wasanii (Taro), Joshua Msambila anasema wasanii wanaipoingia mikataba na rekodi lebo wanatakiwa kujua mambo mawili, yakiwamo ya kibiashara na kisheria.


Kibiashara

Anasema baadhi ya wsanii hawana elimu ya biashara na wana mtazamo kwamba kazi za sanaa zinavyofanyika ni kama wanasaidiwa tu, wanasahau kuwa ile ni biashara, wote wanatakiwa kupata.

Advertisement

“Mara nyingi hii biashara inapokuwa imeanza msanii anakuwa hana kitu (fedha) ila ana kipaji ambacho bila fedha hawezi kufanikiwa. Kwa hiyo watu wanaowekeza kwake wanategemea mwisho wa siku na wao wapate faida, sio warudishe mtaji wao.

“Wasanii wengi anavyofanya mazungumzo kuelekea kusainisha mikataba hawalijadili hili, wao wanawaza kutoka kimuziki, huku mwekezaji anataka kupata faida kubwa baadaye,” anasema Wakili Msambila.

Anasema inapotokea faida imeshapatikana na mtaji wa yule aliyewekeza umesharudi, msanii anaona ananyonywa, kitu ambacho si kweli.

Anasema jambo lingine ambalo wasanii wanapaswa kuliangalia ni aina gani ya mwekezaji wanayeingia naye mkataba, kwani baadhi yao hawataki hasara, badala yake wanataka yote iende kwa msanii.

“Mfano amewekeza milioni 20 inapopatikana milioni 10 yule aliyewekeza anataka achukue fedha yote, lakini amesahau kwenye hii milioni 10 kuna kazi msanii amefanya, hivyo huwezi kuchukua yote. Vile unavyochukua faida, ndivyo uchukua na hasara,” anasema.


Kisheria

Upande wa sheria, Wakili Msambila anasema msanii anapoingia kwenye kazi ya sanaa anatakiwa kuelewa mfumo mzima wa ukusanyaji na ugawanyaji wa mapato kwa faida na hasara.

“Wasanii wengine wanaingia kwenye mikataba ambayo haipo wazi au kuwalalia kwa upande mmoja, mkataba unakuwa yule anayewekeza fedha ndio apate kila kitu. Msanii anausaini vile ulivyo, kisha baadaye akikua kisanii na kuanza kuingiza fedha nyingi huona ananyonywa.

Anasema msanii anaposaini mkataba mbaya hawezi kusema ni kosa la aliyemsainisha, maana ana jukumu la kuhakikisha hasaini mkataba hadi auelewe au atafute wataalamu wamueleweshe.

“Mara nyingi sheria yetu ya hakimiliki imetoa ahueni ndogo sana, kwamba mtu akisani mkataba akagundua unakandamiza haki zake kwenye kazi za sanaa, anatakiwa amtaarifu aliyemsainisha kisha asubiri kipindi cha miaka miwili aombe kuubadilisha na sio kuuvunja,” anasema.

“Ambao hawajaingia mikataba ni rahisi kutetea haki zao kwa sababu kuna sheria inawalinda ambayo ilitengenezwa kuhakikisha uwiano wa haki kati ya mwekezaji na msanii. Sheria yetu ya mikataba imeweka baadhi ya vipengele, lakini hivyo vyote haviwezi kutumika kama umesaini mkataba,” anaeleza.

Anasema kinachoweza kuangaliwa kama mkataba aliusaini katika mazingita halali, aidha alikuwa umelewa, mgonjwa, chizi, alidanganywa au alishurutishwa, pia una jukumu la kuthibitisha hayo, lakini kama hawezi huo mkataba utamkandamiza.

“Mkataba ni maagano ambayo yanatambulika kisheria, kwa hiyo unachokisaini kinatakiwa pia kukubalika na sheria kwa sababu kuna vitu vingine huwa havikubaliki na sheria.


Wasanii, wadau wafunguka

Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya Tanzania (Tuma), Sogy Doggy anasema wasanii wengi Bongo wanapoingia kwenye makubaliano wanakuwa na njaa tu ya kutaka kufahamika na kutembelea nyota ya lebo, lakini hawaangalii mkataba unawabana kiasi gani.

“Wakija kupata upeo wanagundua kumbe inawezekana hata wangekuwa mwenyewe, ndio wanaamua kuachana na lebo.

“Lebo inapomchukua msanii inawekeza, huku mtaani kuna wasanii wazuri kuliko ambao wapo kwenye lebo, lakini hawana jinsi ya kutoka kwa sababu hawana kipato. Kwa hiyo nikitumia fedha juu yako halafu ukapata jina ukafikia wakati wa kula matunda unataka kujitoa, tayari hiyo kwangu ni hasara, ndiyo maana unakuta hata wengine wanagombana.

Sogy Doggy aliyetamba na ngoma, ‘Kibanda cha Simu’, anasema Tuma wameweka mwanasheria ambapo mwanachama wao akitaka kusaini makubaliano yoyote yale, anaweza kuwaona.

Kwa upande wake Mtangazaji wa ‘DJ Show’ ya Radio One, DJ Nicotrack anasema wasanii wanapotaka kutoka kimuziki hawajali sana kuhusu mikataba kwa sababu wanakuwa na tamaa ya kufanikisha jambo lao.“Mara wanapobaini kile wanachoingiza kwa shoo au kazi wanayofanya ndipo wanataka kuachana na lebo zao, mwanzo wakiwa bado hawajatoka kimuziki wanakuwa hawafahamu chochote.

“Marioo pale alipo akiamua kwenda WCB atadumu kuliko wasanii waliotangulia kwa sababu alishafahamu anaingiza vipi fedha yake, waliotangulia kuingia WCB walikuwa hawana kitu au wana namba ndogo ya mashabiki wamesaidiwa baadaye wanakuja kujitambua kama wanadhulumiwa lakini siamini hivyo.

“Nimeona viongozi wa WCB wameweka wazi mikataba yao ni asilimia 60 kwa 40, lakini mbona hawajatufafanulia hizo asilimia ni baada ya mauzo au zinakatwa gharama kwanza,” anahoji. Kuhusu iwapo hilo linaweza kuwa na athari zozote kwa WCB na muziki wa Diamond, DJ Nicotrack amesema hilo linategemea wasanii wanaotoka wanazungumza kitu gani ila kwa upande wa Diamond anaonekana kama mtu anayekuza vipaji kisha baadaye vinajitegemea.


Mnyukano wa wadau mtandaoni

Katika mitandao ya kijamii WCB Wasafi imekabiliwa na ukosolewaji mkubwa baada ya wasanii watatu kuondoka katika lebo hiyo kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, miongoni mwa waliofanya hivyo ni Prodyuza wa Bongo Records, P Funk Majani. “Harmonize kishasepa, Rayvanny kishasepa, Mbosso hapewi hapewi haki ya kutambulika kama mtunzi wa nyimbo, S2kizzy na Lizer hawapewi wala hawatambuliki kwenye mfumo kama watengenezaji wa nyimbo kwa kazi zote walizobuni, asilimia 50 zao ziko wapi” “S2kizzy kakosa ‘publishing advance’ ya Dola75,000 (wastani wa Sh174.8 milioni) Sony Music kisa mmeforgi ‘publishing registration’ za nyimbo alizobuni,” aliandika Majani Instagram.

Baada ya kauli hiyo Meneja wa Diamond na WCB, Sallam SK alijibu hilo kwa kueleza; “Brother, umefanya nini kwenye industry zaidi ya kuwaooiga wasanii na kuwachukulia haki zao, sasa hivi unatetea mtu anayekulele mzazi mwenzio na mwanao au?, get your facts right!”. Hata hivyo, mwongozaji wa video Bongo, Adam Juma aliandika kuwa watu waseme yote ila heshima ya Majani kwenye tasnia ibaki pale pale vinginevyo dunia itakua nyeusi sana. “Ifike sehemu tuyajadili haya mambo kwa upana bila ushabiki na team, tusipokubali kurekebisha leo basi kesho itakua ngumu kwa kila mtu katika tasnia ya mziki. Inawezekana Majani katumia jukwaa sio sahihi kutoa shutuma hizi ila alisemalo linawezekana lina ukweli kwa nafasi alizonazo katika muziki. “Kumbuka tu yeye ni mmoja ya wajumbe wa kamati ya wadau ya Cosota iliyoteuliwa na Waziri juzi tu, anachosema je kina ushahidi? Hamna mwenye chuki binafsi au kutamani maendeleo ya mtu mwingine,” aliandika Adam Juma.


Cosota wafafanua

Ofisa wa Idara ya Leseni na Uaramia kutoka Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota), Devis Kalokola amefafanua kuwa msanii anapokwenda kusajili nyimbo Cosota inaonyesha asilimia za malipo kwa kila aliyehusika na hilo linalindwa na mkataba na sio makubalino ya mdomo.

“Kumbuka msanii anapoingia studio akamlipa prodyuza anacholipia ni studio session sio ule mdundo, kwa hiyo prodyuza anaweza kusema nitamiliki asilimia 30 za wimbo huu, aliyeandika atapata asilimia 20, mimi msanii niliyeimba asilimia 30 na hao wengine asilimia 20,” anasema.

“Ule muziki ukiuzwa fedha ikapatika, tutazigawa kama ilivyoainishwa mwanzo kwa asilimia, mfano ni 100,000 na aliandika prodyuza atapa asilimia 30, ina maana tutampa 30,000,” anasema Kalokola.

Anasema katika hilo lazima mkataba uwepo na prodyuza awe nao unaoeleza anapozalisha kitu hiki atakwenda kumiliki nini na nini hasa.

“Sio makubaliano ya mdomo, maproduza wengi wamekuwa na makubaliano ya kishkaji, inatakiwa mkataba. Sisi ukileta muziki wako tunakuambia tuletee mkataba wa prodyuza kama huna chukua hii fomu mpelekee ajaze utuletee tuonyeshe umiliki ulivyo,” anasema Kalokola.

Advertisement