Miss East Africa kupatikana Novemba 26, waandaaji wapania

Tuesday August 31 2021
miss pic

Miss Rwanda 2016, Jolly Mutesi (watatu kutoka kushoto) akiwa na warembo mbele ya gari ambalo mshindi wa Miss East Africa 2021 atapewa kama zawadi. PICHA NA SUNDAY GEORGE

By Muyonga Jumanne

Dar es Salaam. HATIMAYE kimeeleweka Novemba 26 mrembo wa Afrika Mashariki atapatikana na kuondoka na gari lenye thamani zaidi ya Sh100 milioni.

Katika shindano hilo nchi 16 za Ukanda wa Afrika Mashariki zitatoa washiriki ambao watachuana katika nchi mwenyeji ambayo ni Tanzania huku waandaaji wa shindano hilo, wakiwataka wenye sifa kujitokeza kushiriki.

Rais wa Kampuni ya Rena Events ambao ni waandaji wa shindano hilo, Rena Callist amesema mshindi wa kwanza wa shindano hilo atajinyakulia zawadi ya gari ya kisasa aina ya Nissan Xtrail lenye thamani ya zaidi ya Sh100 milioni.

miss pic 1

 “Mshindi wa pili atajinyakulia Sh11 milioni na mshindi wa tatu atapata Sh5 milioni. Pia kutakuwa zawadi nyingi mbalimbali kwa washiriki mashindano haya zenye thamani ya Sh20 milioni,” alisema Callist.

Callist washiriki wengine ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somali na Malawi ni miongoni mwa mataifa yaliyothibitisha kushiriki kinya’nga’nyiro hicho.

Advertisement

“Mashindano yatarushwa moja kwa moja na kuangalia na watu milioni 300 kupitia runinga na mitandao ya kijamii. Tanzania itafaidika na mashindano haya kwa kutangaza vivutio vya kitalii,” alisema Callist.

Callist alisema miongoni mwa vigezo ni pamoja na mshiriki awe raia wa husika, umri wa miaka 18-26, uwezo wa kujieleza kwa ufasaha. Alisema kwa warembo wenye sifa wanaotaka kushiriki shindano hilo watajaza fomu maalumu zitakazopatikana katika mtandao.

Makamu wa Rais wa kampuni hiyo, Jolly Mutesi alisema mashindano hayo yatakuwa tofauti hivyo kuwataka watu kufuatilia kujionea vitu vingi.

Jolly ambaye ni Miss Rwanda 2016 alisema warembo watakaoshiriki watafaidika na mambo mbalimbali ikiwemo kupata elimu na kujiamini.

Kaimu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Matiko Mniko aliipongeza kampuni hiyo kwa kuuandaa shindano hilo, akisema baraza hilo litawaunga mkono kwa kila hatua katika mchakato huo.

“Wote wenye sifa wajitokeza kugombea, Basata litasimamia masuala yote ikiwemo mikataba na zawadi zitakazotolewa kwa washindi na washiriki,” alisema Mniko.Advertisement